Tigo Tanzania kwa njia ya teknolojia za simu za mkononi imeendelea kuchangia jitihada za serikali na mamlaka ya mapato nchini TRA katika kutimiza azma yake ya kuongeza makusanyo ya GDP nchini kufika asilimia 19.9 kwa mwaka ndani ya miaka mitano ijayo.
Katika mikakati yake yakuwapatia serikali njia rahisi na za kibunifu za kukusanya mapato nchini, mwezi Oktoba mwaka 2010 kampuni ya simu ya Tigo ilianzisha huduma maalum ya kutuma na kupokea pesa ambayo imewawezesha maelfu ya watu na makampuni mbali mbali kufanya miamala kupitia simu zao za mkononi jambo ambalo limeondoa ulazima wa mtumaji na mpokeaji wa fedha kuwa katika sehemu moja. Huduma hii pia imeanza kushamiri kwa walipa kodi wanaoutumia kama njia rahisi yakulipa stahili zao kwa serikali.
Kutokana na maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Bw. Diego Gutierrez, mabenki nchini Tanzania yanawafikia asilimia 10 mpaka 12 tu ya watu ndani ya mzunguko wa kifedha ambayo ni sawa sawa na kuacha asilimia 80 ya Watanzania bila huduma zozote za kibenki.
“Tigo kupitia teknolojia yake ya kutuma na kupokea pesa inaweza ikasaidia ipasavyo serikali na mamlaka yake ya mapato (TRA) kukusanya mapato yake kiurahisi na kiufanisi zaidi, hususan katika soko la watu ambao wako mbali au hawana namna ya kupata huduma za kibenki zitakazowawezesha kulipa kodi katika kipindi hiki ambapo kuna watumiaji wa simu mara nne zaidi ukilinganisha na watu wenye akaunti za kibenki nchini. Wateja hawa wa simu kwa mara ya kwanza wanapata fursa ya kipekee yakulipia kodi kupitia mfumo wa kidijitali,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mpaka sasa Tigo ina wateja milioni 2.6 wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa, ambayo ni asilimia 42% jumla ya wateja wote wa Tigo nchini.
“Kila siku, kupitia njia rahisi yakutumia kiganja cha simu tunatoa fursa kwa wateja wetu milioni 6 kulipia leseni ya barabarani (road license), kodi za mapato (income tax), VAT, pamoja na excise duties. Tayari mpaka sasa Tigo inawezesha ukusanyaji wa mapato cha kiasi cha milioni 800 kwa mwezi kwenye kodi ya leseni za barabarani (road license), pia kwa sababu tunaelewa umuhimu wa aina hizi za kodi, ndio maana tupo tayari pia kutoa huduma aina hii kwa kodi zingine kama (kodi za mapato (income tax), VAT na excise duties.) pale ambapo idara husika zitakapo kuwa tayari kupokea mapato kwa njia hii,” alisema Bw. Gutierrez.
“Kwa sababu mtandao wetu hivi sasa imejipenyeza mpaka vijijini, suluhu hii ya kidijitali ya makusanyo ya mapato inaweza ikatumika mahali popote nchini. Tunachojaribu kufanya ni kutengeneza njia mbadala wakutumia fedha taslimu pale ambapo kunahitaji la kulipa kodi, kwa kutoa mbadala ambao ni bora zaidi kuliko utumiaji wa fedha taslimu, kwa kifupi tunafanya fedha kuwa ya kidijitali, kitu ambacho kinampa mteja urahisi na ufanisi wa kulipia kodi zake,” alisema.
Kutokana na mkakati wa TRA wa ‘kufanya ulipaji kodi kuwa rahisi’, Tigo Tanzania imejikita katika huduma ambayo inaruka vizuizi vya muda na mahali, sifa ambayo inawezesha urahisi, ufanisi, usalama, uwazi na namna bora ya ukaguzi wa mahesabu kwa mlipaji kodi ambaye haitaji tena kwenda umbali mrefu au kusimama katika foleni katika ofisi za TRA kwa ajili ya kutimiza wajibu wake. Hii ina maanisha badala yake anaweza akatumia muda wake vizuri zaidi akijikita katika kufanya biashara zake na kuchangia uchumi wa taifa letu.
Sababu ingine ya kuwa na mfumo wa aina hii ya kidijitali ni kwamba muamala unakua wa haraka na wa papo kwa papo kwa watu wote wawili, mlipaji na mpokeaji wa fedha hizo, kwa sababu njia hii haina mlolongo mrefu kama zilivyo taratibu za kibenki, ambapo miamala inaweza ikafanyika kwa wingi, moja kwa moja na kuingia katika kumbukumbu za TRA, urahisi ambao unawapa mamlaka hiyo ya mapato uwezo mkubwa zaidi yakufanya miamala papo kwa papo.
“Tumejipanga ipasavyo kuwezesha ulipaji na ukusanyaji wa mapato makubwa yenye thamani ndogo ndogo katika mpangilio ambao ni mrahisi, wa wazi, salama, na wenye kukagulika kimahesabu, kwa maana hiyo huduma zetu ni za uhakika zaidi,” alisema Gutierrez.
Mpango wa Tigo Tanzania kujikita kutoa suluhu za kidijitali katika namna za kiuchumi nchini Tanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa kodi kutoka biashara ndogo ndogo na za kati pamoja na kwa watu mmoja mmoja kupitia utaratibu maalum ambao imejiwekea wa gharama nafuu na wa uhakika, ni udhihirisho tosha wa uamuzi wake wa kusaidia serikali na mamlaka ya mapato.
Mfano wa huu unafuu wa gharama na urahisi unakuja pale ambapo gharama ya muda, usafiri na pilika zingine anazopata mteja akiwa anakwenda kulipia kodi unapungua pale ambapo mlipa kodi akitumia simu yake ya mkononi kulipia kodi zake bila ya kuingia gharama na usumbufu wote huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tigo pia alisema kwamba uzuri mwingine wa kutuma na kupokea pesa kupitia Tigo ni kwamba utaratibu huu unatunza kumbukumbu za kudumu na kuweka historia ya miamala yote ambazo zilikwisha kufanyika. Utaratibu huu unasaidia TRA na mteja wake kuwa na mpangilio maalum wa kumbukumbu ambazo zinaweza zikapunguza kesi za kutofautiana kimahesabu.
“Tigo ina rekodi za kisasa za risiti na malipo yote, kwa sababu tunathamini utawala bora, uwajibikaji na uwazi kama kampuni, miiko ambayo inatuongoza katika biashara zetu za kila siku,” alisema.
Kupitia mpango wake wa kuendelea kuwekeza nchini, kupanua mtandao na kuboresha ubora wa huduma zake, Tigo inaendelea kuweka kipaumbele katika teknohama ili kuweza kuwawezesha serikali na mamlaka ya mapato nchini kuendelea kuwafikia idadi kubwa zaidi ya Watanzania kupitia huduma yake ya kutuma na kupokea pesa inayofika katika mikoa yote 30 nchini panapopatikana mtandao wake.
“Tunaamini kwamba aina hii ya ubunifu na suluhu za kudumu utaendelea kuwachangia serikali na mamlaka yake kufikisha malengo yake yakufanya suala la ukusanyagi wa kodi kuwa wa gharama nafuu, mrahisi na bora zaidi huku ikizidi kukusanya mapato zaidi ya thamani kubwa zaidi nchini,” alimalizia kusema Bw. Gutierrez.
Toa Maoni Yako:
0 comments: