Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepiga marufuku mikusanyiko ya aina yoyote ikiwemo mihadhara ya aina mbalimbali ambayo haijapata kibali cha Serikali.

Akitoa taarifa ya Serikali,Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ,Mohammed Aboud Mohammed amesema mbali na suala hilo,pia imewataka wananchi kuheshimu sheria.

Waziri Aboud amesema pia Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika na fujo zilizotokea jana na leo katika mji wa Zanzibar.

“Serikali inakemea vikali vitendo vyote vya hujuma na uharibifu wa mali zilizofanywa katika taasisi za umma, Dini na watu binafsi” Alisisitiza Waziri huyo.

Serikali imetoa mkono wa pole kwa wale wote walioathirika na vurugu hizo ikiwemo Taasisi na wananchi kwa ujumla na imeahidi kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika kufanya vurugu hizo.

Katika hatua nyengine, Waziri Aboud alisema Serikali inawaomba wazazi kuwadhibiti vijana wao kutojiingiza katika vitendo vya viovu ikiwa pamoja na vurugu,hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka sheria na taratibu za nchi.

“Tunawaomba wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida na Serikali itaendelea kuhakikisha amani na usalama wakati wote” Alisema Waziri Aboud katika taarifa yake aliyosoma mbele ya vyombo vya habari katika studio za Shirika la Utangazaji Zanzibar.

Katika taarifa yake,wananchi pia wameombwa na Serikali kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za wahalifu na wale wote wanaotaka kuvunja amani katika jamii.“Tunawaomba wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale ambapo itaonekana zipo dalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao” Alitoa wito Waziri Aboud.

Katika taarifa hiyo,Serikali imewakumbusha viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam na Jumuiya nyengine kufuata taratibu ikiwa wanataka kufanya mikutano au mihadhara inayojadili suala zima la kuandikwa kwa katiba ya Jamhuri ya Tanzania.

Awali, Waziri huyo alisema Serikali iliwaita viongozi wa uamsho kuzungumzia namna bora ya kufanya mikutano inayozungumza wanaotaka kuendesha mijadala ya katiba mpya kwamba watalazimika kufuata sheria na taratibu za Tume ya Katiba iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: