*Afurahia wimbo wake kuingia katika tuzo za kili, Asema bado hajafikia malengo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

SANAA ya muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, inazidi kuchanja mbuga, huku majina ya wakali yakizidi kuchanua.

Vijana mbalimbali wa kike na wa kiume wanapata mafanikio makubwa, kitu kinachowafanya watikise anga ya muziki huo.

Miongoni mwa wasanii hao ni Mwanaisha Said, maarufu kwa jina la Dayna. Dayna kwa sasa macho yake yote yapo kwenye tuzo za Kili, anapowania tuzo hizo kwa mara ya kwanza.

Katika kuelekea kinyang’anyiro hicho, Dayna anayejiita pia ‘Mkali Wao’, ameingia katika kipengele cha Mwimbaji bora wa kike, wimbo bora wa mwaka wa zouk, rhumba na mtumbuizaji bora wa kike.

Huku akipewa namba A-4, D4, W3 kwenda kwa namba 15747 kwa vipengele hivyo, ambavyo vyote vinamuweka mwanadada huyo katika presha kubwa.

Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, fainali itafanyika Aprili 14, kutapofanyika sherehe za kukabidhi tuzo hizo kwa wasanii bora.

Akuzungumza jijini Dar es Salaam juzi, Dayna anasema kwa sasa ameshakamilisha albamu yake, ingawa bado haijaingia sokoni.

Albamu hiyo inaundwa na nyimbo mbalimbali, ukiwamo wimbo wake wa ‘Mafungu ya Nyanya’, ‘Fimbo ya Mapenzi’ na ‘Nivute Kwako’, ulioingia kwenye kinyang’anyiro cha wimbo bora wa zouk, rhumba.

Wimbo wake wa Nivute Kwako, ameimba sambamba na Barnabas, nyota wa Tanzania House of Talents (THT) na kuuweka juu zaidi.

Dayna anasema kuwika kisanaa ni kutokana na kipaji chake imara na mwenye malengo makubwa ya kuhakikisha kwamba anafanya vyema.

“Kila mtu alikuwa akiniambia kwamba mwenekano wangu ni wa kisanii, hivyo niingie humo kwa ajili ya maisha yangu.

“Mwanzo nilisita kidogo, ila baada ya kufikiria kwa muda, nikaona naweza hivyo nikafanya maamuzi sahihi na kuanza kufanya sanaa kwa malengo,” alisema.

Mafanikio yake yamesabishwa na watu wengi, akiwamo Marlaw, aliyeimba naye katika wimbo wa Mafungu ya Nyanya.

Walikutana mjini Morogoro na hatimae kuingia maakubaliano ya kushirikiana kwenye wimbo huo, waliorekodi Studio za MJ Records.

Anamshukuru msanii huyo kwa kukubali kuimba naye katika wimbo uliofanya vizuri katika ulimwengu wa muziki wa Bongo Fleva nchini.

Maisha yake katika sanaa yamekuwa ya kawaida sio ya mizunguuko kama wanavyofanya wengineo.

“Uwezo wangu ni mkubwa katika sanaa, ndio maana kwa miaka michache nimeweza kujiweka juu katika sanaa.

“Najua uwezo wangu huo ndio ulioniweka juu katika Bongo Fleva, kitu kinachonifariji ipo siku mambo yangu yatakuwa mazuri,” alisema.

Msanii huyo anaelezea hisia zake kwa mashabiki wake, juu ya kumpigia kura katika kichang’anyiro hicho cha tuzo za Kili.

Anasema kuingia kwenye shindano hilo ni kuonyesha umakini wake na utendaji uliotukuka, hivyo anaamini mashabiki hawatamuangusha.

“Naomba mashabiki wangu wanipigie kura ili nipate tuzo nilizotajwa kuwamo, ikiwamo ya msanii bora wa kike, mtumbuizaji bora na wimbo bora wa zouk, ambapo Nivute Kwako umewekwa.

“Sina cha kuwalipa zaidi ya kuwatakia kheri na Mungu atawalipia, ukizingatia kwamba ushirikiano wao kwangu ni mkubwa mno,” alisema Dayna.

Dayna aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita, anasema lengo lake ni kuwa msanii wa Kimataifa, kwa juhudi zake na kuhakikisha mambo yake yanakuwa mazuri.

Atahakikisha anatunga nyimbo nzuri, akifanya sanaa ya kweli, ili uwezo wake uwe juu katika sanaa ya Bongo Fleva.

Dayna anayevutiwa na mwanadada Stara Thomas, anasema kwamba anaangalia mbele ili afike malengo yake, licha ya kujua atakuta na na vikwazo vingi katika maisha yake ya muziki.

Dayna ni miongoni mwa wasanii nyota kwa sasa, huku anapokuwa jukwaani mashabiki kupata burudani kubwa kwa umahiri wake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: