JUMLA ya makandarasi 7 waliofanikiwa kupita katika mchakato wa awali wa kumpata mkandarasi atakayeshinda zabuni ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni jana wamefanya ziara ya ukaguzi katika eneo linapotakiwa kujengwa daraja hilo.

Mtaalam Mshauri kutoka Kampuni ya Arab Consulting Engineers (ACE) Mhandisi Mohamed Shaeb, aliongoza ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kuwapatia maeleza ya kitaalam Wakandarasi hao kuhusu maudhui ya mradi husika na changamoto zake kabla ya hawajawasilisha makisio yao kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Awali kabla ya mchakato huu walikwisha jitokeza jumla ya wakandarasi 16 ambao baada ya kuchambuliwa ndipo kati yao wakapatikata hao 7 ambao wanashindanishwa.

Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi wanaendelea na mchakato wa kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni ambalo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwanzoni mwa mwaka 2012.

Daraja hilo ambalo ni la kisasa zaidi kujengwa hapa nchini ambapo litakuwa na barabara tatu kila upande yaani kuwa na uwezo wa kuruhusu magari sita kupita kwa wakati mmoja.

Daraja la Kigamboni linatarajiwa kuwa na urefu wa mita 600 na pindi litakapokamilika litakuwa ni kiungo muhimu kati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni na pia litachangia katika jitihada za kupunguza msongamano wa magari hapa jijini.

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mnamo mwezi Machi mwaka huu wa 2011 ililiagiza Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni unaimarishwa na hivyo kuondoa kero na adha nyingi wanazozipata kwa sasa.

Agizo hilo lilitolewa wakati wa ziara aliyoifanya Waziri Magufuli alipotembelea eneo la Kurasini Vijibweni, ambako daraja hilo litajengwa.

Waziri Magufuli alichukua hatua hiyo kutokana na mazungumzo kuhusu ujenzi wa daraja hili kuwa yamechukua muda mrefu bila ya hatua madhubuti kuonekana.

Ujenzi wa daraja hili utachangiwa kwa asilimia 60 na NSSF wakati ambapo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itachangia asilimia 40 zilizobakia.

NSSF tayari imekwishatenga kiasi cha Shilingi bilioni 100 hadi sasa kwa ajili ya mradi huu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: