Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi - Moshi

MOSHI IJUMAA MACHI 30, 2012. Serikali imeahidi kuendelea kuliboresha Jeshi la Polisi ili liweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi katika maeneo mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo mjini Moshi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mh. Mbara Abduluwakuili wakati wa hafula ya kufunga mafunzo kwa Askari wapya wa Jeshi la Polisi yaliyokuwa yakifanyika kwenye Chuo cha Taaluma ya Jeshi la Polisi Moshi (Moshi Police Academy).

Mh. Abduluwakili amesema kutokana na mabadiliko ya Kisayansi, hali ya uhali ya uhalifu nayo imekuwa ikibadilika kutokana na mazingira hayo na hivyo aina na mbinu za uhalifu nazo zimebadilika na hakuna budi sasa kwa Jeshi la Polisi nalo likabadilika kimbinu na kujiongezea ujuzi zaidi ili kuwashinda wahalifu.

Amesema pamoja na changamoto hizo, lakini kwa siku za hivi karibuni, Jeshi la Polisi limeweza kupata mafanikio makubwa katika Nyanja mbalimbali hasa kwenye suala la kupambana na wahalifu wakiwemo wakorofi na wale wanaotumia silaha za moto na hata kuwashinda na kuwatia nguvuni.

Amesema hivi sasa hata takwimu za makosa ya Jinai yanayoripotiwa katika vituo mbalimbali vya Polisi yamepungua hali inayoonyesha kuwa hali ya uhalifu nayo imepungua kwa kiasi kikubwa.

Amepongeza juhudi zinazofanywa na makamanda wa Polisi wa Mikoa chini ya Uongozi wa Mkuu wa Jeshi hilo Inspekta Jenerali Saidi Mwema katika kuhakikisha kuwa hali inazidi kuwa salama na utuliu kuongezeka siku hadi siku.

Kuhuusiana na ajali za barabarani, Mh. Abdulwakili, amewata Polisi kuhakikisha kuwa wanaendeleza juhudi zao za kupambana na madereva wakorofi na hata ikiwezekana kuwanyang’anya leseni kwa madereva na kuyaondoa barabarani magari mabovu ili kuepusha ongezeko la ajali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta  Jenerali Saidi Mwema,  amesema kuwa Jeshi la Polisi limejipanga ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki na chaguzi nyingine ndogondogo kwa nafasi za udiwani hapa nchini zinafanyika kwa amani na utulivu.

Amewataka wananchi waliopo kwenye maeneo ya upigaji kura waweze kupiga kura zao na kurudi majumbani kusubiri matokeo na kuepuka kufanya vurugu kwani kwa kufanya hivyo watalilazimisha Jeshi la Poilisi kuwachukulia hatua za kisheria.

Akizungumzia kazi inayowakabili askari hao wapya, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Saidi Mwema amesema kuwa kazi ya Polisi ni kuhakikisha kuwa inapambana na changamoto mbalimbali na amewataka kuzigeuza changamoto hizo ili ziwe ni fursa ya kutumia rasilimali chache zilizopo kwa kuleta mafaniko ya kiutendaji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Awali akitoa taarifa ya Mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi cha Moshi ACP Matanga Mbushi, amesema kuwa pamoja na mambo mengine, wahiitimu hao wamejifunza kazi za Polisi, utoaji wa huduma bora kwa mteja anayefika katika kituo cha Polisi, Polisi Jamii na sheria mbalimbali za kitaifa na za Kimataifa.

Jumla ya Askari Polisi 3264 wakiwemo wanaume 2373 na wanawake 891wamehitimu mafunzo yao ya awali ya miezi sita na kupangiwa kazi katika mikoa mbalimbali.

Sherehe hizo ambazo pia zilihudhuliwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa na Wakuu wa wilaya za mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Wakuu wa Vyuo vya Polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji na wananchi, zilitanguliwa na Mgeni Rasmi kukagua gwaride na kutoa zawadi kwa askari 12 waliofanya vizuri zaidi ya wengine kabla ya kuona maonyesho ya Ujasiri na utayari wa wahitimu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: