Ukizungumzia makundi yanayofanya vizuri kwenye uchezaji wa muziki hapa nchini Tanzania, huwezi kuacha kuwataja THT. Pamoja na kuwa ndio walioleta mageuzi kwenye tasnia ya kucheza miziki hapa nchini, hasa kwa kuchanganya miziki ya asili na ya kizazi kipya, kituo hicho bado kimeendelea kuzalisha wachezaji wengi wa miziki hapa nchini.

Kikiwa ni kituo maarufu kwa kuzalisha vipaji vya kuimba pia, THT inaaminika kuwa kituo kikubwa kabisa cha sanaa ya burudani chenye mafanikio makubwa hapa nchini.

Wakati historia ya wacheza muziki hapa nchini ina chimbuko la muda mrefu, kwa THT, Msami Giovani, ndie mtu ambaye anatajwa sana katika kusaidia mafanikio ya kituo hicho.

Msami, ambaye alijiunga kituoni hapo kama mchezaji, lakini kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika kucheza ndipo alipochaguliwa kufundisha wenzake.

Toka wakati huo hajawahi kurudi nyuma, na ameendelea kujijengea jina kwa kuwaandalia wanamuziki wengi wa hapa nchini mtiririko wa show zao.

Msami ambaye ana umri wa miaka 24, anasema alianza kupenda kucheza akiwa na umri mdogo na alivutiwa na Michael Jackson pamoja na miziki ya kikongo.

Msami ameshiriki mashindano ya kucheza mashindano mengi hapa nchini kama Cheza Tanzania, Dance La Fiesta, Malta Guiness Street Dance na Mkali wa Temeke.

Zaidi ya kushiriki kwenye kucheza Msami pia ameshiriki kuandaa mtiririko, au choreagraphing kwa kiingereza, ya matamasha makubwa hapa nchini kama FIESTA, KILLI MUSIC AWARDS, MISS TANZANIA, VISA2DANCE, na mengine mengi.

Kwa mwaka huu umeanza kwa hatua nyingine kubwa katika maisha yake ya kazi na sanaa. Msami alipata fursa ya kipekee kwa kwenda Marekani kufundisha kundi la madansa ambao wanaruka na kamba na kucheza pia, ikifahamika kama Fusion kwa kiingereza.

Kundi hilo alilofundisha Marekani kwa wiki tatu, limeshinda ubingwa wa dunia katika kipengele cha kucheza na kuruka kamba.

Akizungumzia mafaniko hayo makubwa, Msami alisema anamshukuru Mungu kwani hayo ni mafanikio makubwa kwa mtanzania wa kawaida kufundisha madansa Marekani, lakini pia kuweza kuwapa ubingwa wa dunia.

‘Kujituma na kujifunza kila siku ndio msingi mkubwa wa mafanikio yangu, kwani toka nilipoanza kucheza niliamini nitafika mbali katika sanaa hii’ anasema Msami.

Kundi hilo alilolifundisha Msami, la Hot Dog USA, linadhaminiwa na kampuni ya One World, One Rope ambao walishawahi kuja hapa nchini miaka mitatu iliyopita kuendesha kambi ya kuruka kamba kwa ajili ya Watanzania.

Msami anasema akiwa Marekani alipata fursa ya kufundisha makundi kumi tofauti ya muziki lakini mkazo ukiwa kundi la Hot Dog USA.

Akizungumzia mipango yake, Msami anasema ana mpango wa kuandaa kikundi cha wacheza muziki na kuruka kamba hapa nchini ili kikashiriki mashindano ya dunia hapo baadaye.

‘Unajua Fusion, yaani kucheza na kuruka kamba sio mchezo maarufu hapa nchini, hivyo kwa kushirikiana na wadau nina mpango wa kuufikisha mbali’ anasema Msami.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: