Na Mwandishi Wetu, Gazeti la Tanzania Daima
Mtanzania, Abdul Karim, amekamatwa na kuswekwa katika Gereza la Mpimba jijini Burundi katika mazingira ya kutatanisha.
Kukamatwa kwa Mtanzania huyo kumezua utata kwa kuwa tangu mwaka 2005 amekuwa akiidai Serikali ya Burundi mamilioni ya fedha bila mafanikio, kiasi cha kuilazimisha Serikali ya Tanzania kuingilia kati.
Nyaraka kadhaa zilizopatikana na Gazeti la Tanzania Daima, zimeonyesha kuwa Karim anadai Serikali ya Burundi faranga (fedha za Burundi) milioni 547.895 na deni jingine la faranga bilioni 1.714, ambazo inadaiwa zimetokana na kuliuzia Jeshi la Polisi bidhaa.
Inadaiwa wiki tatu zilizopita, Mtanzania huyu ambaye anamakazi ya muda jijini Bujumbura, alikamatwa na askari polisi akiwa ofisini kwake na kuchukua baadhi ya nyaraka muhimu na kumpeleka katika kituo cha polisi na kisha kumweka katika Gereza la Mpimba.
Inadaiwa kuwa kukamatwa kwake kunahisiwa kuwa ni njama za kutaka kumnyamazisha Mtanzania huyo asifuatilie fedha zake ambazo hajalipwa kwa miaka saba sasa, pamoja na juhudi nyingi za kuonana na viongozi wa juu wa Burundi.
Inadaiwa Karim katika kuhangaika malipo yake. alimwandikia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, akimwomba kuingilia kati ili Serikali ya Burundi iweze kumlipa fedha zake.
Katika barua yake ya Septemba 3, 2010, Karim alimwambia Membe kuwa amekuwa akisumbuliwa kulipwa fedha zake kutokana bidhaa mbalimbali alizolipa Jeshi la Polisi la nchi la nchi hiyo, licha ya jitihada za baadhi ya maofisa kumsaidia.
Waziri Membe aliingilia kati na katika barua yake ya Novemba 21, 2011, alimwandikia Waziri wa Mambo ya Nje ya Burundi, Balozi Laurent Kavakure, alimwomba kumsaidia Karim kulipwa fedha hizo.
Membe katika barua hiyo amemtahadharisha Waziri mwenzake wa Burundi kulichuulia kwa Uzito suala hilo, kwa kuwa linaweza kuathiri mahusiano baina ya nchi hizi mbili, na kuwafanya wafanyabiashara na wawekezaji kuingiwa hofu.
Pamoja na Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania kuingilia kati, hakuna ulipwaji wowote uliofanywa na sasa Mtanzania huyo yupo Gerezani.
Jitihada za umpata Waziri Membe jana zilishindikana, kwa kuwa simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: