Na Prudence Karugendo
KWA wakati huu Tanzania imo katika operesheni kamambe ya kuwahamisha wahamiaji wanaoitwa haramu. Wengi wa hawa wahamiaji wanatoka katika nchi za nje na nyingi zikiwa jirani zetu. Kinachofanyika ni kuwakamata watu hao na kuwarudisha makwao kwa nguvu, ingawa wengine walishaona hapa ndio kwao.
Mpaka sasa bado sijaelewa ni watu gani wanaopaswa kuhesabiwa kama wahamiaji haramu. Sababu inaonekana wanaoandamwa na zoezi hilo ni wale wanaotoka katika nchi moja ambayo uhusiano wake wa kidiplomasia na Tanzania umekuwa dhaifu kupitiliza, nchi hiyo ni Rwanda.
Watu wengi, walio na asili ya Rwanda, ambao wengine wameishi Tanzania kwa zaidi ya miaka 70 wamesakamwa sana na zoezi hilo lililopachikwa jina la Operesheni Kimbunga. Hilo ni zoezi ambalo halijawahi kufanyika nchini tangu nchi yetu ijipatie uhuru ikiitwa Tanganyika wakati huo.
Suala la nchi kuwahakiki raia wake ni zuri sana, tangu zamani nimekuwa nikiliunga mkono nikishangaa kwa nini nchi yetu inalifanyia uzembe. Sababu kama tunavyoona ni Tanzania pekee ambayo baada ya zaidi ya nusu karne ya kujitawala ndiyo nchi iliyokuwa haijatengeneza vitambulisho vya uraia. Kwa sasa ndipo zoezi hilo linapofanyika tena kwa kusuasua.
Jambo hilo la Watanzania kukosa vitambulisho vya uraia linajulikana sana kwa watu wa nchi za jirani. Na mara nyingi, majirani wasio wema, wamekuwa wakilitumia tatizo hilo kama njia ya kujipenyeza nchini mwetu kwa ajili ya kufanya vitendo vya kihalifu wakati mwingine.
Kwa maana hiyo zoezi hili la Operesheni Kimbunga ni muafaka kwa wakati huu. Ila swali la kujiuliza ni kwa nini zoezi hili limepamba moto kwa wakati huu? Na je, inahakikishwaje kuwa zoezi hili haliambatani na kukomoana?
Wapo watu wengi ambao kutokana na kutofautiana kimtazamo wamekuwa wakidai kuwa hata mimi ni mtu wa nje ya Tanzania, kisa, natoka katika mkoa wa mpakani na nchi tatu. Swali ambalo mara nyingi nimekuwa nijiuliza ni kwamba ina maana sehemu hiyo ya Tanzania haikuwa na watu waliokuwa wanaikalia kabla ya wakoloni kuweka mipaka ya Tanganyika? Au watu wa nchi jirani walio karibu na mpaka wa Tanzania nao waitwe Watanzania? Je, Tanzania itakubaliana nalo hilo kwamba kila watu wa nchi jirani walio karibu na mpaka wake ni raia wake?
Ni vizuri kuwaondoa watu wanaobainika kuwa ni raia wa nchi za nje na wamekuwa wakiishi nchini kinyume na utaratibu. Tunapoliangalia hilo inabidi pia tuangalie watu hao wameishi nchini kwa muda gani na katika mazingira yapi. Bila hivyo, kuoneana wivu, visasi na kukomoana vitageuzwa vigezo vikuu vya kufanikisha zoezi hilo, ambapo Operesheni Kimbunga itageuka Operesheni Kiama.
Fikiria kuna watu walio na asili ya Rwanda ambao wamekuwa wakiishi Tanzania tangu miaka ya 1940. Leo hii useme kwamba watu hao wanapaswa warudishwe kwao! Hivi kweli uko si kuwaonea watu hao kwa kuwakomoa? Warudi kwao wapi ambapo kwa zaidi ya miaka 70 wanaijua tu Tanzania?
Na ikumbukwe kwamba wakati Tanganyika inapata uhuru wake toka kwa wakoloni lilitolewa tamko la uhuru, kwamba raia wote wa nje ya Tanganyika waliokuwa wameishi nchini kwa miaka 5 na zaidi moja kwa moja walikuwa ni Watanganyika, labda ambao hawakuhitaji kuhusishwa na tamko hilo.
Sasa leo hii haieleweki tamko hilo liliishia wapi, tunawaona tu watu waliokuwa Tanganyika kabla ya uhuru, kwa zaidi ya miaka hata 20, wakisakamwa kuwa ni wahamiaji haramu! Jambo lingine la kusikitisha ni kwamba kuna watu waliozaliwa Tanganyika na baadaye Tanzania, hata kama wazazi wao ni wa kutoka Rwanda, watu hao hawajui kwingine zaidi ya Tanzania, leo nao wanaambiwa waondoke! Waende wapi?
Kinachoonekana hapa ni kile cha kusema kwamba ni lazima kila mtu arudi kwenye eneo la asili yake. Jambo hilo kwangu linaonekana ni tata. Sababu kama tutaliendekeza sielewi ni mtu gani anayepaswa kujiona ni Mtanzania halisi. Historia inaonyesha kwamba kabila zima la Wangoni lilitoka Afrika Kusini.
Je, mgoni anayeshiriki katika Operesheni Kimbunga anaelewa kuwa upo uwezekano wa kumwambia naye arudi kwenye asili yake, Afrika kusini? Je, ni sahihi kufanya hivyo?
Wamakonde nao, wengi wao wako upande wa Msumbiji, ni halali kusema waondoke wote kurudi Msumbiji? Kigoma nako kuna kabila la Wamanyema, kabila hilo asili yake ni Kongo, DRC. Kwahiyo kwa operesheni hii upo uwezekano wa kulirudisha kabila hilo kwao?
Katika hotuba ya Nyerere aliyoitoa kwenye viwanja vya White House, mwaka 1963, alipokaribishwa na rais wa Marekani wa wakati huo, John Keneddy, alisema kwamba Tanganyika ni nchi inayoundwa na mchanganyiko wa watu wa aina mbalimbali, wenyeji na wahamiaji. Akasisitiza kwamba watu wote wa Tanganyika, wawe wahamiaji au wenyeji, walikuwa raia wenye haki sawa.
Sikumbuki maneno hayo ya Mwalimu Nyerere yalikuja kutenguliwa lini kiasi cha kuanza kuwaona wahamiaji ni watu wasiotakiwa kuikalia ardhi ya nchi hii.
Sote tunakumbuka kwamba aliyepandisha mwenge kwenye kilele cha uhuru cha Mlima Kilimanjalo siku ya uhuru, alikuwa Alex Gwebe Nyirenda, mtu wa Malawi. Wakati huo alikuwa Tanganyika, nchi ambayo kwa pamoja na Malawi zilikuwa chini ya himaya ya Mwingereza. Kitendo hicho alichokifanya Nyirenda kilimpatia umaarufu mwingi sana hapa nchini, kiasi kwamba hakuna aliyejali kuwa yeye ni mtu toka taifa lingine. Lakini leo hii angekuwa hai si ajabu naye angekumbwa na hiki kimbunga kinachoendelea kwa sasa.
Pamoja na hiyo, kimbunga hiki kinaonekana kuwasakama sana watu tulio na ngozi moja, kwa maana ya weusi. Na wengi wamesakwa katika mikoa iliyo pembezoni mwa nchi, kwa maana ya mikoa iliyo mipakani.
Katika maeneo ya mijini kimbunga hicho hakijaonekana kuleta madhara makubwa. Na haya ni maeneo yaliyo na watu tunaoweza kuwatambua kirahisi kuwa hawatokani na jamii yetu tofauti na wa kule mikoani. Hapa tunao watu kutoka India, Pakistani, Uarabuni na Mashariki ya Mbali. Na wakati mwingine wazungu.
Mara nyingi watu hao wamekuwa wakijilinda na dhana ya kwamba ukiwasema utakuwa unaleta ubaguzi wa rangi. Yaani tuseme wao wana haki ya kuishi kinyemela nchini kwa kulindwa na rangi zao. Wale ambao hatuwezi kuwabagua kwa vigezo vya rangi zao ndio tunaofanya haraka ya kuwatambua kuwa ni wahamiaji haramu!
Ni jambo la kushangaza kuona watu tunaolazimika kuwa makini ili kutowaonesha ubaguzi wa rangi wao wanatuonesha ubaguzi bila kificho chochote!
Mfano tangu tumeishi na Wahindi hawajakubali kuishi kama tunavyoishi sisi. Kwa hapa Dar, kwa mfano, utawakuta Wahindi wanaishi katika makazi ya ajabu, karibu wote wanaishi katika majumba yaliyo kama viota, maeneo ya mijini tu, hata kama wanazo pesa za kujenga mahekalu katika maeneo mbalimbali.
Kinachowafanya waishi hivyo ni kujilinda wasichanganyikane na wenyeji weusi, ubaguzi wa rangi. Mfano huwezi kuwakuta Waindi wamejenga Kinyerezi, Tabata wala Keko, kama walivyo raia wengine. Mara zote wao wanapendelea kupanga katika majumba ya serikali, National Housing, na wale wachache walioamua kujenga makazi ni katika maeneo maarumu yasiyofikiwa na watu wote.
Bahati mbaya ni kwamba watu hao wanaoonekana kuwabagua wenzao wa asili, kwa kigezo cha rangi, wamepata nafasi kiasi cha kujipenyeza katika sehemu zetu nyeti, kama Bunge na kwingineko. Watu ambao hawako tayari kuishi na wenzao katika eneo moja eti wanajifanya wabunge wao, wanawatungia sheria na mambo mengine yanayohusu mustakabali wao!
Tumesikia mtu mmoja, maeneo ya Karagwe mkoani Kagera, kajinyonga kusudi asirudishwe mahali alipoambiwa ni kwao, si ajabu alikuwa hapakumbuki. Akaona kifo ni bora kuliko kurudishwa kule!
Zoezi hili linaloendelea linafaa, ila lingefanywa kiumakini zaidi. Lisiachiwe liinginze visasi, wivu, vinyongo na kukomoana.
Watu walio haramu sio tu kwamba wanapatikana kwa wahamiaji, wapo watu haramu walio wenyeji kabisa. Majambazi, kwa mfano, wanaweza kuwa watu wa asili, lakini kiukweli ni watu haramu. Vivyo hivyo majangiri, wa rasili mali, wanyama na madini, nakadhalika. Wote hao ni watu haramu, sio lazima wawe wahamiaji. Tusiiachie operesheni hii ya kimbunga ikageuka kiama.
prudencekarugendo@yahoo.com
Toa Maoni Yako:
0 comments: