BARAZA
la Habari Tanzania (MCT), limearifiwa kuwa Mwandishi wa Habari wa
Kituo cha Televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi
ameuawa kwa bomu la machozi.
Katibu
Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema hayo wakati wa ufunguzi wa
mafunzo ya wahariri pamoja na mameneja wa vyombo vya habari yaliyoanza
mkoani Morogoro jana.
Mukajanga
alisema baada ya kupata taarifa za awali za kifo cha Mwangosi, ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (
IPC), alilazimika kumtafuta kwa njia ya simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi.
Alisema
katika mazungumzo yao, Dk Nchimbi alimfahamisha kuwa yupo nje ya nchi,
Afrika Kusini kikazi na kukiri kupata taarifa za kifo hicho.
Mukajanga
alinukuu mazungumzo yake na Waziri huyo kwa kusema; “Nimepata taarifa
za kifo hicho na taarifa za awali zimesema ni bomu la machozi
halikulipuka kitaalamu na limemuua (Mwangosi) na kuwajeruhi watu wengine
wa tatu.”
Alisema Dk Nchimbi alitoa rambirambi kwa waandishi wote wa habari nchini kutokana na kifo cha mwandishi mwenzao.
Kauli
zakinzana “Hapa tunaona kauli ya Waziri inapishana na Polisi ambao
wanadai amekufa kwa kupigwa na kitu kilichorushwa, wakati Waziri anadai
ni bomu la machozi ambalo halikulipuka kitaalamu na kusababisha kifo na
majeruhi watatu,” alisema Mukajanga.
Alisema MCT imefedheheshwa kwa kuwa mwandishi aliyeuawa, alikuwa kazini akitekeleza wajibu wake wa kukusanya habari.
Mbali
ya kufedheheshwa huko, Mukajanga alisema mauaji hayo yametoa picha
mbaya kwa Tanzania wakati huu ambao wajumbe wa Umoja wa Mabaraza ya
Habari Duniani wapo nchini kwa ajili ya mkutano ambao Tanzania ni
mwenyeji.
“Mimi
ni Makamu wa Rais wa Mabaraza ya Habari Duniani, nimefedheheka sana
kwa tukio hili, limefanyika wakati wajumbe kutoka nchi mbalimbali
duniani wa mabaraza ya habari wapo hapa nchini kuhudhuria mkutano…
wanakutana na vichwa vya habari kwenye magazeti na televisheni kuhusu
kuuawa kwa mwandishi wa habari akiwa kazini,” alisema Mukajanga.
MCT
imewataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari ikiwemo kulindwa na
Serikali wanapokuwa kazini. Alisema mauaji hayo yameandika historia
mbaya na ya kwanza tangu kupata Uhuru.
“Kwa
mara ya kwanza tangu Uhuru mwandishi wa habari anauawa akiwa kazini
kutekeleza wajibu wake ... tukio hili limetoa sura kwamba waandishi wa
habari wanatakiwa kupatiwa mafunzo ya kuchukua tahadhari kwenye matukio
ya hatari,“ alisema Mukajanga. HABARI NA TSN
Toa Maoni Yako:
0 comments: