KUNDI la vijana leo limevamia ofisi ya umoja wa mataifa ziliopo mtaa wa Gulioni mjini hapa wakiutaka umoja wa mataifa kutekeleza madai yao ya kutambuliwa kwa taifa la Zanzibar kuwa dola kamili.Kiongozi wa kundi hilo la vijana wapatao mia moja Rashid Salum Adiy alifanikiwa kuwasilisha nakala ya maombi yao kutoka kwa afisa mtendaji mkuu wa ofisi za umoja wa mataifa ziliopo Zanzibar Soro Karna.

Karna alikiri kupokea barua hiyo ambayo alisema ni nakala inayokwenda kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa bwana Ban Ki Moon.

‘Ni kweli nimepokea barua ambayo ni nakala inayokwenda kwa katibu mkuu wa umoja wa Mataifa ambayo ni madai ya siku nyingi ya kundi hilo linalotaka Zanzibar kuwa taifa huru na kujiondowa katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’alisema Karna.

Kwa hivyo alisema madai hayo yeye hana uwezo na mamlaka ya kuyatoleya uamuzi kwa sababu barua hiyo imekusudiwa kwa katibu mkuu ambaye ofisi zake zipo umoja wa mataifa New York Marekani.

Kundi hilo limegoma kuondoka katika maeneo ya ofisi za umoja wa mataifa na kusema watakaa hapo hata kwa wiki nzima hadi wapatiwe majibu kamili kuhusu maombi yao.

‘Hatuondoki hapa….tutakaa hapa hadi tupatiwe majibu yetu kutoka kwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa’alisema Rashid.

Rashid alisema uamuzi wao huo unatokana na maombi ya siku nyingi kuhusu shauri lao la kutaka Zanzibar kuwa taifa kamili linalojitegemea na kujiondowa katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema madai yao hayo sasa wanataka majibu kamili kutoka kwa taasisi hiyo ambayo majukumu yake makubwa ikiwemo kusimamia mataifa mbali mbali wanachama wa umoja huo,baada ya kufunguwa kesi.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa mjini magharibi Mkadam Mselem alifika katika eneo hilo na kufanya mazungumzo na afisa mkuu wa ofisi za umoja wa mataifa ziliopo Zanzibar.

‘Tunafanya mazungumzo naye kuweza kujuwa madai hayo na hatua zitakazochukuliwa na vipi kama wanaweza kuwepo hapa ikiwemo usalama wao’alisema Mkadam.

Hata hivyo afisa mkuu wa umoja wa mataifa alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa vijana hao katika ofisi hizo alisema jengo ziliopo ofisi za umoja huo ni mali ya shirika la taifa la biashara (ZSTC).

‘Hili jengo sio mali ya umoja wa mataifa…..kwa hivyo hao watu hawapo katika mikono salama ya umoja wa mataifa’alisema.

Alisema katika jengo hilo zipo ofisi mbali mbali taasisi za fedha na benki ya Barclays ambapo usalama mkubwa unahitajika.

Karna aliwashauri vijana hao kuondoka na kusubiri shauri lao likipatiwa majibu sahihi kutoka kwa ofisi za umoja wa mataifa ziliopo New York.

Zanzibar ibaki ndani ya muungano ?

Hapana (88%, 1.058 Votes)
Ndio (12%, 148 Votes)

Total Voters: 1.206

Habari hii kwa hisani ya Khatib Suleiman
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: