Jana ijumaa ya Januari 17, 2014 majira ya saa 7 mchana ilikuwa ya nderemo na vifijo kwa familia ya rais Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kijana wake Miraji Kikwete kuachana na ukapera na kuamua kumpata mwezi wake wa maisha Bi. Alma Mahmoud. Harusi hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.

Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita kiasi ambapo hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi maalumu, hata angeomba kwa kupiga magoti.

Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo, isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa Serikali ambao walipewa vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera huku wamevalia kanzu nadhifu.

Hata hivyo, mbali na kunyimwa kuingia waliweza kutumia mbinu kupata picha za maharusi hao pamoja na matukio.

Miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba.

Mwenyezi mungu awajalie maisha mema ya ndoa, Miraji Kikwete na mkeo Alma Mahmoud.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

1 comments: