UTANGULIZI
Mnamo tarehe 7/5/2006 Maafisa wawili ( Bi. Doris Mwanri na Bi. Chaurembo) wa TASAF kutoka Manispaa ya Ilala walikuja kwenye mkutano wa wananchi wa Ugombolwa kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kuhusu miradi yao ya maendeleo ambayo ingefadhiliwa na mfuko wa TASAF. Katika mkutano huo ambao wananchi walihamasika sana Mhe. Diwani wa Kata ya Segerea Bw. Kalunga M. Kalunga alikuwepo pia. Mkutano mwingine wa wananchi uliitishwa tena tarehe 28/5/2006 kwa nia ya kuibua miradi ya kufadhiliwa na TASAF. Miradi iliyoibuliwa wakati ule ilikuwa barabara, soko na maji. Wakati haya yote yalikuwa yanafanyika viwanja na 9 & 10, Kitalu “S” vilikuwa na mabango yaliyosomeka “ HILI NI ENEO LA MAENDELEO YA WANANCHI-SOKO”.
Mwishoni mwa mwaka huo wa 2006 baadhi ya wananchi wa Ugombolwa walipata tetesi kuwa eneo walilotegemea kwa shughuli ya soko linamilikishwa kinyemela mke wa mtaa jirani wa Migombani. Hatimaye tarehe 19/12/2006 wananchi wapatao 40 wa mtaa wa Ugombolwa waliandika barua ya malalamiko kuhusiana na hali hiyo kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Segerea. Nakala ya barua hiyo walipewa Mhe. Diwani wa Kata ya Segerea
( Bw. Bw. Kalunga M. Kalunga ), Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Mbunge wa Jimbo la Ukonga (Dkt. Milton Makangoro Mahanga) na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ugombolwa. Barua hiyo haikufanyiwa kazi na Kiongozi ye yote.
Mnamo tarehe 7/2/2007 wananchi hao 40 wa mtaa wa Ugombolwa walimwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuhusu eneo lao kumilikishwa kinyemela mke wa mtaa jirani wa Migombani aitwaye Rose Samwel Binagi. Barua hiyo nayo haikujibiwa.
MATUKIO MENGINE
Mnamo tarehe 16/3/2007 Kaimu Katibu wa Kamati ya Soko kwa wakati ule Bw. Timothy N.Kirway alikwenda Ofisi ya TASAF Manispaa ya Ilala kuulizia maendeleo ya mradi wa Soko. Alikutana na Meneja wa Mradi wa TASAF Bw. M.K.Msoffe ambaye alieleza kuwa Bw. Samwel Binagi amekwenda kwenye ofisi yake kupinga mradi huo wa wananchi ati kwa sababu eneo husika lina mgogoro. Aidha, Bw. Msoffe alieleza kuwa Maafisa kutoka ofisi yake wangekuja tena Ugombolwa ili kuthibitisha vipaumbele vya miradi iliyoibuliwa awali kwa njia ya mlinganisho kijozi (pair-wise ranking).
Tarehe 13/5/2007 Maafisa wawili wa TASAF kutika Manispaa ya Ilala walikuja kwenye mkutano wa wananchi ili kuthibitisha vipaumbele vya miradi iliyoibuliwa awali kwa njia ya mlinganisho kijozi (pair-wise ranking). Mradi uliopata kipaumbele cha kwanza ulikuwa wa soko. Maafisa hao walikuwa Bi. Lilian Shoo na Bw. Nicas Nsemwa. Wakati wa mkutano huo Kamati ya Soko ilichaguliwa upya chini ya usimamizi wa maafisa hao wa TASAF. Viongozi wakuu waliochaguliwa walikuwa Bw. Emmanuel Kaigarula (Mwenyekiti), Bibi Anna T. Kirway ( Makamu Mwenyekiti), Bw. Mhabuka (Katibu) na wajumbe wengine wanne. Maafisa wa Manispaa walipomwuliza Mwenyekiti wa wakati ule ( Bw. Elly J. Mdundo ) kama eneo la soko lipo, alijibu kuwa lipo.
Baada ya Kamati hiyo ya soko kuchaguliwa jitihada mbalimali zilifanywa na Wanakamati kumwona Kamishna wa Ardhi kwa safari zisizopungua nne kuhusu Bibi Rose S. Binagi kumilikishwa eneo la wananchi kinyemela, lakini kamati hiyo haikufanikiwa kumwona Kamishna huyo. Tarehe ambazo Wanakamati walifanya miadi (appointment) ya kumwona Kamishna bila mafanikio zilikuwa 16/5/2007; 23/5/2007; 6/6/2007 na 21/11/2007.
Mkutano mwingine wa wananchi wa Ugombolwa ulifanyika tarehe 1/12/2007 ambapo maendeleo ya suala la soko yalijadiliwa kwa kina na wananchi wakaamua kuunda upya Kamati ya soko, nje ya utaratibu wa mradi wa TASAF, ili kupeleka tatizo la mgogoro wa viwanja husika kwenye ngazi za juu zaidi baada ya kuona kuwa Kamishna wa Ardhi alikuwa anakwepa kukutana na Kamati ya awali.
Katika uchaguzi huo mpya uliofanyika tarehe 1/12/2007, Bw. Emmanuel Kaigarula alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti na Bw. Timothy N.Kirway alichaguliwa kuwa Katibu. Wajumbe wengine watano wa Kamati hiyo walichaguliwa pia na wananchi hao wa Ugombolwa.
Mara baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Soko alimwandikia Mhe. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ( wakati ule akiwa Mhe.John P. Magufuli ) barua ya malalamiko ya wananchi kuhusu viwanja vyenye mgogoro. Barua hiyo iliandikwa tarehe 6/12/ 2007 na kujibiwa tarehe 18/12/2007 ikimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kulishughulikia tatizo hilo mara moja.
Kwa bahati mbaya baadaye huyo Waziri kahamishiwa Wizara nyingine na na mchakato ukaanza upya. Tofauti na Waziri Magufuli tangu Mhe. John Z. Chiligati ashike uongozi wa Wizara hiyo, Kamati mpya ya soko imekuwa ikipokea ahadi mbalimbali za Waziri huyo kutembelea Ugombolwa tangu Machi, 2008 hadi leo. Aidha, tarehe 23/9/2008 Wizara hiyo iliunda Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Bw. Vincent Shaidi lakini hadi leo wananchi wa Ugombolwa hawajapata matokeo ya Tume hiyo pamoja na kwamba Mhe. Waziri huyo alikumbushwa kwa barua za tarehe 7/11/2008 na tarehe 10/9/2009. Isitishe, majibu ya barua ya tarehe 10/9/2009 yamekuwa yakifuatiliwa na Wanakamati ya Soko huko Ardhi tarehe 30/9/2009; 7/10/2009; 15/10/2009 na Desemba, 2009 lakini bila mafanikio yo yote.
KELELE ZA WAUMINI WA KIKUNDI CHA DINI CHA PENTECOSTE RENEWAL ASSEMBLY
Tangu Agosti, 2008 wananchi wa Ugombolwa tumekuwa tukisumbuliwa sana na kelele za Waumini wa Kikundi cha dini cha Pentecoste Renewal Assembly chini ya Mch. Wilson Mwawogha. Kikundi hicho kiliuziwa eneo hilo lenye mgogoro na Bibi Rose S.Binagi.
VITISHO MBALIMBALI KWA WANAKAMATI
Kamati mpya ya soko imekuwa ikipata vikwazo mbalimbali kutoka kwa wapinga maendeleo wa eneo lao. Kwa mfano, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa aliyetanguliwa pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Soko na Katibu wake wamewahi kushitakiwa na Bw. Samwel Binagi kwa Katibu Tarafa ya Ukonga (Bw. Jeremiah Makorore ati kwa kuwahamasisha wananchi; Mwenyekiti wa Kamati ya Soko na Katibu wake pia walibambikiziwa kesi ya kuchoma kitambaa cha Kanisa na Mch. Mwawogha akishirikiana na Bw. Binagi. Kesi hiyo haijapelekwa Mahakamani hadi leo. Aidha, mjumbe mmoja wa Kamati ya Soko alinusurika kupigwa jembe kichwani na Bw. Binagi.
Viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya wamefika Ugombolwa kuhusu Tatizo hili. Kwa mfano aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala( Balozi Patrick Tsere) alitutembelea tarehe 18/9/2008 na Mkuu wa Wilaya aliyemfuata (Bw. Evans Balama) alikuja kusikiliza matatizo ya Ugombolwa tarehe 24/7/2009. Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam ( Mhe. Abbas Kandoro) alifika mwaka 2009.
JARIBIO LA KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI
Tarehe 10/1/2010 baadhi ya wananchi wa Ugombolwa walimwandikia Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kufungua kesi dhidi ya Rose S. Binagi na Mchg. Wilson Mwawogha kuhusu kelele zinazotokana na Kikundi cha dini cha Pentecoste Renewal Assembly. Mkurugenzi huyo hakuchukua hatua yo yote. Aidha, wananchi hao walimwandikia Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam (Mhe. William Lukuvi) amwagize Mkurugenzi wa Manispaa kufungua kesi hiyo. Kwa bahati mbaya hadi leo hao wananchi hawajaona matokeo yo yote.
UWEZEKANO WA VIGOGO JUU YA MANISPAA NA MKOA KUKWAMISHA JUHUDI ZA WANANCHI WA UGOMBOLWA
Kiburi cha kikundi cha Mch. Wilson Mwawogha kupigia wananchi wa Ugombolwa kelele bila kujali kama kuna wagonjwa na wanafunzi wanasoma na pia mlolongo wa matukio mbalimbali hapo juu kuna- ashiria kuwa kuna uwezekano mkubwa wa vigogo juu ya manispaa na mikoa kulindana au kuogopana na hivyo haki isiweze kutendeka kwa wananchi w Ugombolwa. Kwa hali hii kimbilio la mwisho la sisi wananchi wa Ugombolwa ni Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete). Kwa hiyo ni juu ya wananchi kuteua baadhi ya watu miongoni mwao walio waadilifu na jasiri ili kumwona huyo Mkuu wanchi yetu na kuwasilisha tatizo hili kwake kwa ufasaha bila woga, chuki wala uendeleo wo wote.
MWISHO
Katika kushughulikia tatizo hili la soko Kamati ya Soko imegungua kuwa baadhi ya viongozi katika ngazi mbalimbali kweli ni wachapa kazi kwa kutumikia vizuri Umma wa Tanzania. Katika ngazi ya Taifa tutamkumbuka sana Mhe. Magufuli alivyolishughulikia kwa haraka tatizo letu. Kwenye ngazi ya Kata tumepata ushirikiano mzuri sana kutika kwa Afisa Mtendaji wa sasa wa Kata ya Segerea. Aidha, Mtendaji wa sasa wa Mtaa wa Ugombolwa amekuwa wa msaada sana kwetu sisi wananchi. Isitoshe, Mwenyekiti wa zamani wa Mtaa wa Ugombolwa Bw. Elly J. Mdundo wakati wa uongozi wake alitupa ushirikiano mzuri sana. Ni Mwenyekiti huyo wa zamani aliyeshinda katika kura za maoni ya CCM lakini jina lake halikurudishwa kwetu kupigiwa kura wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mtaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa upande mwingine, kwa maoni yetu, baadhi ya viongozi hawakututendea haki. Kwa mfano Mhe. Diwani wa Kata ya Segerea na Mhe. Mbunge wa Jimbo la Ukonga walihahamu tatizo hili tangu mwaka wa 2006 lakini walishindwa kabisa kutusaidia. Mnamo tarehe 21/8/2008 majira ya saa 2:00 usiku wakati Kamati ya Soko ilikuwa inakaaa Mwenyekiti wa Kamati alimpigia simu Mhe. Mbunge wa Jimbo la Ukonga uwezekano wa kukutana naye ili kujadiliana na Kamati ya Soko kuhusu eneo lenye mgogoro. Kwa mshangao mkubwa wa Wanakamati hao Mhe. Mbunge alijibu kuwa yeye hawezi kuzungumzia suala la kiwanja kilichomilikishwa mtu “kihalali”.Mwenyekiti wa sasa wa Serikali ya Mtaa (Bi. Mariam Machicha) pamoja na kuwa hakuwa ameongoza kwenye kura za maoni za CCM, jina lake ndilo lililorudishwa kupigiwa kura wakati wa uchaguzi. Kwa makusudi Mwenyekiti huyu wa sasa amekuwa akikwepa suala la soko lisijadiliwe katika mikutano miwili aliyoiitisha tangu achaguliwe. Aidha, ameshindwa kuchukua hatua dhidi ya kikundi cha dini cha Pentecoste Renewal Assembly kinachowasumbua sana wananchi wa Ugombolwa. Katika mkutano wa wananchi uliofanyika tarehe 21/3/2010 aliingiza tatizo la mgogoro wa familia yake na Mwenyekiti aliyetangulia na hatimaye mkutano kuvunjka. Mwenyekiti huyu wa sasa amekuwa akikataa, kwa makusudi, kupokea barua ya wananchi wa Ugombolwa ya tarehe 12/4/2010 kumwomba aitishe haraka mkutano maalum wa wananchi kujadili suala la soko.
Kwa upande wake Bw. Samwel Binagi, akiwa mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa muda usiopungua miaka kumi, alikuwa anajua fika nia ya wananchi wa Ugombolwa kujenga soko katika eneo hilo. Badala yake akawazunguka hao wananchi na kummilikisha eneo hilo haraka haraka mke wake. Hadi Desemba, 2009 kiwanja cha jirani Na. 8 hakijamilikishwa kwa mwombaji wa tangu 2006. Bw. Binagi alitoa taarifa ya Uwongo kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kuwa ana kibanda kwenye eneo lenye mgogoro wakati akijua sio kweli. Bw. Binagi alitaka kumpiga jembe kichwani mmoja wa Wanakamati. Isitoshe, Bw.Binagi anatuhumiwa kuuza eneo la wazi lililotengwa kwa maendeleo ya Kata ya Segerea ( Kwa maelezo zaidi soma Gazeti la Dar Leo la Jumatatu ya tarehe 3 Mei, 2010 uk. wa 3).
Toa Maoni Yako:
0 comments: