*Dk. Bana asema harakati zao hazikubaliki
*Tendwa naye awatega kuhusu ruzuku

Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetupiwa lawama kwamba harakati zake za kisiasa zinatishia usalama na amani ya nchi.

Hayo yalijitokeza jijini Dar es Salaam leo, katika Kongamano liliitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa na kuwashirikishaviongizi wa vyama vyote vya siasa.

Kongamano hilo lilikuwa likijadili umuhimu wa amani na usalama wa nchi, wajibu wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa katika kukuza demokrasia ya vyama vingi.
 
Baadhi ya wadau na vyama kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini walikitupia lawama chama hicho na kudai kuwa kimekuwa mstari wa mbele katika kuvunja sheria na maadili ya taifa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema harakati zinazoendeshwa na CHADEMA, hazikubaliki na zinalenga kuvunja sheria za nchi.

Dk. Bana, alisema alikosoa kile harakati za chama hicho kupitia oparesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), kwa kufanya mikutano kila kona ya nchi  haina tafsiri nyingine yoyote zaidi ya kutaka kuvunja amani na usalama wa nchi.

Katika mada yake, iliyohusu, Mazingira wezeshi na hatarishi katika kujenga na kukuza mfumo wa vyama vingi vya siasa, Dk. Bana, alisema, CHADEMA, ni chama kikubwa na chenye nguvu kuweza kuchukua dola, hivyo kinapaswa kuonyeshwa mfano kwa umma hasa katika kutii na kuheshimu sheria.

Alisema  mikutano na maandamano ya CHADEMA yanayofanyika kila mahali nchini hayana lengo zuri kwa sababu muda huu si wakati wa kampeni za uchaguzi.

Mharidhi huyo wa siasa ambaye pia ni Mwenyekiti wa REDET, alisema kinachofanywa sasa na chama hicho si kueneza sera zake bali ni sawa na kampeni za uchaguzi kabla ya muda wake.

Alisema wakati huu ni wakati wa vyama vya siasa kujijenga kwa kufanya mikutano ya ndani ya chama, kuandaa viongozi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mkuu 2015 pamoja na kuhamasisha wananchi washiriki shughuli za maendeleo na si kufanya mikutano na maandamano yanayofanana na kampeni za uchaguzi.

Alisema, kauli mbiu ya M4C, ni nzuri  lakini haifai  kwa wakati huu, na kusema ikitokea kila chama cha siasa kilichopata usajili kutaka kufanya siasa kwa maandamano na mikutano kama CHADEMA nchi haitatawalika.

Dk. Bana, pia alizungumzia hatua ya CHADEMA kususia kongamano hilo, huku akisema si hatua nzuri kwani inaonyesha chama hicho hakina uvumilivu wa kisiasa.

“CHADEMA ni chama kikubwa ambacho kimejijengea heshima kubwa na kinatarajiwa kuchukua dola wakati wowote, kwa hiyo hakina budi kufuata na kuzingatia sheria za nchi ili kuonyesha mfano kwamba kipo tayari kuongoza umma.

“Mimi sielewi hizi harakati zao zinalenga nini, sioni umuhimu wake, vyama vya siasa baada ya uchaguzi huwa vinapata muda wa kujitathimini na kufanya mikutano ya ndani siyo vuguvugu, lakini kinachofanywa na CHADEAMA sasa ni kampeni za uchaguzi ambazo si wakati wake,

“Hii si nchi ya mabadiliko, tunayo serikali iliyowekwa madarakani na wananchi kwa mujibu wa sheria, sasa wanaandamana kupinga nini? Alisema na kuhoji Dk. Bana

“Wakiendelea namna hii, nchi itapelekwa pabaya, haya maandamano na vuguvugu hizi zinaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi, hakuna uhuru,

Tendwa naye anena

Msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa, alisema kitendo cha CHADEMA kususia kongamano hilo siyo cha kiungwana.

Alisema, kongamano hilo, lilikuwa na nia njema ya kuwaweka karibu viongozi wa jeshi la Polisi, vyama vya siasa pamoja na ofisi yake ili kutafuta muafaka wa kitaifa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: