MAELEZO YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WAKATI WA MKUTANO WAKE NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MGOGORO WA MASLAHI YA MADAKTARI ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA KARIMJEE, DAR ES SALAAM, TAREHE 29 JANUARI 2012
1.UTANGULIZI
1.UTANGULIZI
·Tangu mwishoni mwa mwezi Desemba 2011 kumekuwa na madai ambayo yalikuwa yakitolewa na Wataalam mbalimbali waliokuwa kwenye mazoezi kwa vitendo (interns) kwamba wangeitisha mgomo kwa sababu ya kucheleweshewa posho zao.
·Kama mnavyofahamu, baada ya hali hiyo kujitokeza, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ilifanya juhudi na kuwalipa wataalamu hao fedha walizokuwa wakidai ambazo ni kiasi cha Shilingi Milioni 876/-.
·Baada ya malipo hayo kufanyika tarehe 5 Januari 2012, Mgogoro ukahama kutoka kwa interns na kuwahusisha watalaam wa Kada nyingine za Afya wakiwemo Madaktari.
2.HATUA ZA AWALI ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI
·Ijumaa jioni tarehe 20 Januari 2012, ujumbe wa watu sita ulifika ofisini kwangu ukitaka kuonana na Waziri Mkuu. Hata hivyo, kwa kuwa nilikuwa tayari na ratiba ya kwenda Arusha, nilimwelekeza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu akae na Naibu Waziri wa Afya na kuwasikiliza halafu nikawataka wanijulishe wakati nikiwa Arusha.
·Katika mazungumzo haya, ambayo yaliongozwa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dkt. Namala Mkopi, walifikia maelewano ya kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuendelea na majadiliano ya madai yao.
·Jumamosi tarehe 21 Januari 2012, Ujumbe huo ulikwenda Wizara ya Afya na kujadiliana na Uongozi wa Wizara ambapo madai yote yalipitiwa na wakafikia muafaka wa utaratibu wa kuyafanyia kazi. Hata hivyo, waliporejesha kwa wenzao matokeo ya majadiliano na Wizara ya Afya, yalifanyika mapinduzi ya Uongozi na ikaundwa Kamati ya Mpito ya kushughulikia madai ya Madaktari ikiongozwa na Dkt. Stephen Ulimboka.
·Nilipotoka Arusha tarehe 23 Januari 2012, nilipokea maombi yao ya kuonana nami na wakapangiwa tarehe 24 Januari 2012, saa 11 jioni, lakini hawakutokea. Namba za simu walizoacha kwa Katibu Mkuu zilikuwa ni za watu waliokwishapinduliwa na hawakuwa tayari kuja tena ofisini.
·Nilipoongea na Wahariri wa Vyombo vya Habari, mnamo Januari 25, 2012 nilitumia fursa hiyo kuwaomba waje tuonane ili niwasikilize na tuainishe njia ya kutafuta ufumbuzi wa madai yao.
·Pamoja na jitihada zote hizo, hakuna aliyekuwa tayari kufuata ushauri nilioutoa. Kwa hiyo, si kweli kwamba Serikali imetoa taarifa ya muda mfupi ya kutaka kukutana nao kama walivyodai na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari.
3.UJUMBE WA SERIKALI
·Wakati wakiendelea na Vikao vyao, nilikutana na Mawaziri kadhaa pamoja na Viongozi wa TUGHE wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Ramadhani Kiwenge na tukakubaliana tutume Ujumbe wa Serikali ili uende kuwasikiliza. Kwa nia njema ya kuendeleza jitihada za kutaka kuonana na madaktari hao, nilituma Uongozi wa Serikali ukiongozwa na Mawaziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma uende kuonana na Madaktari hao kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Starlight tarehe 27 Januari 2012.
·Kwenye Mkutano huo Madaktari waliwasilisha malalamiko yao na kuomba kuonana na mimi. Katibu wa Waziri Mkuu alipowapigia simu jana asubuhi mara kadhaa ambazo hazikupokelewa na ikabidi aende hadi walipokuwa katika Hoteli ya Starlight, kuwafikishia Ujumbe wa mimi kukutana nao. Katika majadiliano yao walikataa mwaliko kwa njia ya mdomo na wakataka waandikiwe barua rasmi. Kufuatia maombi hayo, Katibu wangu aliwaandikia barua ya kuwataka tuonane leo tarehe 29 Januari 2012 saa 4:00 asubuhi kwenye Ukumbi wa Karimjee.
·Walipopigiwa simu waje kuichukua barua yao Ofisini kwangu kama walivyokubaliana na Katibu wangu pale Starlight Hotel, walikataa kuja na badala yake wakataka wapelekewe hadi Magomeni kwenye Ofisi za Mkuu wa Wilaya nasi tukaipeleka kwa Dispatch ili wasaini kuwa wameipokea.
·Jana saa 3:00 usiku, walileta barua yao ya kukiri kupata barua yangu na kutoa masharti yafuatayo:
(a)Hawako tayari kukutana na mimi hadi kesho tarehe 30 Januari ili kusubiri wenzai wa mikoani waweze kuhudhuria mkutano huu.
(b)Ofisi ya Waziri Mkuu iwajibu kwanza kwa maandishi madai yao kabla ya kukutana nao ili wapate nafasi ya kujadili hoja moja baada ya nyingine.
(c)Wakati wakija kuongea na mimi, wanataka Serikali itoe tamko kwamba hakutakuwa na adhabu ya aina yoyote ile kwa daktari au mtumishi wa kada yoyote ya afya itakayotokana na mgomo/mgogoro huu.
4.MADAI YAO
·Kulikuwa na mawasiliano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Uongozi wa Medical Association of Tanzania (MAT) na baadaye Mwenyekiti wa muda wa Kamati ya Mapato ya Madaktari kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea.
·Katika barua yao ya tarehe 27 Januari 2012, walitoa madai nane yalijuimuisha vipengele vifuatavyo:
(a)Posho ya Kulala Kazini (on Call Allowance)
Kwa sasa Madaktari wanalipwa Posho Shilingi 10,000/= (Elfu Kumi) kwa siku. Wanapendekeza Posho hiyo ilipwe kwa Kiwango cha Asilimia 10 ya Mshahara wa mwezi.
(b)Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Hatarishi (Risk Allowance)
Inapendekezwa Madaktari walipwe Posho ya kufanya kazi katika Mazingira Hatarishi ya Asilimia 30 ya Mshahara wa mwezi.
(c)Posho ya Nyumba
Madaktari wanapendekeza wapewe Nyumba na pale inaposhindikana wapewe Posho ya Asilimia 30 ya Mshahara wa mwezi.
(d)Posho ya Kufanya Kazi katika Mazingira Magumu (Hardship Allowance)
Madaktari wanaofanya Kazi katika Mazingira Magumu walipwe Posho ya Asilimia 40 ya Mshahara wa mwezi.
(e)Kupatiwa posho ya usafiri
Madaktari walipwe Posho ya Asilimia 10 ya Mshahara na iwapo inatashindikana, Madaktari wakopeshwe Magari.
(f)Nyongeza ya Mshahara
Wanadai mshahara wa Shilingi 700,000/= kwa Daktari anayeanza kazi ni mdogo sana, hivyo wanapendekeza Daktari anayeanza kazi alipwe Shilingi 3,500,000/= kwa mwezi.
(g)Kupatiwa Bima ya Afya
Inapendkezwa Madaktari pamoja na familia zao wapewe kadi za kijani za Bima ya Afya.
(h)Kutaka wenzao warudishwe Muhimbili
Dai hili linahusu Madaktari waliokuwa katika mafunzo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na baadaye kurudishwa Wizarani, warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote.
·Serikali imeyafanyia uchambuzi madai yao na kuyaainisha kama ifuatavyo:
ULINGANISHO WA MISHAHARA:
·Wanadai Mshahara wa Shilingi 700,000/= kwa Daktari anayeanza kazi ni mdogo sana, hivyo wanapendekeza Daktari anayeanza kazi alipwe Shilingi 3,500,000/= kwa mwezi. Hata hivyo, Mshahara wa Daktari anayeanza kazi kwa sasa ni Shilingi 957,700/= kwa mwezi, na siyo Shilingi 700,000/= kwa mwezi kama wanavyodai.
·Wanapendekeza kwamba Madaktari wanaoajiriwa hivi sasa walipwe mshahara wa Shilingi Milioni 3.5/-. Katika ajira ya seriikali, madaktari wapya wanaoajiriwa wanalipwa sh. 957,700/- wakati watumishi wa kada nyingine kama vile Wahandisi wanaanza ajira na sh. 600,000/=, Wahasibu wanaanza na mshahara wa kati ya sh. 300,000 hadi 400,000/-.
ATHARI ZAKE KWA BAJETI YA SERIKALI
·Posho zote wanazodai madaktari zikijumlishwa zinafikia asilimia 120 ya mshahara wa Daktari mmoja.
·Ili kuhakikisha kunakuwa na hali ya utulivu katika mazingira ya kazi utekelezaji wa pendekezo la Madaktari la kulipa mshahara wa sh. 3,500,000/= kwa mwezi kwa Daktari atakayeanza kazi, utailazimu Serikali kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa Kada za Afya pamoja na Kanda nyingine ili kuweka uwiano kufuatana na Stahiki za Miundo katika Utumishi wa Umma (Scheme of Service).
·Kwa mujibu wa mapendekezo yao ina maana kwamba kiwango cha kuanzia mshahara kwa Mhudumu wa Afya kitakuwa sh. 670,316/= na mshahara wa juu kwa kada za Afya utakuwa sh. 8,145,573/= kwa mwezi. Utekelezaji wa pendekezo hili utagharimu jumla ya sh. 83,508,834,430/= kwa mwezi ambayo ni sawa na sh. 417,544,172,150/= kwa kipindi kilichobaki cha miezi 5. Kiasi hiki ni sawa na nyongeza ya sh. 301,730,372,400/= katika bajeti ya mshahara kwa mwaka 2011/12.
·Kwa mujibu wa mapendekezo ya Madaktari ya mshahara pamoja na posho mbalimbali, itamaanisha Daktari anayeanza kazi atapata jumla ya Shilingi 7,700,000/= kwa mwezi ikijumuisha Mshahara na Posho nyingine. Aidha, kwa mujibu wa mapendekezo hayo Daktari Mshauri Mwandamizi atapata sh.17,231,020/= kwa mwezi. Kwa kuzingatia ukubwa wa gharama hizi utekelezaji wa mapendekezo ya Madaktari utakuwa hauwezekani kwa kuzingatia hali halisi ya Bajeti ya Serikali.
·Kiasi hiki ni sawa na nyongeza ya sh. 301,730,372,400/- katika bajeti ya mshahara kwa mwaka 2011/2012.
·Endapo Serikali itatekeleza madai yao kwa mwaka mmoja, jumla ya mishahara yao itakuwa ni sh. 799,692,615,592.98 badala ya sh. 222,214,936,800.00 za sasa hadi kufikia Juni 2012.
·Madaktari hao wanadai kwamba watumishi wa kada nyingine za afya wapandishiwe mishahara na posho kama zao. Endapo nao watapewa fedha wanazodai, Serikali itapaswa kulipa sh. 202,413,397,568.00. Na kama madai yao yatatimizwa kwa miezi mitano iliyobakia, watapaswa kulipwa sh. 84,338,915,653.00.
·Katika makundi haya mawili tu, nyongeza yao ya mishahara ni sawa na sh. 1,002,106,013,160 kwa mwaka. Ukijumlisha na nyongeza ya posho zao wanayodai ya sh. 1,037,184,854,550.00 unapata sh. 2,039,290,867,710/- ambayo ni sawa na THELUTHI MBILI YA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI WOTE SERIKALINI ambayo kwa sasa ni sh. Trilioni 3.45/-.
·Hii maana yake ni kwamba kiasi kinachobaki cha theluthi moja ndicho kigawanywe kwa watumishi wengine.
HALI ILIVYO KATIKA HOSPITALI NYINGINE
Tangu mgomo uanze, Serikali imekuwa ikifuatilia na kupokea taarifa za mgomo huu kutoka Mikoa yote. Mpaka tarehe 28 Januari 2012, Mikoa 21 ilikuwa imewasilisha taarifa za awali juu ya hali ya mgomo huo. Ufuatao ni muhtasari wa Taarifa hizo zilizo katika makundi makuu mawili zikionyesha hali ya mgomo Mikoani na Wilayani.
Mikoa Ambayo Haina Kabisa Mgomo:
Kundi la kwanza ni lile ambalo katika Hospitali zake zote za Mikoa na za Wilaya hazina mgomo kabisa. Mikoa hiyo ni:
1.Ruvuma
2.Lindi
3.Mtwara
4.Shinyanga
5.Arusha
6.Tabora
7.Kagera
8.Iringa
9.Mara
10.Pwani
11.Kigoma
12.Singida
13.Manyara; na
14.Rukwa.
MIKOA AMBAYO INA MGOMO:
Kundi hili la pili linajumuisha Mikoa ambayo imekumbwa na mgomo. Chini ya kundi hili, baadhi ya Hospitali za Mikoa zimekuwa katika mgomo huku Wilaya zote za Mikoa hiyo ikiwa haina mgomo na kuendelea na kazi kama kawaida. Mikoa hiyo na hali halisi za mgomo ni kama ifuatavyo:
1.Kilimanjaro:
Kuna mgomo katika Hospitali ya KCMC ambao unahusisha Madaktari waliopo katika mafunzo kwa vitendo. Hata hivyo, katika Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi pamoja na Hospitali zote za Wilaya hakuna mgomo.
2.Mbeya:
Kuna mgomo wa Madaktari waliopo katika mafunzo ya vitendo wapatao 65 na Madaktari waliosajiliwa (Registered Doctors) 10 na Madaktari Bingwa 10 ambao mgomo wao ni wa chinichini na hauko wazi. Hakuna mgomo katika Hospitali zote za Wilaya.
3.Mwanza:
Hakuna mgomo wa wazi. Japokuwa Madaktari 46 wa Hospitali ya Bugando walitoa tangazo kwa maandishi la kushiriki mgomo. Dalili za mgomo huo zinaonekana kwa Madaktari waliopo katika mafunzo kwa vitendo. Hakuna mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure na Hospitali zote za Wilaya.
4.Morogoro:
Kuna mgomo katika Hospitali ya Mkoa. Hata hivyo, tarehe 28 Januari 2012 Mkuu wa Mkoa alikutana na Madaktari hao kusikiliza matatizo yao. Hakuna mgomo katika Hospitali zote za Wilaya.
5.Tanga:
Kuna mgomo wa chinichini katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo ambao unahusisha Watumishi wa kada zote katika Sekta ya Afya. Hata hivyo, hakuna mgomo katika Hospitali zote za Wilaya.
6.Dodoma:
Kuna mgomo katika Hospitali ya Mkoa. Huduma za dharura tu ndizo zinazotolewa baada ya kufanyika vikao na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali, Balozi Job. Lusinde. Hata hivyo, hakuna mgomo katika Hospitali zote za Wilaya.
7.Dar es Salaam:
Dar es Salaam mgomo upo na ndipo ulipoanzia.
MAELEZO KUHUSU DKT. STEPHEN ULIMBOKA
·Dkt. Ulimboka Stephen alihitimu Shahada ya Udaktari (MD) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004, alipata usajili wa muda (Provisional Registartion No. 2022) wa Baraza la Madaktari mwaka huo huo na kupangiwa Internship katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
·Mwezi Novemba 2005 aliongoza mgomo wa Madaktari Nchini na usajili wake ulisitishwa na Baraza la Madaktari. Alishtakiwa mbele ya Baraza hilo kwa ukiukwaji wa maadili ya Taaluma ya Udaktari kwa kuitisha na kufanya mgomo ambayo ni makosa ya kimaadili katika taaluma hiyo. Alikataa kufika mbele ya Baraza kujibu tuhuma zilizokuwa zinamkabili na hivyo, shauri lake halikumalizika.
·Mwezi Julai, 2006, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimsamehe, na hivyo kurejeshewa usajili na Baraza na kuruhusiwa kuendelea na Internship.
·Katika kumpa taarifa za msamaha wa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la Madaktari kwa nyakati tofauti walimtaka Dkt. Ulimboka kutojihusisha na mgomo au suala lolote ambalo ni kinyume na maadili ya Taaluma ya Udaktari. Naye kwa barua yake kwa Baraza ya tarehe 2 Februari 2007 alikiri kwamba hatajihusisha wala kutoa ushawishi wowote kwa wengine kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya Udaktari. Barua hii tunayo.
·Hadi sasa hakuna taarifa kama alimaliza Internship kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi hayo na hakuna taarifa juu ya mahali anapofanyia kazi. Aidha, Dkt. Ulimboka siyo Mtumishi wa Serikali na wala hajasajiliwa kama Daktari.
UAMUZI WA SERIKALI
·Katika hatua iliyofikiwa, Serikali imetambua kwamba Madaktari wanaongozwa na Kamati ya Mpito, hawataki suluhu licha ya juhudi zote ambazo zimefanywa za kuwaita ili kushughulikia madai yao.
·Kuanzia sasa, Serikali inawahimiza Madaktari wote walio katika mgomo kuacha mara na kuripoti kazini ifikapo kesho asubuhi, Jumatatu tarehe 30 Januari, 2012.
·Watakaoshindwa kufanya hivyo, watakuwa wamepoteza Ajira zao.
·Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hii kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na JKT kupeleka madaktari wake katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini. Kwa hiyo, huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida.
·Aidha, Serikali inatoa pongezi kwa TUGHE kwa kuwa wametambua hoja za Madaktari lakini wakasema njia zilizotumika na Madaktari hao kuwasilisha madai yao na kugoma si sahihi.
·Serikali inasisitiza kuwa mgomo wao siyo halali kwa sababu haukufuatwa taratibu za kuitisha mgomo. Wao walipaswa kutangaza mgogoro na kisha kutoa notisi ya siku 60, jambo ambalo wao hawakulifanya.
·Katika muda huo wa notisi wa siku 60, majadiliano yalitakiwa yawe yanaendelea ili kushughulikia madai yao.
·Vilevile, Serikali inatoa pongezi kwa Madaktari na Wauguzi wote ambao walikuwa kazini wakiendelea kutoa huduma kwa Wagonjwa na kwa kutambua hali ilivyo, walikutana na kuwasihi Madaktari wenzao waache mgomo na kurejea kazini.
Toa Maoni Yako:
0 comments: