Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe amesema Katiba inayoandaliwa siyo lazima ipatikane kwa sasa kutokana na hofu ya kukosekana kwa maridhiano yanayoendelea kujitokeza miongoni mwao na wajumbe wanaosimamia muundo wa serikali mbili.

Kauli hiyo imekuja takribani siku nne tangu Wajumbe wa Ukawa wasusie vikao vya Bunge kutokana na mvutano unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa Serikali.

Akizungumza jana nagazeti hili, Mbowe alisema hatua iliyofikiwa kwa sasa ni mbaya kutokana na mpasuko unaoendelea kukomaa, hivyo ni vyema kusubiri kuliko kupitisha muundo wa serikali mbili.

Kwa hali ilivyo sasa, Watanzania wanatakiwa kuwa wavumilivu, kwa sababu Katiba ni maridhiano, Kenya walitumia miaka 11 kupata Katiba yao kwa hivyo siyo lazima tupate Katiba hii katika uongozi wa Rais Jakaya Kikwete,” alisema na kuongeza:

“Tunachohitaji ni maridhiano, hatuwezi kubakia na muundo wa serikali mbili ikiwa ni tofauti na mahitaji ya Watanzania. Wazanzibar wamelala miaka mingi kukandamizwa na Serikali ya Muungano, lakini bado inashindikana hivyo tutaendelea kutafuta mwafaka zaidi mpaka tutakaporidhiana.”

Mbowe alisema hoja kuu inayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na aina ya muundo wa serikali unaohitajika kwa Watanzania.

“Katiba ni zaidi ya muundo wa serikali, lakini lazima tuangalie Social Contract’ (makubaliano ya kijamii), nchi haiwezi kutawalika kwa muundo ambao haukubaliki kwa wananchi wake ndiyo sababu ya kuvutana katika hoja hii,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ukawa inapinga hoja ya serikali mbili kwa sababu ndiyo muundo ambao umesababisha Wazanzibar leo hii wasiwe na amani kwa sababu ya kumezwa na muungano. Kwa hatua hii ni lazima maridhiano yakapatikana na siyo lazima Katiba ipatikane kwa wakati huu, inahitaji uvumilivu wa miaka mingi kama ilivyokuwa kwa Kenya.” 

Habari kwa hisani ya Mwananchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

1 comments:

  1. Kweli mbowe amekuwa popo Leo anasema katiba Siyo lazima tena?Mbona anaweka ulimi piano ndugu zangu watanzania.pimeni wenyewe

    ReplyDelete