Madee kushoto akiwa na dogo Janja

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

KUIBUA au kusimamia wasanii wachanga, wakati mwingine kunahitaji moyo wa chuma. Ni kutokana na baadhi yao kushindwa kukubali wala kukumbuka fadhila, jambo ambalo ni magumu matokeo yake.

Matokeo yake ni magumu kiasi cha kuwaumiza vichwa wengine, wale waliokuwa na nia njema na watu ambao kwa hakika, wametumia muda na gharama kubwa.
Chid Benz, mkali wa michano Tanzania

Nimelazimika kusema hili baada ya kusikia na kuona maneno ya msanii chipukizi wa muziki wa Hip Hop, Abdulimalick Chande maarufu kama Dogo Janja, alivyoweza kumjia juu mkombozi wake kisanaa, Ahmad Ally Madee.

Nasema hivyo baada ya kuona kwamba Dogo Janja, amebwatuka, kupayuka juu ya Madee ambaye ndiye aliyefanya juhudi ili awe juu. Sitaki kukubali kwamba Dogo Janja alikuwa anaibiwa au kudhulumiwa na Madee na kundi lake la Tip Top ‘Connection’ lenye maskani yake Manzese.

Nasema hivyo maana naelewa vizuri soko la muziki lilivyokuwa hapa nchini. Najua zipo fedha zinazoingia, hasa za maonyesho, kama walivyokuwa wasanii wengine. Sio siri, Dogo Janja anaimba muziki wa Hip Hop ambao soko lake ni gumu mno. Ni wachache wanaotamba, ndio maana hata shoo zao sio nyingi.

Ukiangalia kwenye ramani ya muziki huo wa kizazi kipya, wasanii wa kuimba, iwe zouk, rhumba, R&B ndio wanaotamba, kiasi cha mapato yao kuwa mengi. Sio Dogo Janja. Bado, kwanza ni mdogo kiumri ni kisanaa pia. Dogo Janja, fedha zake sio nyingi, maana hata zile shoo za usiku hazipati.

Dogo Janja, nyimbo zake ni tatu tu, ukiwamo ule wa ‘Anajua’ aliyoimba sambamba na nahodha wa kundi lake la Tip Top, Tunda Man.

Kwa mujibu wa sheria, Dogo Janja hawezi kufanya shoo za usiku, hasa za vinywaji vya pombe. Huo ndio ukweli, hivyo tunapojaribu kuliangalia sakata lake juu ya Madee, aliyemuibua, tuwe makini.

Mimi kama mdau wa muziki, niliwahi kuzungumza mengi na msanii huyo kabla hata ya kuwa maarufu kwa asilimia chache. Ndoto, mawazo mengi yaliongozwa na moyo wa dhati wa kundi lake, linaloongozwa na Madee. Leo Dogo Janja amesahau kiasi cha kumtusi mkubwa wake?

Kwa mujibu wa Dogo Janja, ameamua kurudi kwao Arusha, maana Madee alimuibua ili amuibie. Hapa utacheka. Maana anaongea bila kujua. Hivi kama Dogo Janja leo analalama kuibiwa, vipi jana alipokuwa akitumia fedha za watu, kuandaliwa kisanaa hadi kwennda studio.

Vipi pale gharama za kumtangaza zilipochukua nafasi yake ili awe maarufu na kufahamika? Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kama wapo waliokuwa na nia njema na Dogo Janja, ilikuwaje wasubiri hadi aendelezwe kipaji chake na Madee, chini ya Meneja wa kundi lake, Babu Tale na Abdu Bonge.

Hili nalo linahitaji elimu ya Chuo Kikuu kubaini kwamba sio kukosa shukrani tu, bali amekurupuka juu ya kumtusi muungwana wake. Ndio, maana ugumu wa sanaa ni kutoka tu. Kila mtu ni msanii na ana nyimbo nzuri kuliko wanaojulikana. Ila wanashindwa jinsi ya kutoka na kujulikana.

Sasa kama hivyo ndivyo, kwanini tusiheshimu mchanngo wa wenzetu katika maisha yetu kisanaa? Kwanini Bongo Fleva ni wapayukaji? Ama kwakuwa wengi wao wanaendeshwa na vilevi? Na hawa ndio wanaojifanya marafiki wa kweli kwa vijana wetu, ambao nao huwaamini

Sawa, ila kabla ya kupewa maneno ya kuwadharau wakombozi wetu, ni vizuri tukatumia muda huo walau robo tu, kukumbuka tulipotoka. Kwa mfano mimi. Mafanikio yangu, au kujua kwangu kwa kiasi kidogo kuandika, hakika wapo au yupo ambaye amechangia kuniweka hapa.

Sasa itakuwa ujinga, wendawazimu kutembea hadharani na kumtukana, kwa sababu tu, tumeshindwa kuelewana katika baadhi ya mambo. Nafikiri hili ni jambo la busara na lazima liangaliwe upya na wasanii wetu. Tuweke mbele hekima, maana sanana ipo na wakali wanazaliwa.

Aina hiyo ni kuwafanya wengine washindwe kusaidiwa kama wewe ulivyosaidiwa? Tatizo sio kuondoka kwenye kundi, tatizo ni kutoa lugha za matusi, jambo linaloniumiza na kunichukiza na aina hii ya maisha ya wasanii wa Tanzania.

kambimbwana@yahoo.com

0712 053949

0753 806087
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: