Na Mwandishi Wetu
MWIMBAJI na Mkurugenzi wa kundi la Jahazi Modern Taarabu, Mzee Yusuph, amesema kwamba bado anaendeleza harakati zake kimuziki ili kundi lao liendele kuwa imara.
Jahazi ni miongoni mwa makundi yenye mguso na mashabiki wengi, akifanikiwa kujaza katika kumbi mbalimbali za burudani pamoja na ziara zao za mikoani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita, Mzee Yusuph alisema kwamba mashabiki wao wamekuwa wakiwaheshimu sana, jambo linalomfanya aone kuwa heshima katika soko la taarabu wanayo.
Alisema kwa kutunga vibao moto moto, ni mbeleko ya mashabiki wao, hivyo juhudi zao zitaendelea kuongezwa kwa ajili ya kufanya vyema zaidi katika muziki huo nchini.
“Nashukuru tumeendelea kuwa vinara katika soko la muziki wa taarabu hapa nchini, hivyo nadhani mashabiki wetu wasubiri mambo mazuri kutoka kwa wana Jahazi.
“Hiyo ndio mipango yetu kwa ajili ya kujiweka kileleni zaidi katika tasnia ya muziki wa taarabu hapa nchini, ukizingatia kwamba kwa miaka kadhaa shoo zetu zimekuwa zikijaza watu wengi,” alisema.
Mbali na kuwa mtunzi wa nyimbo mbalimbali zinazotikisa katika chati za muziki huo nchini, pia Mzee Yusuph ni mpiga kinanda mahiri, pamoja na kuwa muandaaji wa nyimbo mbalimbali za kundi lake.
Toa Maoni Yako:
0 comments: