Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
 
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kukuza na kuimarisha miundombinu ya kiusalama kwenye Sekta ya Utalii ili kuwafanya wageni wanaitembelea Zanzibar kuwa salama wakati wote wanapokuwa hapa nchini.

Ahadi hiyo imetangawa za Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Zanzibar Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, wakati akifunga maunzo kwa Askari wa Kikosi kazi cha Doria ya Utalii yaliyokuwa yakiendeshwe kwenye Chuo cha Polisi cha Zanzibar.

Mafunzo hayo ya pamoja ya miezi miwili, yamewashirikisha Maafisa na Askari kutoka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji (KZU, Kiukosi Maalum cha Kuzuia Magendo (MKMK), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Chuo cha Mafunzo(Magereza), Kikosi cha Valantia (KVZ) pamoja na Maafisa wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.

Waziri Mwinyihaji amesema kuwa kuanzishwa kwa kikosikazi hicho kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kulinda usalama wa watalii wanaoitembelea nchi na watakapoondoka wataweza kuvuta wageni wengine na hivyo kuimarisha utalii na kukuza pato la Taifa.

Amesema kuwa kutokana na kwamba zaidi ya aslimia 70 ya wananchi wa Zanzibar wameajiriwa na kunufaika na Sekta ya Utalii ambao pia unaliingizia taifa zaidi ya aslimia 80 ya pato la uchumi, Serikali ya Zanzibar imeazimia kuhakikisha kuwa inajenga mazingira mazuri ya kuimarisha usalama kwa wageni wote wanaoingia hapa nchini.

Naye Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amesema kuwa kuanzishwa kwa mafunzo hayo ya kikosikazi cha Utalii, kunatokana na mawazo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Janerali Saidi Mwema, ya kuanzisha kwa cha Polisi kinachoshughulikia masuala ya Utalii.

Kamishna Mussa amesema kuwa Mafunzo hayo ambayo yana baraka zote za Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, yamewajengea wahitimu hao uwezo wa kiutendaji na moyo wa kuaminiana kati ya askari wa kikosi kimoja na kingine pamoja na wale wa kamishneni ya Utalii.

Awali Mkuu wa Chuo cha Taalum ya Polisi Zanzibar SSP Ramadhani Mungi, alisema kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamepatiwa mafunzo mbalimbali yakiwemo ya ukamataji salama, Polisi Jamii pamoja na lunga mbalimbali za kigeni kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kitaliano na Kispanyola lugha ambazo zitawawezesha kuwasiliana vema na wageni wanapokuwa na matatizo ama kutaka kujua jambo kutoka kwao.

Amesema wakufunzi wa Chuo cha Jeshi la Polisi Zanzibar pia wamepata msaada wa kitaaluma kutoka kwa wakufunzi wenzao wa Chuo cha Maendeleo cha Utalii kilichopo Maruhubi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkuu wa Chuo hicho ASP Ali Abdallah Kitole, amesema kuwa majukumu makubwa ya askari hao ni kusaidia kuzuia uhalifu dhidi ya watalii, kubainisha, kuzuia na kushughulikia uhalifu na jinsi ya kutawala kiusalama eneo lenye watalii wengi.

Nao baadhi ya wawekezaji na viongozi mbalimbali wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar wameelezea matumaini yao kwa Serikali ya Tanzania katika kujiimarisha kwa ulinzi wa watalii hapa nchini.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: