Na Mwandishi wetu.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani, ameteuliwa kuwamo kwenye ujumbe rasmi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), utakaosimamia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zilizopangwa kufanyika Januari mwakani, nchini Afrika Kusini.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou na Kamati yake ya Utendaji, ukiwa na lengo la kuweka sawa ujumbe huo wa CAF kwa ajili ya fainali hizo muhimu kwa Afrika, nchini Afrika Kusini, huku ukiwa na wajumbe 148.
Taarifa iliyotumwa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, ilisema kuwa Nyamlani ni mmoja wa wajumbe watatu watakaoshughulia masuala ya rufani katika michuano hiyo ya Afrika.
Aliwataja wajumbe wengine kuwa ni Prosper Abega kutoka Cameroon na Pierre-Alain Monguengui wa Gabon, huku bodi hiyo ya rufani ikiwa na wajumbe 12.
Katika hatua nyingine, mchakato wa uchaguzi wa (KAREFA) umefutwa kutokana na wagombea watano kati ya nane vyeti vyao vya elimu ya sekondari kuwa na utata.
Wambura alisema badala yake, mchakato wa uchaguzi huo utaanza upya Novemba 21 mwaka huu kwa ajili ya kupatikana viongozi wapya.
Nao mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA), utaanza upya Novemba 26 mwaka huu baada ya mchakto wa sasa kupata wagombea kwenye nafasi mbili tu za Kamati ya Utendaji ya chama hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments: