Na Pardon Mbwate na Felister Chubwa wa Jeshi la Polisi Kigoma

Askari Polisi mmoja wa Kikosi cha Mawasiliano cha Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma Kostebo Shaban Hamisi Gobeka(37), amefariki dunia papo hapo baada ya pikipiki aliyokua akiendesha kuacha njia na kugonga mti kushoto pembeni mwa barabara ya Lumumba mjini Kigoma.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma Kamishns Msaidizi ACP Frasser Kashai, amesema kuwa ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 12.15 jioni katika mtelemko mkali eneo la Lubengela wakati askari huyo akiendesha pikipiki yenye namba T.757 BYY aina ya Toyo akitokea Mwanga kuelekea Kigoma mjini.

Kamanda Kashai amesema wakati wa ajali hiyo Kostebo Gobeka mwenye namba F. 1561 alikuwa amempakia kijana mwingine aitwaye Filbert Kibuka(25) mkazi wa Mwanga mjini Kigoma ambaye yeye amejeruhuwa vibaya na amelazwa katika Hospitali ya mkoa Maweni kwa matibabu zaidi na hali yake imeelezwa kuwa ni mbaya.

Amesema ingawa Polisi bado inachunguza chanzo cha ajali hiyo, lakini imebainika kuwa imesababishwa na mwendo kasi uliotokana na kukatika kwa bleki ya pikipiki hiyo huku ikiwa kwenye mteremko mkali.

Kamanda Kashai amesema Konstebo Gobeka alikuwa ni dereva wa kutumainiwa wa pikipiki za Polisi na alipata mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki ambapo kabla ya kuhamishiwa kikosi cha mawasiliano ya Polisi mkoani hapo, marehemu alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa wakiendesha pikipiki za doria mkoani Kigoma na hakuwa na kumbukumbu zozote za ajali.

Hata hivyo Kamanda Kashai amesema Jeshi la Polisi limempoteza Askari shupavu na mchapakazi lakini pia amesema pikipiki aliyopatanayo ajali Askari huyo haikuwa mali ya Jeshi la Polisi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: