Na Pardon Mbwate, wa Jeshi la Polisi Kigoma

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linawashikiria watu wawili mmoja Raia wa Rwanda na mwingine Raia wa Burundi wakiwa na silaha moja aina ya SMG na risasi 55 wakiwa katika maeneo tofauti ya wilaya ya Kibondo mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma ACP Fraisser Kashai, amewataja watuhumiwa huo kuwa ni Samson Emmanuel(36) raia wa Rwanda aliyekuwa na silaha aina ya SMG yenye namba 0382 huko kwenye kijiji cha Busunzu na mwingine ni Bizimana Belikimasi(20) raia wa Burundi aliyekuwa na risasi 55 za SMG akiwa katika kijiji cha Nyagwigima tarafa ya Mabamba wilayani humo.

Kamanda Kashai amesema kuwa watuhumiwa huo walikamatwa jana usiku kwa muda tofauti tofauti ambapo Emmanuel raia wa Rwanda alikamatwa majira ya saa 5.30 usiku akiwa na silaha hiyo huko kwenye Kijiji cha Busunzu na Belikimasi raia wa Burundi yeye alikatwa majira ya saa 1.00 usiku akiwa na risasi hizo 55 katika kijiji cha Nyabisinda.

Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa wote hao walikamatwa wakiwa katika harakati za kutaka kufanya uhalifu katika maeneo hayo ingawa aliyekamatwa na silaha hakuwa na risasi na aliyekamatwa na risasi hakuwa na silaha na kila mmoja akiwa katika eneo tofauti mbali na mwingine.

Kamanda Kashai amesema kuwa bado Polisi wanagonganisha vichwa kuona kama watuhumiwa hao wana uhusiano ama kila mmoja alikuwa na kundi lake la kihalifu. Amesema kuna uwezekano mkubwa kuwa aliyekamatwa na silaha alikuwa na watu wengine waliobeba risasi na na kwa aliyekamatwa na risasi kulikuwa na watu wengine waliokuwa na silaha.

Amesema wakati Polisi wakiendelea na Operesheni na Upelelezi wa matukio hayo mawili, lakini pia inawatafuta watu wengine kutoka katika makundi ya kila mmoja ili kuweza kupata silaha zaidi pamoja na risasi ambazo bado zipo katika mikono hatari ya majambazi kutoka nchi mbili za jirani.

Kamanda Kashai amesema kuwa kupatikana kwa silaha pamoja na risasi hizo, kunatokana na taarifa za siri zilizotolewa na Raia wema kuwa katika maeneo hayo tofauti kulikuwa na watu wasiofahamika katika maeneo ya vijiji hivyo hali ambayo iliwapa mashaka wakazi wa vijiji hivyo.

Katika tukio lingine wananchi wa kijiji cha Mole mkoani Kigoma waligundua maiti ya mtoto mdogo wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kumi ambaye hakufahamika jina ama mahala alikotoka. Maiti hiyo ilionekana ikiwa inaelea pembezoni mwa Ziwa Tanganyika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: