Wakati viongozi wakuu wa nchi na serikali wakitarajiwa kukutana kwa siku tatu hapa Umoja wa Mataifa kujadiliana, kubadilishana mawazo, uzoefu na kuweka mikakati na maazimio mapya ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha- Rose Migiro anasema vijana ni nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Asha- Rose Migiro ameyasema hayo mwishoni mwa wiki mbele ya waandishi wa habari,wakati wa uzinduzi wa ripoti ya maendeleo ya mataifa kuhusu vita dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Ripoti hiyo ambayo inasema miaka 30 ya ukimwi, mataifa bado njia panda, imeandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya ukimwi (UNAIDS).

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo viongozi utakaoanza siku ya jumatano, utaongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. Mohammed Gharib Bilali.

Migiro anasema anaamini vijana wakisaidiwa na kujipanga vizuri ni nguzo muhimu sana kwa sababu amejionea kwa macho yake kile kinachofanywa na vijana wa Tanzania kupitia mtandao wao wa Tanzania Youth Alliance .

Anasema vijana wale wanaukabili vilivyo ugonjwa huo kwa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, katika namna ambayo hata watu wazima hawezi kufanya hivyo.

“Nimeyaona haya nchini kwangu mwenyewe nilipokuwa huko miezi michache iliyopita, nilivutiwa sana na vijana wale namna wanavyosaidiana kwa kuhamasishana, wanaelimishana kwa uwazi na ukweli njia sahihi na salama, na kwakweli wanasaidia sana katika kupunguza kasi ya ugonjwa huu”.anasisitiza Naibu katibu Mkuu.

Akabainisha kuwa juhudi za vijana wale wa Tanzania kupitia mtandao wao, zinaweza kuonekana kama tone la maji katika ndoo. “ Lakini kukiwa na matone mengi, matone hayo yanaweza kuzalisha mawimbi , mawimbi ya mageuzi na hili ndilo linalosisitizwa katika ripoti hii”
Akizungumzia zaidi kuhusu ugonjwa wa ukimwi, Naibu katibu mkuu anasema, miaka 30 iliyopitia wanasayansi waligundua ukimwi, ulikuwa ugonjwa wa ajabu, unaoua na kusambaa.

“ Miongo mitatu baadaye , sasa watu wengi zaidi wanafursa ya kupata dawa, maambukizi yanapungua, na idadi kubwa ya wanawake wajawazito wanaoishi na virusi vya ukimwi wana nafasi kubwa ya kuwakinga watoto wao dhidi ya ugonjwa huo” akasema migiro.

Na kuongeza kuwa mafanikio hayo na mengine mengi dhidi ya ugonjwa wa ukimwi ni matokeo ya ushirikiano wa wadau mbalimbali, zikiwamo serikali, wataalam wa afya, taasisi binafsi,na mashirika ya kimataifa.

“Lakini pamoja na yote hayo, ni mchango mkubwa uliotolewa watu wenyewe wanaoishi na virusi , au wanaishi katika mazingira hatarishi. Hawa walisimama kidete na kujitokeza hadharani na kuzungumza na wakasikika, harakati zao ndizo zimetufikisha hapa tulipo leo hii ingawa bado tunasafari ndefu.” akasisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Akizungumzia mkutano wa viongozi wakuu wa nchi na serikali, Naibu katibu mkuu anasema viongozi hao kupitia mkutano huo wanatarajiwa kutoa tamko jipya la namna gani wamepanga kuchukua hatua kama nchi mojamoja na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuukabili ukimwi miaka 10 ijayo.

“Tunatarajia watueleze juhudi watakazochukua kama nchi moja moja, lakini pia kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, asasi zisizo za kiserikali ili dunia ifike mahali pakuwana na kiwango sifuri cha maambukizi, kiwango sifuri cha unyanyapaa na kiwango sifuri cha vifo vitokanavyo na ukimwi”anasema Migoro.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: