Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa michuano ya taifa ya kikapu (Taifa Cup) kwa mwaka jana, bado hawajathibitisha ushiriki wao katika michuano ya mwaka huu kutokana na ukata wa fedha.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka kwa mabingwa hao wa mwaka jana ambao ni Mkoa wa Tanga, mpaka sasa timu yao inafanya mazoezi bila matumaini ya kuelekea mjini Mbeya itakapofanyika michuano hiyo kwa mwaka huu mwishoni mwa mwezi wa 11.
“Michuano hii ya kikapu taifa kwa mwaka jana ilifanyika mkoani hapa (Tanga), hivyo ikawa rahisi kwetu kuweka kambi na kupata mahitaji mengine, ndiyo maana tukaibuka mabingwa, lakini mwaka huu hali katika kambi si nzuri kwani bajeti inatubana mpaka sasa hatujui mustakabali wetu,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Tanga (TRBA), Carlistus Zakaria timu hiyo inahitaji kiasi cha Sh mil 11, ili kuweza kusafiri mpaka Mbeya. Vilevile kiasi hicho cha fedha kitaweza kuhudumia kambia kwa malazi na chakula pamoja na vifaa vya michezo kwa muda wote watakaokuwa Mbeya.
“Timu yetu ina wachezaji 24 Wavulana na Wasichana pamoja na viongozi wanane hivyo kufanya idadi ya watu 32, tunahitaji kiasi cha Sh mil 3.5 za nauli kuenda na kurudi, Sh mil 5.2 za chakula kwa siku zote tutakazokuwa Mbeya pamoja na Sh mil 8.8 za vifaa vya michezo na fedha za dharura,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Aidha kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho kimetaka hifadhi ya jina lake mpaka sasa Mkoa wa Tanga, haujaonyesha nia ya kuwasaidia mbali ya kuwapelekea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), ambayo inaweka wazi kila kitu juu ya ushiriki wetu.
“Kinachotutia uchungu juu ya kupuuzwa huku ni kuwa, mwaka jana tulipouletea heshima Mkoa wetu kila mtu alitusifia, lakini hawakujua kama vizuri vyataka gharama. Sasa ili tuendelee kuuletea vikombe mkoa wetu tunawaomba wadau wa mchezo huu watusaidie tufike Mbeya.
“Tumeamua hatuhitaji fedha, hata wakitokea watu wakitudhamini usafiri, wengine wakatupa vifaa na wengine wakatuhakikishia chakula hatuna matatizo, kikubwa tunahitaji kushiriki michuano hii kwa hali na mali, tukishindwa kushiriki itakuwa aibu kubwa kwa mkoa wetu,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa barua ya TBF, iliyotolewa Aprili mwaka huu na kutiwa saini na Katibu Mkuu Msaidizi wa shirikisho hilo Michael Maluwe, imeweka wazi kuwa Serikali ya Mkoa inawajibika moja kwa moja kuhakikisha timu hizo zinashiriki michuano ya Taifa Cup.
“Ni wajibu wa kila mkoa kuhakikisha unawajibika katika maandalizi na kuipeleka timu ya mkoa kwenye kituo cha mashindano,” imesema sehemu ya barua hiyo na kuongeza kuwa. “Mambo muhimu ya kuzingatia ni gharama za nauli kwa timu, gharama za malazi na chakula vilevile usafiri wa ndani, posho na ada ya ushiriki ambayo ni Sh 100,000.”
Aidha timu ya kikapu ya Tanga imeweka wazi kuwa mtu binafsi, kampuni ama taasisi ambayo itaguswa na matatizo ya kambi hiyo, ambayo inapigana kuhakikisha inatetea ubingwa wake ilioupata mwaka jana wanafungua milango kupokea msaada wowote utakaowawezesha kuishi mjini Mbeya kuanzia Novemba 30 mpaka Disemba 8 mwaka huu itakapokamilika michuano hiyo.
Wamebainisha kuwa wapo tayari kutangaza biashara ya mfadhili yeyote atakayewasaidia ama mtu aliyeguswa anaweza kuwatumia fedha katika akaunti ya benki namba 4172506984 NMB Bank (badaraka Branch).
Toa Maoni Yako:
0 comments: