Na
Mwandishi Wetu.
NAIBU
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene (pichani), ameziagiza
halmashauri zote kuhakikisha zinatoa kipaumbele cha mgao wa mapato ya
uwekezaji wa mafuta, madini na gesi katika maeneo ambako nishati hizo zimegunduliwa na kuchimbwa.
Agizo
hilo alilitoa katika Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara jana, wakati
alipozungumza na wananchi wa kijiji hicho.
Alisema
ni vema wananchi katika maeneo hayo wakapata manufaa ya haraka kwa
rasilimali hizo.
Alisema
si busara kwa watu wanaoishi na wawekezaji wanaochimba gesi au mafuta
katika maeneo yao huku wakiwa hawana maendeleo na huduma muhimu
zilizo bora.
“Kuna
kodi ambazo hawa wawekezaji wanalipa serikalini na hii kodi kuna
kiasi kinarejeshwa katika Serikali za Mitaa ambazo mamlaka zake
zinaanzia ngazi ya kijiji, sasa ni vyema wenzetu wa halmashauri
mkaweka kipaumbele na mgao wa mapato katika maeneo yaliyo na nishati
hiyo, ili nao wanufaike na waone tija ya kuwapo miradi mikubwa katika
maeneo yao,” alisema Simbachawene.
Alisema
hata migogoro mingi inayotokea kati ya wawekezaji na wenyeji
inatokana na wananchi kutoona manufaa ya uwekezaji jambo ambalo ni
vema likatatuliwa kwa kuwapa mgao na kuchochea maendeleo kwa
kuboresha miundombinu, maji, zahanati na huduma nyingine muhimu.
“Hawa
watu wetu hawana tatizo na mipango ya Serikali lakini pengine sisi
viongozi na wataalamu wetu tunawachanganya, leo natoa agizo
hili hapa lakini unaweza kukuta utekelezaji wake unachukua muda mrefu
au haulitekelezwi,” alisema Simbachawene na kuongeza:
“Sasa
wananchi wanapouliza hawajibiwi vizuri, hii si busara hawa watu
wasiishie kubugia vumbi la magari ya wawekezaji kwa hiyo ni vema
wanufaike na miradi yao.
“Sisemi
fedha zote mtakazopata mzigawe kwa maeneo hayo tu, hapana, lakini
ninachotaka kuona ni maeneo ya uwekezaji yanapewa kipaumbele.
“Najua
kutaibuka mvutano mkubwa kwa madiwani kutaka kila mmoja katika kata
yake kupata mgao, lakini hilo si tatizo ila kinachotakiwa ni busara
itumike.”
Toa Maoni Yako:
0 comments: