Hakika kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN Ki-moon kwa kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha maisha yangu ya utumishi wa umma. Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.
Utumishi wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee. Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na madhila makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia, kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mazingira magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa.
Daima nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi wangu. Nawashukuru sana.
Hapana shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha kufahamiana kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali mbali waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani thamani ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya mwanawe.
Maendeleo
Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa utendaji wa Sekretariati na kuimarisha uongozi wa Umoja Mataifa katika medani za uchumi na maendeleo ya jamii. Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu yaliongezeka kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering as One - DaO) ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zetu hususan za maendeleo.
Kwa bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda. Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama kubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo kama kilingo cha msingi katika kutokomeza umaskini.
Katika kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs Integrated Implementation Framework ). Ninaona fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa umekamilika ambapo Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara ya kwanza mfumo huu umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wote kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na kifedha. Hapana shaka utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za maendeleo.
Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la Kuhimiza Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika (MDG Africa Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza kikosi-kazi (MDG Africa Working Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya miaka mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa mapendekezo kamambe ya utekelezaji. Endapo mapendekezo haya yatazingatiwa basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na mikakati madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa ujumla. Napenda kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba mwaka 2013. Hata hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi duniani, hususan barani Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii nyingi zimenufaika na utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za kujiletea maendeleo stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.
Mkutano wa Rio + 20
Ni jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika hivi karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka 2015, mwaka uliokusudiwa kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilipokabidhiwa jukumu la kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia makubaliano katika masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri kwa wanawake na wasichana.
Uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika kuendelea na juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia. Wakati wa utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi kushughulikia suala hii. Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza sauti za wanawake na wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana. Tumezihimiza mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa kushika nafasi za uongozi katika jamii. Ndiyo maana kwa upande wetu hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa idara inayojulikana kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa Mataifa iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na wasichana.
Huduma ya Pamoja
Kwa upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote waliomo katika utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia ujuzi na weledi wao wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii tunazozihudumia. Natoa shukrani za pekee kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya Makao Makuu na ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo nyingi. Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo cha kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One) Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”. Ni dhahiri kwamba uwezo wa nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa imara zaidi pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa Mataifa na fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa maendeleo. Wakati uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa utaratibu wa kutoa “Huduma ya Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye tija.
Nchini mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia mpango mmoja uitwao “Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan – UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani Julai 1 hadi Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.
Afya ya Jamii
Katika eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo wanaathirika zaidi, hatua muhimu zinachukuliwa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila mtoto anakingwa na maradhi, hususan kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu Ban Ki-moon, Michel Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia mfano hai wa jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na mwanamke aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu waliozaliwa bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya ya mama na mtoto (Commission on Information and Accountability on Women's and Children's Health) ambayo iliendeshwa kwa umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani kwamba jumuiya ya kimataifa hivi sasa imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji, usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka kwamba mfumo huu utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi karibuni.
Hali kadhalika, kazi nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde Osotimehin, na Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuboresha afya ya mama na mtoto. Matokeo ya jitihada za wenzangu hawa yalikuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Naibu Katibu Mkuu katika nyanja zote za maendeleo. Ama kwa hakika matunda ya kazi zao yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa Mataifa ni Shirika lenye umuhimu mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo, unasaidia sana katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na imani kama hiyo nikiwa katika ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa Montevideo, Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu Michelle Bachelet, Helen Clark na Alicia Barcena, tulisimama kidete kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko ambalo lilikuwa kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha takriban karne moja, nilikutana na watu ambao walikuwa wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia nzima, waliopata ulemavu wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu hawa walikuwa na nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na wa wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru Laos, ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na wadau wengine wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuisaidia Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya “cluster munitions”.
Hii ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa Mataifa.Ujumbe wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote duniani ni mashuhuda na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa. Kwa wanyonge na wahitaji walio wengi Shirika hili ni nguzo ya kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za kujiletea maisha yenye utu na heshima.
Mageuzi katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu. La hasha! Ndiyo maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza kikamilifu kwenye kuboresha masuala ya utawala, uendeshaji na namna tunavyofanya kazi. Ni wazi kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa umebadilika kutoka chombo cha huduma za mikutano na kuwa mtendaji mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa ushirikiano na msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika kuhamasisha mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na kujenga desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku tukitumia rasilmali chache.
Ilitubidi pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza. Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na njia ya mkato wala njia mbadala ya kuliimarisha Shirika letu na kulifanya liwe la kisasa zaidi katika kutekeleza majukumu yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda sambamba na changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti, misimamo tofauti na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi ili kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba raslimali chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila tulipoendelea na jitihada za kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kwa kuwapatia fursa za mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini. Ni jambo lililo dhahiri kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza majukumu yao katika mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara. Tunafahamu, tena kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa - “bendera ya bluu” - hivi sasa si kinga tena. Haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja, Nigeria, ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la kigaidi la tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu wanapotangulia mbele ya haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu ya maisha. Ni faraja kubwa kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo tuliyasimamia kabla ya kumaliza utumishi wangu ni kuanzisha mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia wahanga wa majanga hayo pamoja na familia zao.
Utawala wa sheria
Mojawapo ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga kulinda haki za binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele suala la kuimarisha utawala wa sheria, hususan kufuatia umuhimu wake katika ajenda za ujenzi wa amani (peace-building) na maendeleo stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi nilipopata fursa ya kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa utekelezaji wa shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama. Kwa upande wao nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni kuendeleza jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani na kujenga amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia tamati, naamini hakuna tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi na maadili ya Umoja wa Mataifa. Ili mradi bado kuna umaskini duniani na mahitaji ya chakula; bado kuna changamoto ya kutunza utu na heshima ya binadamu na haja ya kuimarisha amani duniani basi hakika nitaendelea kuunga mkono jitihada, misingi na malengo ya Umoja wa Mataifa popote pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri kwamba njia bora ya kukabiliana na changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni kujenga ubia na ushirikiano wa karibu baina ya serikali, asasi za kiraia, wafanyabiashara, mashirika ya hisani, taasisi za kitaaluma na watu binafsi.
Aidha, ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa na kiu ya kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani, watauchukulia Umoja wa Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga mustakabali wao.
Toa Maoni Yako:
0 comments: