Rais Jakaya Mrisho Kikwete |
Ndugu Wananchi,
Naomba sote tumshukuru
Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutuwezesha kuzungumza tena mwisho wa
mwezi huu. Katika mwezi tunaoumaliza leo taifa letu lilipata msukosuko
mkubwa kufuatia mgomo wa madaktari. Nashukuru mgomo huo umeisha lakini
makovu yake yatabaki maisha katika kumbukumbu za historia ya taaluma ya
tiba hapa nchini.
Leo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amenipa taarifa kuwa Kamati aliyounda
kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha
taarifa yake kwake. Kuanzia kesho Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo
na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo. Nawaomba ndugu zetu
madakatari kuwa na moyo wa subira. Napenda kutumia fursa hii
kuwahakikishia ndugu zetu madaktari na watumishi wengine wote wa sekta
ya afya kwamba Serikali inatambua, inajali na kuthamini kazi wazifanyazo
na mchango wao katika kulinda na kudumisha afya za wananchi wa
Tanzania. Aidha, narudia kutoa pole zangu za dhati kwa wananchi na hasa
wagonjwa nchini kwa mateso waliyoyapata katika kipindi cha mgomo. Ni
matumaini yangu kuwa hali kama ile haitajirudia tena katika nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio lingine la kusikitisha ni mauaji ya
Songea. Yapo yale yanayohusishwa na imani za ushirikina, na yapo yale
ambayo yalitokea kwenye maandamano. Napenda kutumia nafasi hii kuelezea
masikitiko yangu kwa vifo hivyo na kutoa pole na rambirambi zangu na za
wananchi wa Tanzania kwa ndugu wa marehemu wetu hao. Tupo pamoja nanyi
katika misiba hii mikubwa na majonzi. Napenda kuwahakikishia wananchi
wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama imekuwa
inafanya na itaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji haya mpaka
wahusika wote wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Nimearifiwa kuwa, mpaka sasa kwa mauaji 13 yanayohusishwa na imani za
ushirikina watuhumiwa 26 wamekwishakamatwa. Na kwa mauaji yaliyotokana
na maandamano, askari polisi wanne wamekamatwa na upelelezi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Nashukuru kwamba amani na utulivu
vimerejea katika Manispaa ya Songea. Nawapongeza sana viongozi wa ngazi
zote na wananchi kwa ujumla kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuwezesha
usalama na utulivu kupatikana. Tafadhali endeleeni na juhudi hizo mpaka
mambo yatengemae kabisa.
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu pia, Bunge letu Tukufu
lilifanya mkutano wake wa sita na miongoni mwa maamuzi makubwa
yaliyofanywa ni kupitisha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya mwaka 2011 hususan kuhusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya
Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba ya nchi. Nimekwishatia saini
marekebisho hayo tarehe 20 Februari, 2012 na hivyo sasa yako tayari
kutumika.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi kwa Wabunge wetu kwa kazi
kubwa na nzuri waliyoifanya ya kupitisha marekebisho hayo. Aidha, natoa
pongezi maalum kwa vyama vya siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR -
Mageuzi pamoja na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa
maoni na mapendekezo yao ambayo ndiyo yalikuwa chachu ya marekebisho
yaliyofanyika. Pia, nawashukuru kwa ushirikiano wao uliowezesha
mafanikio kupatikana.
Tulipotoka
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka
mtakumbuka kuwa baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadikiko
ya Katiba tarehe 18 Novemba, 2011, kulikuwepo na maneno mengi na maoni
mbalimbali katika jamii. Wapo baadhi ya wadau hasa baadhi ya vyama vya
siasa na asasi za kiraia ambao waliniomba nisitie sahihi Muswada huo
kuwa Sheria na badala yake niagize Bunge liuzungumze upya. Aidha, vyama
vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR – Mageuzi na Baraza la Taifa la
Asasi Zisizokuwa za Kiserikali waliomba kukutana nami tuzungumzie
mchakato mzima wa Katiba. Sikusita kuwakubalia na kwa nyakati
mbalimbali tulikutana na kuzungumza nao.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yangu nao niliwaeleza
ugumu niliouona kuhusu kuacha kutia sahihi Muswada huo na kuurudisha
tena Bungeni kujadiliwa upya. Nilichelea kuliingiza taifa letu katika
mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba usiokuwa na lazima. Mgogoro ambao
tunaweza kuuepuka kwa kutumia njia nyingine za kikatiba na kisheria
kufikia malengo yale yale. Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi
kingejenga chuki kwa upande wa Wabunge walio wengi ambao waliujadili
Muswada na kuupitisha. Wengeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana
hawana thamani.
Katika mazingira hayo mtakapowarudishia Muswada huo kuujadili kuna
hatari ya kutokupata ushirikiano wao na kushindwa kupata kile
kinachotarajiwa. Wanaweza kujadili na kuamua kukataa mapendekezo yote
mapya na kubakia na msimamo wao ule ule.
Ndugu Wananchi;
Kwa ajili hiyo, busara ilinielekeza kuwa
tusitumie njia hii bali tutumie njia za kawaida za kufanya marekebisho
ya Sheria zilizotungwa na Bunge. Hakuna Sheria iliyotungwa na Bunge
ambayo haiwezi kufanyiwa marekebisho. Kinachotakiwa ni kupeleka
mapendekezo ya vifungu au vipengele vya Sheria husika vinavyotakiwa
kurekebishwa. Bunge litavijadili na kama hoja zinatosheleza vitafanyiwa
marekebisho. Mimi nilipendelea busara na hekima hiyo. Niliwaeleza
wadau sababu za kuamua kutia sahihihi Sheria na kuwasihi wakubali
tufanye lililo bora zaidi ambalo ni kupeleka Bungeni mapendekezo ya
sheria hiyo katika maeneo ambayo tunataka marekebisho hayo yafanywe.
Nilitahadharisha kuwa hata kufanya hivyo kunaweza kuwa na ugumu
wake hasa pale dhana zisizokuwa sahihi zitakapopandikizwa kwa Wabunge.
Niliwaomba tushirikiane kuhakikisha dhana potofu hazijitokezi na
zinapojitokeza tuzisahihishe. Niliwahakikishia utayari wa Serikali
kushirikiana nao katika hatua zote, tangu kutayarisha mpaka kuwasilisha
mapendekezo hayo Bungeni iwapo watapenda Serikali ifanye hivyo. Aidha,
niliwaambia kuwa hata sisi Serikalini tulikuwa na dhamira ya kupeleka
marekebisho kwa baadhi ya vifungu vya Sheria hiyo kwa sababu mbalimbali.
Nafurahi kwamba, kwa pamoja licha ya tofauti zetu kuhusu uamuzi
wangu wa kutia saini Muswada tulikubaliana kushirikiana kutoa
mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo, ambayo tuliyawasilisha katika
Bunge lililopita. Nafurahi na kufarijika kwamba, baada ya mjadala
mkali, na Wabunge kufanya marekebisho kadhaa na hata kuingiza mambo
mengine mapya, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ulipitishwa na Bunge tarehe 10 Februari, 2012. Baadaye uliwasilishwa
kwangu na nikatia sahihi kuwa Sheria tarehe 20 Februari, 2012. Sina
budi pia kukitambua Chama cha Mapinduzi ambacho kilileta mapendekezo
yake. Mapendekezo hayo yalizingatiwa kama ilivyofanywa kwa yale ya
wadau wengine.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa
pongezi maalum kwa vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi na
CCM na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa uelewa wao
na ushirikiano wao kulikotuwezesha kufikia hapa tulipo katika mchakato
wa kutengeneza Katiba Mpya kwa usalama, utulivu na kwa maelewano.
Kwa kweli, jinsi hali ilivyokuwa huko nyuma, hatuna budi kushukuru na
kujipongeza. Ni matumaini yangu na rai yangu kuwa tutaendeleza
ushirikiano na utamaduni huu wa mazungumzo tuliouanzisha na kuutumia
katika hatua zingine zinazofuata.
Nchi imetulia joto na jazba kuhusu Katiba havipo. Kumbe tukiamua
na hasa tukizungumza inawezekana. Naomba wadau wote tuazimie kuwa mambo
yaendelee hivi hata katika hatua zijazo za mchakato huu na masuala
mengine muhimu kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Katika
mazungumzo yetu na wadau tulikubaliana kwamba tushughulikie marekebisho
ya Sheria hii kwa awamu. Kwa kuanzia tushughulikie mambo yanayohusu
Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi Kuhusu Katiba ili iundwe
na kuanza kazi. Baada ya hapo tuangalie mambo yahusuyo Bunge Maalum na
Kura ya Maoni.
Bahati nzuri Sheria ya sasa inaelekeza kuwa Kura ya Maoni
itatungiwa Sheria yake maalum, hivyo mambo yanaweza kusubiri wakati huo.
Hivyo basi, baada ya muda si mrefu, Serikali na wadau tutaanza
mazungumzo kuhusu mapendekezo ya marekebisho kuhusu Bunge Maalum. Kama
yatakuwepo na kama kutafikiwa makubaliano, mapendekezo yatafikishwa
katika Bunge letu tukufu kwa hatua zipasazo.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri pia kuna kipindi kirefu
kidogo wakati Tume inaendelea na kazi yake mpaka hapo Bunge Maalum
litakapoanza kazi. Tume imepangiwa kukamilisha kazi yake ndani ya miezi
18 na inaweza kuongezwa miezi miwili. Wadau wanaweza kutumia sehemu ya
muda huo wa Tume kushughulikia na kufanya marekebisho yahusuyo Bunge
Maalum. Hata hivyo, kama mapendekezo yatakamilika mapema ni bora zaidi
yafikishwe Bungeni na kushughulikiwa ipasavyo.
Wadau Kupendekeza Majina
Ndugu Wananchi;
Miongoni
mwa marekebisho muhimu yaliyofanywa katika Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba katika Bunge lililopita ni kuwekwa kwa utaratibu wa wadau
kupendekeza kwa Rais majina ya watu wanaoona wanafaa kuteuliwa kuwa
Wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni kuhusu Katiba. Nafurahi
kutoa taarifa kwamba nimekwishatoa mwaliko kwa wadau husika, yaani vyama
vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia
pamoja na jumuiya, taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana
kuleta mapendekezo hayo.
Mwaliko wangu huo umeshatangazwa katika Gazeti la Serikali Namba 66
la Ijumaa tarehe 24 Februari, 2012. Kuanzia kesho itatangazwa katika
magazeti ya kawaida. Katika mwaliko huo, wadau wanatakiwa kupendekeza
majina yasiyozidi matatu ya watu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika
kifungu cha 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sifa hizo ni hizi
zifuatazo:-
(a) Uzoefu katika
kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo
ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii.
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na
(c) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Aidha, nimeelekeza kuwa siku ya mwisho ya wadau kuwasilisha
mapendekezo yao ni tarehe 16 Machi, 2012. Wadau wanatakiwa kupitishia
mapendekezo yao kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Muungano au
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar. Nimewapa viongozi watendaji wakuu hao jukumu la
kupokea mapendekezo ya majina na kuyawasilisha kwangu. Baada ya hapo
nitashauriana na Rais wa Zanzibar kuteua Wajumbe wa Tume pamoja na
Mwenyekiti na Makamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba pia inatoa fursa kwa Rais kuteua Wajumbe wa
Tume kutoka hata nje ya orodha ya wadau. Ilionekana ni vyema kufanya
hivyo kwani wapo watu wengine wazuri ambao wanaweza kuwa hawamo katika
makundi yaliyotajwa na Sheria hii. Aidha, upo uwezekanao kwa
mapendekezo ya makundi kutozingatia baadhi ya mambo ya msingi kama vile
jinsia, jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kadhalika. Fursa hii aliyopewa Rais itasaidia katika
kuzingatia matakwa haya ya Sheria.
Pamoja na hayo napenda kuwahakikishia kuwa iwapo nitaitumia fursa
hiyo watu hao hawatakuwa wengi kuliko wale waliopendekezwa na makundi
yaliyotajwa katika kifungu cha 6 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwakumbusha wadau na wananchi kwa jumla kuwa Tume
ya Kuratibu na Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba ina Wajumbe 30 tu
wanaopatikana kwa idadi sawa kutoka sehemu zotu mbili za Muungano wetu
yaani 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar. Unapoongeza
Mwenyekiti na Makamu wake kwa jumla Tume itakuwa na wajumbe 32 yaani 16
kila upande. Hivyo basi, fursa ya kila aliyeleta majina kupata nafasi
katika Tume si kubwa.
Nayasema haya kutahadharisha juu ya ukweli huu ili tusijipe
matumaini makubwa mno na wala tusije tukashutumiana baada ya uteuzi.
Hata hivyo, pamoja na ugumu wa kuchagua miongoni mwa orodha ya watu
wengi wazuri, nitajitahidi tu Wajumbe wa Tume wawe watu makini,
wanaowakilisha sura pana ya jamii za nchi yetu na makundi yake muhimu na
utashi wa watu wa Tanzania yetu.
Tunapokwenda
Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu
kuwa zoezi la kuunda Tume litakamilika muda mfupi kadri inavyowezekana,
baada ya kupokea mapendekezo ya makundi. Kama nilivyokwishawahi
kudokeza siku za nyuma, napenda Tume ikamilike kuundwa katika robo ya
pili ya mwaka huu na kuanza kazi muda mfupi baada ya hapo.
Naomba nitumie nafasi hii kutoa wito maalum kwa wananchi wenzangu
kuanza kujiweka tayari kutoa maoni yao kwenye Tume. Mambo yataanza
miezi michache ijayo. Najua Tume itatengeneza utaratibu wa kuelimisha
wananchi kuhusu Katiba. Lakini nawaomba kila mtu binafsi yake aanze
kuchukua hatua za kuifahamu Katiba iliyopo sasa ili apate ufahamu wa
maudhui muhimu ya Katiba. Kufanya hivyo kutamuwezesha kuamua kwa
usahihi anataka kupendekeza nini kiwemo katika Katiba mpya. Nimeagiza
Mpiga Chapa wa Serikali kuhakikisha kuwa vitabu vya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania vinachapishwa kwa wingi ili wananchi waweze kuwa
navyo na kuvisoma. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Toa Maoni Yako:
0 comments: