WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka waajiri mbalimbali nchini kutoa ruhusa kwa watumishi waliowaajiri ili waweze kujiendeleza kielimu kwa kutumia njia ya elimu masafa.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Septemba 9, 2011) wakati akizindua kituo cha Mkoa wa Rukwa cha Chuo Kikuu Huria eneo la Eden mjini Sumbawanga.
Amesema kuna baadhi ya waajiri wanawanyima ruhusa ya kusoma watumishi walio chini kwa kuhofia kwamba watakapomaliza masomo watakuja kuchukua nafasi zao za uongozi.
“Kuna baadhi ya viongozi wana tabia ya kuzuia wenzao wasijiendeleze kwa kuhofia kuwa nafasi zao zitachukuliwa pindi wanapohitimu... wawaache wenzao wakasome. Na ikithibitika hao waliosoma wana uwezo mkubwa wa utendaji kazi, sisi hatutaacha kuwateua,” alisisitiza.
Alisema asilimia kubwa ya waajiri ni Halmashauri na akaonya kwamba kama viongozi wa Halmashauri hawatawaruhusu watumishi wakajiendeleza, utafika wakati watajikuta wanawaongoza watu wasio na sifa au waliosoma miaka ya 47.
“Ninawasihi waajiri mbadilike, muwaruhusu watumishi wenu wakasome na muwape fursa za kujiandaa kwa mitihani,” aliongeza.
Alisisitiza haja ya wanawake kujiunga zaidi na Chuo Kikuu Huria kwa sababu hadi udahili wao uko chini sana. “Kwa mwaka 2007/2008, wanawake waliodahiliwa na Chuo Kikuu Huria ni asilimia 23 tu ya wanafunzi 19,909 wakati mwaka 2010/2011 idadi ya wanawake ilikuwa asilimia 30 ya wananfunzi 44,272,” alisema.
“Nawasihi akinamama wachague elimu inayotolewa na vyuo vikuu kwa njia ya masafa kwa sababu inamwezesha mwanamke kupata elimu wakati akiendelea na majukumu yake kwa familia na Taifa,” alisisitiza.
“Nafahamu majukumu mengi na makubwa waliyonayo wanawake kwenye jamii. Hata hivyo, hatuna budi kuwahimiza kuongeza viwango vyao vya elimu, kwani tunatambua kuwa ukimwelimisha mwanamke umelielimisha Taifa,” alisema.
Kesho asubuhi, (Jumamosi, Septemba 10, 2011) Waziri Mkuu atakwenda wilayani Mpanda ambako pia atazindua tawi la Chuo Kikuu Huria Mpanda, kisha atazindua tawi la Benki ya CRDB Mpanda. Mchana huo huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: