Mkakati mpya uliobuniwa wa kuwahusisha viongozi wa  jadi kwenye kijamii katika  kupiga vita  mila na desturi zinazochangia ukatili wa kijinsia  unaoeneza  maambukizi vya virusi vya UKIMWI (VVU)  barani Afrika  umeanza kuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza maambukizi mapya.

Mpango  huo ulianza kufanyiwa majaribio nchini Zimbabwe mwaka 2005  na  baada ya mafanikio yake kuonekana ulisambazwa katika nchi nyingine sita za kusini mwa Afrika ambazo ni Botswana, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Msumbiji na umeweza  kuepusha  vitendo vya ukatili vinavyosababisha maambukizi ya VVU.

Mkakati huo uliobuniwa na shirkika la Kiraia  la  SAfAIDS  na unatambua viongozi wa kijadi kwenye jamii kuwa ni wale walioko miongoni mwa  makundi kama vile ya  wazee, vijana wa kike na wa kiume, wakunga wa jadi, waganga wa jadi na wajane.

Afisa  masuala ya kitaalamu  wa SAfAAIDS Rouzeh Eghtessedi  amewaambia washiriki wa mkutano wa 16  kuhusu UKIMWI na magonjwa  yanayoambukizwa kwa  kujamiana  barani Afrika (ICASA) unaoendelea Addis, Ababa, Ethiopia kuwa  mpango huo umefanikiwa kuwajengea uwezo viongozi wa kijamii  na jamii yenyewe  kupiga vita mila na vitendo vinavyochangia maambukizi ya VVU.   

Akielezea mpango huo unavyotekelezwa Mkurugenzi Mtendaji wa SAfAIDS   SAfAAIDS Lois Chingandu  amesema  katika hatua ya awali utafiti hufanyika ili kutambua mila na desturi na  vitendo vya ukatili vilivyopo katika jamii husika ambavyo vinasababisha maambukizi ya VVU.

Amesema baada ya utafiti nyenzo za kampeni na mafunzo hutengenezwa kutokana na  taarifa zilizopatikana kutokana na utafiti huo kwa lengo la kuweza kugusa makundi yote kwenye jamii  ili yachukue hatua sahihi kuleta mabadiliko chanya katika kutokomeza  ukatili, magonjwa ya kujamiiana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.

Chingandu   amekaririwa na mwandishi wa TAMWA akisema kuwa   maswali yanayoulizwa kwenye utafiti huo wa awali  hulenga kuwezesha walengwa katika makundi mbalimbali kwenye jamii kuzungumza kwa uhuru kabisa kuhusiana na  mambo  ya mila na desturi katika jamii yao. 

Amesema kwa mfano  kama jamii ina tatizo  la wanandoa  kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa maswali ya utafiti yanaulizwa  kwa namna ambayo wanandoa  wanaeleza chanzo cha tatizo hilo ili  shughuli za kampeni ziandaliwe kwa namna ambavyo  wahusika wataguswa na kubadilika.

Kwa mujibu wa Chingandu viongozi wa kijamii ndio huwa wa kwanza kupatiwa mafunzo kuhusu njia mbalimbali za maambukizi ya UKIMWI na  umuhimu wa uongozi wao  katika mapambano ya kuepusha maambuziki mapya.

Alisema viongozi hao wakishaelimika na kuhamasika wao wenyewe huwa chachu ya kuleta mabadiliko  katika jamii zao.

“Baada ya miaka mitatu ya kampeni kabambe mabadiliko huonekana katika jamii” alisema  kiongozi huyo wa SAfAIDS  na kuongeza kuwa  kinachofuatia ni kupima mafanikio na kwamba maswali yaliyoulizwa wakati wa utafiti wa awali ndiyo hutumika kufanya tathmini ili  kuweza kuona ni kwa kiasi gani jamii imebadilika.

Alisema kwa mfano mpango huo  umeweza kuleta  mabadiliko katika  makabila kadhaa nchini Zimbabwe  ambapo  mwanaume akifiwa  na mke jamii ilikuwa inampatia binti  mdogo awe  mke wake mpya bila hata kupima virusi jambo ambalo lilichangia ongezeko kubwa la maambukizi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: