Deidre Lorenz akimkabidhi picha ya Ground Zero (New York) Rais wa Mt. Kili Marathon 1991 Onesmo Ngowi baada ya kukimbia mbio hizo.
Deidre Lorenz akiwa anahojiwa na waandishi wa Habari mjini Moshi.
---
Na Grace Soka, Afisa Uhusiano
MT. KILIMANJARO MARATHON 1991
Mcheza sinema maarufu wa Marekani Deidre Lorenz ameahidi kuleta wacheza sinema wenzake na kushiriki kwenye mbio za mwaka kesho za mt. Kilimanjaro Marathon zitakazokuwa zinatimiza miaka 23 tangu zianzishwe mwaka 1991.
Lorenz aliyekimbia mbio za mwaka huu ambazo zilipewa jina la “mbio za kutimiza miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika” na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) amesema kuwa atakuja na timu yake ya wapiga picha ili kupiga picha vivutio kadhaa vya Tanzania ikiwa ni pamoja na mlima Kilimanjaro. Qwiji hili la sinema za Santorini Blue, The Great Fight, Perfect Strangers na nyingine nyingi ameelezea kuipenda sana Tanzania.
“Sikutegemea kuikuta nchi nzuri kama hii” alisema mcheza sinema huyo ambaye ameshawahi kuchaguliwa zaidi ya mara 4 kugombea tuzo maarufu za Oscar. “Sasa nimeamini kuwa mlima Kilimanjaro ni mali ya Tanzania na nitautangaza katika sinema zangu zote” aliendelea kusema Deidre Lorenz.
Mcheza sinema huyu ambaye ameingia kwenye mkataba na kampuni kubwa ya Google hivi karibuni ili kuuza sinema zake katika mtandao aliielezea Tanzania kama nchi nzuri na yenye watu wakarimu sana.
Mbio za Mount Kilimanjaro Marathon zilianzishwa mwaka 1991 na Marie Frances anayetoka katika jiji la matajiri la Bethesda nchini Marekani baada ya kuombwa na balozi wa zamani wa Tanzania nchini Misri. Tangu kuanzishwa kwake mbio hizi zimekuwa zinaleta watalii matajiri katika mji wa Moshi kupanda mlima Kilimanjaro na kukimbia mbio hizi zinazojulikana kama Seven Continental Races.
Hakuna masharti yote ya kukimbia mbio hizi na watanzania wanaoshiriki katika mbio hizi huwa hawatozwi pesa za kiingilio.
Kwa kutambua mchango wake katika uchumi wake Manispaa ya Moshi iliibadilisha jina barabara ya zamani ya Bustani Ale na kuiita Marie Frances Boulevard ili kumuenzi mama huyu aliyejitolea maisha yake kuutangaza mlima Kilimanjaro.
“Kila siku napokea ujumbe kutoka nchi mbalimbali niende huko kuanzisha mbio za marathon lakini kwa sasa basi” alisema mama huyo aliyekuwa mtayarishaji wa vipindi vya televisheni ya ABC kabla ya kunzisha Mt. Kilimanjaro Marathon.
Alisema kuwa mwaka jana yeye na Rais wa klabu ya Mt. Kilimanjaro Marathon mtanzania Onesmo Ngowi walifanya makubaliano ya Ethiopia Airlines (ET) jijini Addis Ababa kuzifanya mbio hizo kuwa za kimataifa zaidi. “ET walikubali kutoa ufadhili kwetu na pia kugharamia kushiriki kwetu katika mbio za New York Marathon, Boston Marathon na Los Angelos Maratthon ili kuitangaza vyema Tanznaia” alibainisha Frances.
Katika makubaliano hayo, Ngowi na Frances pia wataanzisha mbio za “King Solomon Marathon” zitakazofanyika katika jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia.
Deidee Lorenz amefungua pazia kwa watu mashuhuri kushiriki katika mbio za marathon nchini Tanzania na ni jukumu la Watanzania kuchangamkia fursa zinazoletwa na ujio wao.
Toa Maoni Yako:
0 comments: