Na Juma Mohammed, MAELEZO Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Julai 19 hadi Julai 21 kufuatia maafa ya ajali ya Meli ya Mv. Skagit  iliyozama karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein akitangaza maombolezo hayo, alisema bendera zote zitapepea nusu mlingoti na kwamba shughuli za sherehe na burudani zimefutwa kwa muda wa siku tatu za maombolezo.

Dk. Shein alisema shughuli za Serikali zitaendelea kama kawaida. Katika taarifa yake aliyoitoa Ikulu usiku wa kuamkia Julai 19, Rais Dk Shein amewahakikishia wananchi na hasa waliopoteza jamaa zao kuwa Serikali itabeba gharama zote za mazishi na pia kugharamia huduma za matibabu kwa majeruhi.

“Nimesikitishwa sana na msiba huu, Katika wakati huu si vema tukaanza kulaumiana jambo la muhimu hivi sasa  ni kuokoa maisha ya watu” Alisema Rais Dk. Shein.

Mbali ya taarifa hiyo, Rais Dk Shein aliungana na wananchi, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, Viongozi wa dini katika kutambua maiti zilizofikishwa katika eneo maalum la viwanja vya Maisara Suleiman.

Mbali ya kwenda katika viwanja hivyo, pia alifika katika eneo la bandari ya Zanzibar kufuatilia taarifa za tukio hilo. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilisitisha shughuli zake kufuatia maafa hayo ambapo wakati wa jioni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi alitarajiwa kufanya majumuisho ya bajeti yake.

Baadhi ya Wabunge wakiongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Jeshi la Polisi walitembelea majeruhi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na eneo la viwanja vya Maisara ambapo maiti hufikishwa kwa ajili ya utambuzi.

Mbali ya Bunge, pia Baraza la Wawakilishi Zanzibar jana lilisitisha kwa muda shughuli zake ili kutoa nafasi kwa Wawakilishi hao wa wananchi kushiriki katika shughuli  za uokozi ambapo wengi walifika bandarini kusaidia kazi mbalimbali ikiwemo kuwafariji waliopoteza ndugu zao.

Taarifa kutoka Mamlaka za Serikali zinaeleza kwamba hadi asubuhi hii maiti 30 zilipatikana ambapo 20 kati ya hizo zimetambuliwa na kuchukuwa na jamaa zao huku wananchi wengine wakiendelea na kuzitambua maiti zinazofikishwa katika eneo la Maisara.

Aidha, katika taarifa hiyo, watu 145 wameokolewa wakiwa hai, wengi wao wapo katika hali nzuri wameruhusiwa kuungana na familia zao baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Zanzibar.

Meli ya Mv. Skagit ilizama  Julai 18,2012 saa 7:50 mchana ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa imebeba abiria 250 watu wazima, watoto 31 na mabaharia 6.

Kazi ya  utafutaji na uokoaji zinaendelea asubuhi hii  katika eneo la tukio ilikozama meli hiyo umbali wa maili sita Kusini mwa Kisiwa cha Yasin karibu na Kisiwa cha Chumbe Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: