Muimbaji maarufu nchini Tanzania Bi. Stara Thomas akiwasilisha ujumbe kwa njia ya uimbaji kuhusu umuhimu wa matumizi ya Takwimu katika kupanga mipango ya Maendeleo leo jijini Dar es salaam.
Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi nchini Thobias Andengenye ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuhusu mchango wa takwimu katika kufanikisha majukumu ya Jeshi la Polisi nchini.
 Naibu Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya akizungumza na wadau wa sekta mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza kabla ya ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika. Amesema kuwa Ofisi yake pamoja na majukumu mengine inaendelea kuhimiza matumizi ya takwimu kutoka katika vyanzo sahihi kwa mipango ya maendeleo.
Sehemu ya washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa leo jijini Dar es salaam.---
Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam.

Ikiwa ni takribani miaka 20 tangu kuasisiwa kwa Siku ya Takwimu Afrika, Serikali imesema ipo haja ya kufanyika kwa tathmini ya ufuatiliaji wa takwimu zinazotolewa na mchango wake katika kupanga mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yaliyowashirikisha wadau wa sekta mbalimbali leo jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya amesema kuwa maendeleo bora huchangiwa na upatikanaji na matumizi ya takwimu Bora zenye kuelezea uhalisia wa jamii husika.

Amesema Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazothamini mchango wa takwimu katika maendeleo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa matumizi ya takwimu sahihi yanapewa kipaumbele katika kutatua kero mbalimbali nchini zikiwemo za ulinzi wa raia na mali zao, elimu, Afya, Kilimo na ufugaji.

Bi. Saada amesema kuwa kutoakana na umuhimu wa takwimu wapo baadhi ya watanzania wanaodhani kuwa takwimu zinatumiwa na serikali pekee jambo ambalo si sahihi na kuwataka kuondoa fikra hizo kutokana na umuhimu na mchango wake kuanzia ngazi ya familia.

“Ni vema sote tukaelewa matumizi ya takwimu sahihi na mchango wake katika maendeleo kuanzia ngazi ya familia pia kuondoa mtazamo kuwa takwimu zinatumiwa na serikali pekee na kusahau kuwa takwimu zinagusa maisha ya kila siku ya watu na zina umuhimu mkubwa sana katika kupanga mipango ya maendeleo” Amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza kabla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo amesema kuwa Tanzania kama zilizvyo nchi nyingine za bara la Afrika huadhimisha Siku ya Takwimu Afrika kwa kuwa Ofisi yake pamoja na majukumu mengine inaendelea kuboresha na kuimarisha matumizi ya takwimu nchini.

Dkt. Chuwa amesema kuwa takwimu ni maisha ya kila siku ya mwanadamu na zina umuhimu katika nyanja zote na kuongeza kuwa wabunge wanahitaji takwimu ili kupanga mipango ya maendeleo ya majimbo yao, serikali nayo inahitaji takwimu ili iweze kutekeleza mipango ya maendeleo na kutoa huduma stahiki kwa wananchi vilevile mashirika mbalimbali yanahitaji takwimu sahihi ili yaweze kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bw. Thomas Daniel Witz akitoa salam za Benki ya dunia wakati wa maadhimisho hayo amesema kuwa Benki ya dunia na washirika wa maendeleo wanatambua na kuthamini mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu nchini Tanzania.

Amesema takwimu zinazotolewa zinaongeza uwazi na uwajibikaji na kuongeza uwezo wa nchi kupanga mipango ya maendeleo kwa wananchi wake.

“Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa maendeleo na mafanikio makubwa ya utoaji wa takwimu ambazo sasa zinaiwezesha serikali na wadau kupanga mipango yao ya maendeleo”

Naye Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi nchini Thobias Andengenye ambaye alikuwa miongoni mwa wachangiaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini amesema jeshi la polisi linathamini mchango wa takwimu katika kufanikisha majukumu yake.

Amesema takwimu zinalisaidia jeshi la polisi kutekeleza majukumbu mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa vituo vya polisi, kurahisisha mgawanyo wa ajira kufuatana na mahitaji ya wilaya na mikoa, uimarishaji wa mafunzo kulingana na uhitaji pamoja na kutambua ongezeko la makosa na namna ya kukabiliana nayo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: