Waziri
wa
Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe (kulia) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es
Salaam jana wakati akitangaza kuwafukuza kazi Wakurugenzi wa Bandari.
Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu – Wizara ya Uchukuzi , John Mngodo na
katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,
Mhandisi Omar Chambo.
WIZARA ya Uchukuzi imewatimua kazi Wakurugenzi wa 3 na Mameneja 2 wa Waliokuwa Watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Makao Makuu Dar es Salaam.
Akitangaza Uamuzi huo kwa Wana Habari Ofisini kwake, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa katika taarifa yake aliyo isoma kuwa Wakurugenzi hao walitimuliwa kazi kwa nyakati tofauti baada uchunguzi wa Tuhuma zilizokuwa zikiwakabili kukamilika ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kuhojiwa.
Kubwa zaidi lililowapelekea wakubwa hao wa TPA kuachwa nje ya Meli yaDk. Mwakyembe ni Matumizi mabaya ya Madaraka na Ubadhirifu wa Mali ya Umma na kuitia Hasara serikali na huenda Bodi ya Wakurugenzi ikijiridhisha ikawafungulia Mashitaka Mahakamani.
Dk. Mwakyembe ambaye yupo mstari wa mbele katika vita dhidi ya ubadhirifu wa Mali za Umma kwa kuwashughulikia ipasavyo watendaji wa Sekta zake zote hasa TPA na ATC, aliwataja walio timuliwa kazi kuwa ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma, Hamadi Koshuma, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Julius Mfuko, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ngamilo, Meneja Kituo cha Kupakuluia Mafuta, Tumaini Massaro.
Tuhuma zilizokuwa zikiwakabili ni kama ifuatavyo kwa kila mmoja:-
MKURUGENZI MKUU TPA: EPRAIM MGAWE
Akiainisha tuhuma zilizomfukuzisha kazi Mgawe kuanzia Ijumaa iliyopita Januari 18 mwaka huu, Dk Mwakyembe alisema ni pamoja na uzembe uliokithiri.
Dk Mwakyembe alidai kuwa Mgawe alizembea na kuruhusu kuwepo kwa muda mrefu utaratibu usiofaa wa upokeaji na uondoshwaji bandarini wa mafuta machafu.
Katika tuhuma hiyo, Mgawe anadaiwa kuachia kiasi kikubwa cha mafuta safi kuibiwa; na kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji bandarini wa mafuta machafu kinyume na mikataba iliyowekwa.
Tuhuma ya pili iliyomuondoa kazini Mgawe, ni ufanisi duni ambao Dk Mwakyembe alifafanua kuwa alishindwa kudhibiti wizi uliokithiri bandarini wa mizigo na mali ya Mamlaka.
Pia anadaiwa ameshindwa kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya Kitengo cha Kuhudumia Kontena Bandarini (TICTS) na TPA ambapo TICTS kwa muda mrefu inadaiwa wamekuwa wakikiuka mkataba huo.
Pia Mgawe anadaiwa kuipotosha Bodi mpaka ikaridhia uanzishwaji wa chombo cha pili cha ununuzi ndani ya Mamlaka kinyume ya Sheria.
Kosa la tatu la Mgawe ni kukosa uaminifu kulikopindukia, ambapo anadaiwa kutumia chombo cha pili cha ununuzi kilichoanzishwa kinyume cha sheria na kuingia zabuni mbalimbali bila kufuata utaratibu na kanuni za zabuni kama zilivyoainishwa na Sheria ya Manunuzi.
Pia inadaiwa miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo ya chombo cha pili cha ununuzi, haikuwa na tija kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kasa la mwisho lililomuondoa Mgawe kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ni kukiuka sheria na utaratibu ambapo anadaiwa kuingia mkataba na Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC) bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.
Pia anadaiwa kuongeza mishahara kwa asilimia 15 tarehe mosi Julai, mwaka jana bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi, hivyo kukiuka utaratibu uliowekwa na sheria.
NAIBU MKURUGENZI MKUU WA HUDUMA, HAMADI KOSHUMA
Tuhuma zilizomng’oa Koshuma kwa mujibu wa Dk Mwakyembe ni nne, ikiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka. Katika hilo, Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Huduma, anadaiwa kuruhusu michakato mbalimbali ya zabuni bila kufuata utaratibu kwa kisingizio cha kwamba ni miradi mikubwa.
Koshuma pia anadaiwa kuwa na ufanisi duni, ambapo akiwa Mjumbe wa Bodi ya Zabuni, alishindwa kuijulisha Bodi ya Mamlaka ya Ununuzi ya Umma (PPRA), kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi.
Ukiukwaji huo umefafanuliwa kuwa unahusu kuruhusu Mamlaka kuingia mkataba wa kibiashara na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni na kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji.
Kosa la tatu analodaiwa kufanya ni kukosa uaminifu kulikopindukia, ambapo Koshuma anadaiwa kushiriki kuipotosha Bodi mpaka kuanzishwa cha chombo cha pili cha manunuzi kinyume ya sheria.
Baadaye, anadaiwa kutumia chombo hicho batili bila kufuata utaratibu kwa kisingizio kuwa ni miradi mikubwa ambapo miradi mingi iliyongiwa kwa njia hiyo, haikuwa na tija kwa Mamlaka zaidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma.
Mwisho Koshuma amedaiwa kukiuka sheria na taratibu kwa kushiriki kuingia mkataba na CCCC bila kuishirikisha Bodi ya Zabuni ya Mamlaka.
Pia anadaiwa kushiriki kwenye uamuzi wa kuongeza mishahara kwa asilimia 15 kuanzia Julai mosi, mwaka jana bila idhini ya Waziri wa Uchukuzi.
NAIBU MKURUGENZI MKUU WA MIUNDOMBINU, JULIUS MFUKO
Kwa upande wa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Miundombinu, Mfuko Dk Mwakyembe alisema bosi huyo wa zamani anadaiwa kushindwa kusimamia maandalizi ya miradi mbalimbali ya miundombinu ya mamlaka.
Kwa mfano inadaiwa miradi ya ex-AMi yard, Port Community System na CCTV kwa muda mrefu iko kwenye utekelezaji bila kukamilika kutokana na misingi mibovu ya maandalizi. Imeelezwa kuwa fedha nyingi ya Mamlaka imetumika kwenye miradi hiyo bila matokeo tarajiwa.
Pia anadaiwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa mikataba mbalimbali, na kusababisha kutokamilika kwa wakati na kuisababishia Mamlaka hasara kubwa.
Kasa la tatu ni kushindwa kuisimamia kwa ufanisi divisheni ya maendeleo ya miundombinu na kuathiri maendeleo ya Mamlaka kwa ujumla.
Mfuko pia anadaiwa kushindwa kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka katika udhibiti na uendeshaji wa Mamlaka.
Mameneja
Panga la Mwakyembe limewaangukia pia Mameneja wawili ambao ni MENEJA WA BANDARI YA DAR ES SALAAM, CASSIAN NGAMILO na MENEJA KITUO CHA KUPAKULUIA MAFUTA (KOJ), TUMAINI MASSARO.
NGAMILO: Yeye amedaiwa kutumia madaraka yake vibaya, uzembe uliokithiri na kushindwa kusimamia mkataba wa mafuta machafu.
Pia anadaiwa kushindwa kusimamia ulinzi wa mali za wateja, kutoa nyongeza ya mkataba kinyume cha sheria.
MASSARO: Ameachishwa kazi kutokana na madai ya uzembe uliokithiri, kushindwa kusimamia udhibiti wa mafuta machafu na kuisababishia Serikali hasara kubwa pamoja na ufanisi duni.
PICHA KWA HISANI YA FATHER KIDEVU BLOG.
Toa Maoni Yako:
0 comments: