Ikiwa ni miezi sita tu tangu kuanza kwa mwaka wa biashara unaoanzia tarehe 1 Aprili 2013, kampuni ya Vodacom Tanzania imetangaza kulipa kodi ya kampuni ya shilingi bilioni 29.2/= kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Rene Meza, amesema, malipo ya kodi hiyo ni asilimia 86% ya malipo ya mwaka wa fedha wa 2012 ambapo kampuni hiyo ililipa Bilioni 15.7 kwa kipindi cha nusu mwaka.

Meza amesema kampuni yake imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inachangia pato la serikali kutokana na kupata faida katika uwekezaji wake ambao sasa unafikia Trilion 1.5 nchini Tanzania ikiwa ni uwekezaji mkubwa zaidi kupata kutokea katika sekta ya mawasiliano.

“Tutaendelea kuwekeza katika Upanuzi na Uboreshaji wa wa mtandao wetu, Kufikia sasa tuna zaidi ya minara 2700 nchini kote ambayo inatoa huduma ya mawasiliano kwa zaidi ya asilimia 90% ya Watanzania wote,” alisema Meza na Kuongeza, “ Pamoja na hayo tunaendelea kujivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata kwa kubadilisha maisha ya zaidi ya Watanzania milioni 5 ambao wamechagua M pesa kuwa sehemu ya mfumo wa maisha yao katika upataji wa huduma za kifedha. Kupitia huduma hii tumetengeneza ajira zaidi ya elfu hamsini na kuwa sehemu muhimu katika kujenga uchumi wan nchi,” alisema Meza.

Aidha Meza ametanabaisha kuwa matumizi ya teknolojia bado yameendelea kuwa changamoto kwa watanzania akifafanua kuwa matumizi ya Intaneti nchini kwa sasa ni asilimia 10% tu ukilinganisha na asilimia 40 nchini Kenya huku akitoa wito kwa wadau wa sekta ya mawasiliano na serikali kushirikiana katika kuweka mipango thabiti na kuendelea kuleta mapinduzi ya kiteknolojia ili kuongeza matumizi ya intaneti kwa Watanzania katika kupata taarifa mbalimbali.

Meza alienda mbali zaidi na kusema kuwa Ongezeko la kodi kwa kampuni za simu litaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta hiyo katika upanuaji wa huduma na uendelezaji wa teknolojia mpya kukwama kwa sababu huduma hiyo itakuwa ghari na Watanania wengi watashindwa kuimudu, Pia itakuwa ngumu kwa kampuni kuendelea na ukuzaji na uboreshaji wa miundombinu na kuleta teknolojia mpya.

“Kodi ya laini ya simu ya Shilingi 1000/= kila mwezi itaendelea kuwa kikwazo kikubwa katika ukuzaji wa sekta ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na upanuaji wa huduma za mawasiliano maeneo ya vijijini, na itaendelea kuifanya huduma ya mawasiliano kuwa ghari na kuhindwa kutumiwa na Watanzania wengi wenye kipato cha chini, alisema Meza na kuongeza, “Itakuwa vigumu kuendelea kupanua huduma zetu katika maeneo ya vijijini kama hakuna soko la wateja kwa sababu wengi watashindwa kutumia huduma za mawasiliano,”

Kwa upande wao wachambuzi wa sekta ya Mawasiliano wanasema kufungiwa laini kwa wateja watakaoshindwa kulipa kodi hiyo ya shilingi 1000 ya kila Mwezi itapunguza pato la serikali kwa sababu wateja wengi hao wanalipa asilimia 14.5% ya matumizi na asilimia 18% ya VAT kwa matumizi hayo madogo ya kila siku.

Meza alihitimisha kwa kusema kuwa Vodacom Tanzania imeendelea kuwa kampuni pekee na inayoongoza kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma za jamii ambapo kwa Mwaka 2012 kampuni hiyo kupitia kitengo chake cha huduma za jamii cha Vodacom Foundation ilitumia shilingi bilioni 11, katika kuendeleza sekta ya Afya, Elimu na miradi mbalimbali ya kukuza uchumi kwa wanawake nchini ikiwa ni kiwango kikubwa kutengwa na kampuni katika utoaji na uungaji mkono wa huduma za kijamii.

“Vodacom Foundation imewezesha miradi zaidi ya 120 hadi sasa, ikiwa ni pamoja na uchangishaji wa fedha katika kupambana na kutokomeza ugonjwa wa Fistula nchini, kuboresha miundombinu ya mashule mbalimbali, na Miradi ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo kiuchumi hasa wanawaske kupitia mradi wa mikopo isiyokuwa na riba wa MWEI, na miradi ya kuwezesha upatikanaji wa maji katika maeneo yanayo kabiliwa na changamoto hiyo” alihitimisha Meza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: