Serikali imesema wananchi watapata fursa ya kujadili kuwepo au kufutwa kwa adhabu ya kifo katika sheria za Tanzania wakati wa kutoa maoni juu ya Katiba mpya.

Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani (pichani) aliyasema hayo katika hotuba aliyoitoa jana jijini Rome, Italia katika Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Mawaziri wa Sheria.

“Kama mnavyofahamu, Tanzania imeanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Kwa kuzingatia kuwa Haki ya Kuishi ipo katika Katiba, kuna uwezekanao wananchi wakapata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu adhabu ya kifo,” alisema.

Pamoja na kuwa Haki ya Kuishi ipo katika Katiba, Waziri Kombani alifafanua, Katiba hiyohiyo pia haipingi sheria sheria zilizopo ikiwemo ile inayotoa adhabu ya kifo kwa makosa makubwa kama ya mauaji na uhaini.

“Naomba niseme pia Katiba hiyohiyo inayotoa haki hizo, ikiwemo haki ya kuishi, haizuii sheria yeyote wala kutungwa kwa sheria yeyote kwa lengo la kuhakikisha haki za watu au maslahi ya taifa yanahujumiwa,” alisema na kuongeza:

“Ni kutokana na sababu hizi, sheria zetu zinatoa adhabu ya kifo kwa makosa ya mauaji na uhaini,” alifafanua katika mkutano huo wa siku mbili uliomalizika jana.

Waziri Kombani aliwaambia wajumbe wa Mkutano huo kuwa, nchini Tanzania adhabu ya kifo hutolewa na Mahakama Kuu tu na msaada wa kisheria hutolewa kwa watuhumiwa wote wanakabiliwa na mashtaka ambayo adhabu yake ni kifo.

“Mtu anayehukumiwa kifo na Mahakama Kuu ana haki ya moja kwa moja ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo chombo cha mwisho Tanzania” alisema na kufafanua kuwa adhabu hiyo inapotolewa na kuthibitishwa na Mahakama ya Rufani, kuna Kamati ya Ushauri ambayo humshauri Rais kabla ya utekelezaji.

“Mfumo huu, kwa kiasi kikubwa, unatoa ulinzi dhidi ya utekelezaji usiofaa wa hukumu hiyo,” alifafanua.

Pamoja na kuwepo kwa adhabu hiyo, Waziri huyo alisema, kwa miaka 16 iliyopita Tanzania haijatekeleza hukumu hiyo: “Kwa maneno mengine, utekelezaji wa hukumu hiyo ulifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 1994. Uamuzi huu unafanywa kwa utashi wa Rais,” alisema.

Katika mkutano huo, Waziri Kombani pia aliishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa juhudi zake za kuhakisha adhabu ya kifo inafutwa na kusema kuwa Tanzania inaamini katika kuwashirikisha wananchi kabla ya kufikia uamuzi wa kuifuta.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: