Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitabu cha maombolezo
nyumbani kwa Marehemu Meja jenerali Kamazima Tegeta, Dar es salaam, leo.
---
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za pole Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange
kufuatia kifo cha Meja Jenerali Anatory Ruta Kamazima (Mstaafu) aliyefariki
jana tarehe 25 Septemba, 2012 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nimepokea
kwa mshituko na huzuni nyingi habari za kifo cha Meja Jenerali Kamazima,
ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
Taifa kwa ujumla” Rais amesema katika salamu hizo.
Mchana wa leo Rais ameitembelea familia ya marehemu
nyumbani kwao Tegeta kuwafariji wafiwa.
Marehemu alizaliwa mwaka 1946 katika kijiji cha Maruku,
Mkoani Kagera. Alijiunga na Jeshi mwaka 1967, mara baada ya kuhitimu
Chuo Kikuu mwaka 1966.
Marehemu Kamazima amesoma kozi mbalimbali za kijeshi
hapa nchini na nchi za China, India, Uingereza na Misri na kulitumikia
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika ngazi mbalimbali ambapo
mwaka 1989, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia Rushwa
Tanzania, hadi alipostaafu Juni 2003.
Rais amemuelezea marehemu Kamazima kama mzalendo
na mtu aliyeipenda na kuitumikia nchi yake kwa weledi mkubwa, uaminifu
na moyo mmoja.
“Nimemfahamu Marehemu kwa miaka yote ya utumishi wake jeshini na
serikalini kama mzalendo, muaminifu na mwenye moyo wa kulinda nchi yake
wakati wote” amesema “Marehemu
Kamazima alikua mtu wa kutumainiwa sana katika nchi yetu na kamwe hatutamsahau
kwa utumishi wake uliotukuka”.
“Tutamkumbuka
na kumuenzi siku zote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na tunamuombea
mapumziko mema Marehemu Kamazima. Amina”. Rais ameongeza.
Marehemu ameacha mjane, watoto
na wajukuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: