Ndugu Zangu,

KUNA tofauti ya mjinga na mpumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka; ” Kusoma sio kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza”. Kila mwanadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata Profesa anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za kuchomea hindi bichi likachomeka. Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda Profesa.

Lakini upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo ndio upumbavu. Na ndio maana binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa jambo fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?

Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo. Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa amechoka kufikiri. Nilidhani amgetamka, kuwa angeanza kujifunza kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au nchi kavu.

Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na kufikiri ndio njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi mwanadamu anapoacha kufikiri? Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid

Iringa,

Jumanne, Machi 22, 2011
http://mjengwa.blogspot.com

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: