Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Wilson Mukama kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza, Ndugu Bhikhu Karia.

Katika salamu alizomtumia Mheshimiwa Mukama, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM amesema kuwa amestushwa na kuhuzunishwa na kifo cha ghafla cha Ndugu Karia ambaye alifariki usiku wa kuamkia Alhamisi ya wiki hii katika Hospitali ya Regency, mjini Dar es Salaam kwa matatizo ya figo. Alikuwa na umri wa miaka 61.

Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa kifo cha Ndugu Karia kimekipora Chama cha Mapinduzi kada hodari na mwenye bidii ambaye alitumia maarifa yake na vipaji vyake vingi katika kukitumikia, kukinadi na kukitetea Chama hicho.

Mheshimiwa Kikwete amesema katika salamu zake hizo: “ Nimepokea kwa mshituko na huzuni nyingi habari za kifo cha kada mwenzetu, ndugu Bhikhu Karia. Kwa hakika Chama chetu kimempoteza kada hodari na mwenye bidii ambaye alitumia maarifa yake na vipaji vyake vingi kukitumikia, kukinadi na kukitetea Chama cha Mapinduzi.”

Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ameongeza kuwa ni jambo la kusikitisha zaidi kuwa CCM imempoteza Ndugu Karia wakati ambako uwezo wake, ari yake na bidii yake vilikuwa vinahitajiwa zaidi na chama chake katika Wilaya ya Ukerewe.

“Nachukua nafasi hii, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Chama Chetu, kukutumia wewe salamu zangu wa rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa. Napenda pia kupitia kwako uniwasilishie salamu zangu za dhati kabisa za rambirambi kwa familia yote ya Ndugu Karia, wana-CCM wa Ukerewe na Mkoa wa Mwanza, “ amesema Mheshimiwa Kikwete na kuongeza:

“ Napenda kuwahakikishia kuwa moyo wangu uko pamoja nao katika msiba huu. Msiba wao ni msiba wangu. Naelewa machungu yao na nawaombea Mwenyeji Mungu awape uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha majonzi kwa sababu yote ni mapenzi yake.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: