Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi.

Dereva mmoja wa Bodaboda amefariki dunia papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa kwenye ajali baada ya pikipiki mbili kugongana usukani kwa usukani huko kwenye eneo la Mzundu wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga ACP Constantine Massawe, amemtaja Dereva huyo wa Bodaboda kuwa ni Ismail Mhando(30), mkazi wa Kabuku wilayani Handeni.

Amesema kuwa ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Mzundu wilayani Handeni mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo katika uchunguzi wa awali wa tukio hili Polisi walibaini kuwa imesababishwa na mwendo kasi kwa kila mmoja na kutokuwa makini barabarani.

Amesema marehemu Mhando akiendesha pikipiki yenye nambari za usajili T.256 AYM akitokea Kabuku kwenda Mzundu akiwa amempakia dada mmoja aitwaye Salama Bakari, aligongana na pikipiki nyingine iliyokuwa ikitokea Mzundu kwenda Kabuku yenye namba za usajili T. 584 CCS.

Alisema pikipiki hiyo ikiendeshwa na Sudi Nassoro ilikuwa imepakia abiria wawili maarufu kama mshikaki na ilikua ikitokea katika kijiji cha Mzundu kwenda Kabuku wilayani humo.

Kamanda Massawe amesema majeruhi wanne wa ajili hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu zaidi na hali zao amesema zinaendelea vizuri.

Kamanda Massawe ametoa wito kwa Madareva wote wa Bodaboda kuwa makini wanapokuwa barabarani na kujiepusha na upakiaji abiria zaiidi ya mmoja ili kuepuka matukio ya ajali zinazowahusisha watu wengi kwa wakati mmoja.

Amewataka kila mmoja wao kuwa mlinzi wa mwingine na kutoa taarifa pale wanapomuona mwenzao mmoja anavunja sheria na kutotii sheria bila ya shuruti ili achukuliwe hatua ili kuwanusuri wengine wanaofanya kazi zao vizuri.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: