Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Massawe akitoa ufafanuzi namna Serikali livyojipanga kukabiliana na ugonjwa wa Ebola mkoani humo kwa kuongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalam wa afya wanaofanya kazi ya uchunguzi wa dalili za ugonjwa huo walioko katika vituo vya ukaguzi mpakani.
Afisa Afya wa Kituo cha ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi Bw. Amos Mangaluke akipitia fomu zilizojazwa na raia kutoka nje ya nchi wanaotumia mpaka huo kufuatia zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za ugonjwa wa Ebola linalofanyika kituoni hapo.
 Picha na 3. Ofisi ya Uhamiaji ya Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Kizuizi cha magari katika mpaka wa Kabanga unaotenganisha Tanzania na Burundi, Wilayani Ngara..

Na Aron Msigwa – MAELEZO, Kagera.

Mkoa wa Kagera umechukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola kwa kuongeza nguvu katika udhibiti na ukaguzi wa raia wa kigeni kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaoingia nchini Tanzania kupitia vituo vya mpakani vya mkoa huo.

Akizungumza katika mahojiano maalum wilayani Ngara, Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Massawe amesema kuwa kufuatia hali hiyo serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeongeza vifaa kinga na kuwawezesha kielimu wataalam wa afya walioko katika hospitali za mkoa huo na vituo vya ukaguzi mpakani.

Amesema kuwa mkoa huo kijiografia unapakana na nchi tatu zikiwemo Uganda kwa upande wa Kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi na kuongeza kuwa mkoa kupitia kamati za Afya na wataalam wa afya walioko maeneo yote ya vituo vya ukaguzi wanafanya kazi zao ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa kila anayeingia nchini kupitia vituo hivyo anachunguzwa dalili za Ebola.

“Mkoa wa Kagera kama tunavyojua unapakana kwa karibu sana na nchi za Burundi, Rwanda na Uganda, kuna mwingiliano mkubwa sana wa watu kutoka eneo moja kwenda jingine hapa lazima tuchukue tahadhari kubwa , ninawahakikishia wananchi kuwa tumejipanga vizuri katika kuimarisha uchunguzi kupitia kamati zetu za afya” Amesisitiza.

Amesema kufuatia uwepo wa ugonjwa huo katika nchi ya jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uongozi wa mkoa kupitia kamati ya Afya na ile ya Ulinzi na Usalama unaendelea kuwaelimisha wananchi kupitia vituo vya mbalimbali vya radio vya mkoa huo kuhusu dalili za ugonjwa huo , namna ya kujikinga na namna ya kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Kwa upande wake Afisa Afya wa Kituo cha ukaguzi cha Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi Bw. Amos Mangaluke akizungumzia hali ya ukaguzi wa raia wanaoingia nchini kupitia mpaka huo amesema kuwa zoezi la uchunguzi wa dalili za awali za ugonjwa wa Ebola linafanyika kwa ufanisi mkubwa kufuatia kituo chake kuwa na vifaa kinga vinavyomsaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema takribani watu 500 wanaotumia mpaka huo wa Kabanga huchunguzwa afya zao kwa siku ambapo hujaza fomu maalum ya taarifa ambayo hutumiwa na wataalam wa afya kituoni hapo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: