Dk. Ali Mohamed Shein: “Zanzibar Serikali yenye mamlaka yake kamili”
..Azindua rasmi maadhimisho ya Miaka 37 ya kuzaliwa CCM
..Amnadi Mahmoud Thabit Kombo

Na Andrew Chale, Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amesema Zanzibar itaendelea kusimama imara katika kushughulikia mambo ya Taifa na Kimataifa bila kutekeleka, kwani ni nchi na yenye mamlaka kamili na yeye ndiye Rais anayetawala.
Dk. Shein alisema hayo jioni ya jana (Januari 26), kwenye mkutano wa nne wa hadhara wa cham,a hicho katika kumnadi mgombea wa Uwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo, uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Kiembesamaki, sambamba na kufungua rasmi sherehe za maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa CCM.

Akihutubia umati mkubwa wa wanachama wa chama hicho sambamba na wananchi waliofurika kwenye uwanja huo wa mpira wa Kiembesamaki, Dk. Shein aliwapongeza wazanzibar kwa kuitikia wito kwenye sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ambazo zilifahana na dunia nzima ilizitambua na kuwapongeza ambapo aliwabeza watu wachache ambao hawataki kuona Zanzibar wanafikia malengo yao.

“Kwanza nawapongezeni kwa kuitikia wito wa sherehe zetu za Miaka 50 ya Mapinduzi zilizomalizika hivi karibuni na hii inafanya tuwaenzi kwa vitendo wazee wetu na viongozi walifanikisha hilo kuanzia vyama vya Afro Shiraz party, ASP, TANU na baadae CCM, hili si dogo na si la kubezwa kwani bila wao Muungano huu usingefikia hapa’ alisema Dk. Shein.

Na kuongeza kuwa, Licha ya wapinzani na watu wachache kubeza maendeleo, mafanikio na umoja wetu katika suala hili la Muungano, wanatakiwa kubezwa kwani hawatambui, kwani wao wanasimamia sera na Ilani ya chama katika utekelezaji na maendeleo yanaonekana, hadi chama kufikia ukubwa wa miaka 37, na miaka 50 ya Muungano.
“Leo Januari 26,nafungua rasmi, maadhimisho ya Sherehe za miaka 37 ya kuzaliwa kwa chama chetu, ambacho kilianzia Visiwani Zanzibar. Hii ni nafasi ya kipekee kwetu na tunawaomba tuendeleze mshikamano” alisema Dk. Shein.

Pia alisema licha ya kusherehekea miaka 37, ambapo kilele chake kinatarajia kuwa, Februari Mbili, huku maadhimisho ya kufunga sherehe hizo zikitarajiwa kufungwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Aidha, akizungumzia suala la Zanzibar kuwa na Mamlaka Kamili, Dk. Shein aliwataka wananchi kupuuza watu wachache ambao wanadai kuwa Zanzibar haina Mamlaka kamili.

Akiongea kwa umakini na kutilia mkazo suala hilo, Dk. Shein alisema Zanzibar ni nchi kamili na yenye mamlaka yake kama nchi nyingine na inatambulika na Serikali zote duniani. “Zanzibar ni nchi na Inaserikali yenye mamlaka yake kamili inayojitegemea. Tuna bunge letu, Tuna bendera, Tuna wimbo wetu, Tunakatiba yetu na Tuna Rais…na Mimi ndiye Rais wake’ alisema Dk. Shein hali aliyoinua shangwe na vigelegele kwa wananchi waliofurika uwanjani hapo.

Na kuongeza kuwa, vitu vyote hivyo vinaifanya Zanzibar kuwa na mamlaka yake ambapo kupitia Muungano, ambnao hadi sasa umeweza kudumu kwa miaka 50, ni ishara tosha kuwa viongozi waliotangulia watenda vyema majukumu yao na waliopo sasa wanaongoza misingi ile ile iliyoachwa bila kuvunja huku akiwataka wananchi kuelewa kuwa, CCM itaendelea kuunga mkono mfumo wa Serikali mbili kama imnavyoeleza kwenye sera yao ya mwaka 2010-2020.
“Tutaendelea kushikiria mfumo wa Serikali mbili, kama Sera na Ilani ya chama ya mwaka 2010 hadi 2020, hii ni sisi tunataka hivi, na hao wanaosemasema nao wanachama chao na wanasera yao waseme watakavyo, lakini sisi ni hivi hivi tunataka Serikali mbili” alisema Dk. Shein.

Katika mkutano huo, pia alimnadi, mgombea wa jimbo hilo nafasi ya uwakilishi, Mahmoud Thabit kombo ambapo aliwataka wananchi wa jimbo hilo la Kiembesamaki, watumie nafasi yao vizuri kumchagua Mahmoud Thabit Kombo ili aende kuwawakilisha kwenye baraza la Katiba na maendeleo mbalimbali ya jimbo hilo.

Kwa upande wake, katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana alisema kuwa, CCM itaendelea kutawa na hilo halina ubishi kutokana na kusimamia sera na misingi thabiti ya sera na ilani ya chama.

“Nawapongezeni kwa miaka 50 ya Mapinduzi, na nina waahidi, Aprili kabla ya Miaka 50 ya Muungano, nitafanya ziara ya Zanzibar nzima Unguja na Pemba, kuanzia mtaa, kitongoji, Kata, wilaya mkoa na Taifa ilikuendelea kuamsha hali ya chama” alisema Kinana.

Aidha, kwa upande wake, Mahmoud Thabit Kombo aliwaomba wananchi wa jimbo hilo, kumpigia kura hiyo Februari mbili, ili akawawakilishe kwenye Baraza la Wawakilishi.

“Nawaomba Wanakiembesamaki, kutumia fursa ya kipekee ya kunichagua ilikuweza kuwawakilisha kwenye Baraza, hakika chama chetu ni sikivu na daima kipo na wananchi katika kuwatetea na kuwaletea maendeleo” alisema, Mahmoud.

Kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiembesamaki, zilianza rasmi Januari 21, ambapo zinatarajia kufungwa rasmi jioni ya Februari Mosi, mwaka huu huku wananchi wakitarajia kupiga kura ya chaguzi huo, Februari mbili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: