Meneja wa Huduma kwa Jamii wa Tigo Bi. Woinde Shisael (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mpango wao wa kuinua elimu nchini ijulikanayo kama ‘Elimu Mwanzo Mwisho’ wakishirikiana na mfuko wa elimu ya Bonnah Education Trust Fund. Kushoto ni Mkurugenzi wa Bonnah Education Trust Fund Bi. Bonnah Kaluwa na Msemaji wa mfuko huo Bw. Haji Dachi.
---
Tigo Tanzania ikishirikiana na mfuko wa elimu wa Bonnah Trust Fund hivi leo wamezindua mpango maalumu wa elimu ijulikanayo kama ‘Elimu Mwanzo Mwisho’ yenye malengo yakuinua kiwango cha elimu nchini kupitia sanaa ya mitindo.

‘Elimu Mwanzo Mwisho’ ni kampeni mahususi yakuhamasisha jamii kuhusiana na umuhimu wa elimu, pamoja na kujaribu kutafutia suluhu za changamoto tofauti tofauti zinazokabili sekta hiyo kupitia onyesho la wazi la mitindo itakayofanyika katika mitaa na sehemu mbali mbali ya jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Huduma kwa Jamii Bi Woinde Shisael amesema kwamba Tigo inatambua umuhimu wa elimu katika kujenga jamii yeyote na ndio maana wameamua kushirikiana na mfuko wa elimu wa Bonnah Trust Fund kwa ajili yakutoa mchango wao ili watoto waweze kuwa na uwezo wa kupata elimu bora nchini.

“Kuwawezesha watoto na kuboresha elimu na mafunzo ni miongoni mwa malengo yetu muhimu. Kwa maana hiyo Tigo inaona hii onyesho la wazi ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza nchini ni namna yakipekee sana ya kutia hamasa kwenye masuala ya uboreshwaji wa elimu jijini Dar es Salaam, pamoja na kuwasisitizia wadau mbali mbali kuweza kuchangia katika mfuko huu,” alisema Bi. Shisael.

“Mwisho wa siku, tunapenda kuona kila mzazi akiguswa na onyesho hili la wazi la mitindo ili aweze kuelewa umuhimu wa kumpeleka watoto wao shule. Tunapenda kuona pia watoto wakipata uelewa wa thamani ya kweli ya elimu, na jinsi ambavyo kwenda shule kunavyoweza kuwahakikishia kuwa na maisha bora mbeleni. Pamoja na hayo, ni matumaini yetu kuwa wahisani wengi zaidi watajitokeza kuweza kuwadhamini watoto ambao hawana uwezo wa kulipa karo zao za shule,” aliongeza.

Wakati huo huo, Muasisi wa mfuko wa elimu ya Bonnah Trust Fund, Bi. Bonnah Kaluwa, alisema kwamba tukio hili ambayo litafanyika tarehe 12 Oktoba jijini Dar es Salaam imeandaliwa mahususi kwa ajili ya kuinua elimu na kuhamasisha watu mbali mbali kuhusiana na sekta hiyo yenye changamoto mbali mbali nchini kupitia njia itakayokuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa watu pamoja na kuwa burudisha kupitia onyesho hilo la mavazi, muziki na namna zingine za burudani zitakazokuwepo katika msafara huo utakaopita katika mitaa na kusimama sehemu mbali mbali muhimu jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mpango huo, Bi. Kaluwa alisema kwamba wameamua kuhamasisha elimu kupitia onyesho hilo la wazi la mitindo kwa sababu watu wengi wanapenda maonyesho ya mavazi na mitindo ila wanakua wanashindwa kuhudhuria kwa sababu ya gharama.

“Kwa maana hiyo tunawaletea watanzania maonyesho haya ya mitindo bure kabisa huku ikiambatana na ujumbe muhimu wa kuinua kiwango cha elimu nchini,” alisema.

“Kuna faida nyingi sana za elimu katika jamii, zikiwemo; watoto watahamasishwa kufanya vizuri katika masomo yao na kuwa mabalozi wazuri wa elimu katika jamii, huku wazazi wao nao wakinufaika na watoto wao kuelimika kwa sababu watoto watapunguza kuwa tegemezi kwao. Pamoja na hayo, ni mchango mkubwa sana katika maendeleo binafsi ya mwanafunzi, familia na taifa nzima kwa ujumla, kwa sababu mwisho wa siku inasaidia mpaka serikali kuu kutimiza malengo ya milenia ambayo yanatakiwa kufikiwa mwaka 2015,” alisema Bi. Kaluwa ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kipawa, jijini Dar es Salaam.

“Taasisi yetu inaamini kwamba, tukiwekeza katika vijana leo, tutakuwa tunawekeza katika Tanzania ya kesho, kwa sababu shule za sekondari zinawapatia vijana elimu yakujinasua kimaisha ambayo itawafanya kuweza kupata maisha bora huko mbeleni. Pia inawasaidia watoto kupata mafunzo ambayo inawafanya waishi kwa afya bora na mtazamo chanya wa maisha ambayo itawafanya kuwa watu wenye kuisaidia jamii yao, kukuza utamaduni wao pamoja na kutoa mchango wao wa kijamii na kisiasa katika maeneo yao wanayoishi. Elimu inamfanya mtoto kuwa mbunifu, na mtu wakujiamini, vitu ambavyo ni muhimu sana katika sekta ya nguvu kazi nchini Tanzania,” alimalizia kusema Bi. Kaluwa.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Matukio wa onyesho hilo, Bi. Regina Ogwal, onyesho hilo la mitindo linalenga kuhamasisha jamii katika masuala ya elimu kama hatua ya awali itakayofuatana na harambee yakuchangisha dola laki 1 (shilingi milioni 160) kwa ajili ya kuwapeleka watoto wasiojiweza shule. Harambee hiyo itafanyika mwezi Novemba.

Onyesho hilo la wazi la mavazi linazinduliwa asubuhi ya tarehe 12 Oktoba na Meya wa Manispaa ya Ilala Mstahiki Jerry Slaa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, halafu itapita Kariakoo, maeneo ya Fire, Upanga, Salenda Bridge, Morocco, Mwenge na hatimaye kufikia tamati jioni Mlimani City. Onyesho hili linategemea kugusa watu laki 2 Dar es Salaam nzima.

“Umma ushazoea kuona hamasa ikitolewa kwa namna ya matembezi ya hisani na maonyesho ya kawaida ya barabarani, lakini sisi tunataka kutumia namna ya tofauti, na ndio maana tumekuja na hili onyesho la wazi la mitindo litakalopita barabara na mitaa mbali mbali ya jiji la Dar es Salaam,” alisema Bi. Ogwal.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: