Jinsi ya kuamsha na kulinda ari ya kutimiza malengo yako
Na Jeff Msangi,
Kila mtu ana malengo. Tunachotofautiana ni jinsi tunavyofafanua malengo yetu na mbinu tunazozitumia ili kutimiza malengo yetu. Iwe ni kumaliza madeni uliyonayo, kuwekeza pesa kwa ajili ya kuchukua likizo ndefu,utajiri,familia bora,ndoa nzuri iliyojaa furaha,watoto wenye heshima na adabu, kufanya mazoezi ili kuwa na afya njema zaidi nk yote ni malengo ambayo binadamu hujiwekea mara kwa mara katika safari ya maisha.
Wengine hufanikiwa na wengine hushindwa. Furaha,mafanikio na maendeleo maishani ni vita ya kudumu.Kuna kupanda na kushuka. Cha msingi ni jinsi mtu anavyokabiliana na hali halisi katika wakati halisi.
Kama ambavyo nimeshaandika katika makala zangu za siku za nyuma,kujiwekea na kufafanua vizuri malengo yako ni sehemu muhimu sana ya maisha,maendeleo na mafanikio.
Ni lazima ujue unataka kufanya nini,kwanini na kwa namna au mtindo gani. Malengo ya uhakika ni kama vile kuwa na uhakika na unapotaka kwenda. Usipojua unapotaka kwenda kamwe hutokuwa na uhuru wa kusema “umepotea” kwani hata ulikuwa hujui unapotaka kwenda!Umepoteaje?
Ulikuwa unataka kwenda wapi? Maswali magumu.
Lakini pamoja na malengo ni lazima pia pawe na tamaa au ari ya kutimiza malengo hayo.
Hapo ndipo swali la kwanini linapokuja. Kwanini unatamani utajiri? Kwanini unataka kuwa mwanafunzi bora kushinda wengine wote?Kwanini? Tunapojiuliza maswali kama hilo la kwanini,inatusaidia kuamsha tamaa au ari.Tunakumbuka zaidi malengo yetu na yanakuwa ya uhakika zaidi.Tunajua tunapotaka kwenda na sababu za safari yetu tunazo.
Hata hivyo, mara kwa mara mambo mbalimbali hutokea maishani ambayo yanaweza kutukatisha tamaa. Hapo ndipo tunapohitaji motisha kama ambavyo niliongelea wiki kadhaa zilizopita.
Sasa ili kuhakikisha kwamba siku zote unabakia kuwa katika mstari mnyoofu kuelekea kwenye malengo yako, yapo mambo mbalimbali (unaweza kuyaita maandalizi ukipenda) ambayo unaweza kufanya ili kuhakikisha kwamba safari yako kuelekea kwenye kutimiza malengo yako inakuwa ngumu(siku zote ni ngumu) lakini yenye mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugumu wowote utakaojitokeza.Hicho ndicho ninachotaka kuongelea hivi leo; ufanye nini ili usikate tamaa katika kuelekea kwenye malengo yako?
Chagua malengo yanayofaa: Kama nilivyotangulia kusema,tuna malengo tofauti hapa duniani. Jambo la msingi ni kuchagua malengo yanayokufaa.Ni lazima kujifanyia uhakiki binafsi na kujikosoa kwa dhati.Unataka kufanya nini au kuwa kama nani? Unavyo vitendea kazi(vikiwemo vya kimaadili) ili kutimiza malengo yako?Umechagua malengo yanayofaa na hata kukubalika katika jamii yako?Yapo maswali kadhaa(mfano tu) ambayo yanaweza kukusaidia katika kuchagua malengo yanayokufaa
-Je ulimwengu usingekuwa na kitu “pesa” bado ungetaka kutimiza lengo ulilonalo?
-Je tayari umeshaanza kuyafanyia kazi malengo uliyonayo?
-Je ningekupatia Tshs Bilioni moja hivi leo bado ungeendelea kushikilia malengo uliyonayo?
Kama umejibu Hapana katika swali moja au yote hapo juu,una haja ya kuyakagua upya malengo yako. Swali la mwisho hapo juu ni muhimu sana kwani pengine hutopenda kusikia nikikuambia kwamba pesa haitokupa furaha maishani.Kinachoweza kukupa furaha ni ile process ya kuzipata pesa.Hili nitakuja kuliongelea kwa undani katika siku za mbeleni.
Tambua kwamba unaweza kufanya unachotaka kufanya: Ukimuuliza mtu yeyote ambaye tayari ana malengo kwamba ni kwa kiasi gani na kwanini angependa kutimiza malengo aliyonayo, utasikia hadithi nzuri na ndefu ya jinsi ambavyo maisha yake yangebadilika endapo itatokea akatimiza malengo yake. Sasa jiulize, ni kwanini hatimizi malengo yake?
Nini kinamzuia? Au nikuulize wewe msomaji,nini kinakuzuia? Jibu rahisi ni kwamba kama ilivyo kwa wengi wetu,hatuamini kwamba tunaweza kufanya tunachotaka kufanya.
Kwa hiyo tunabakia kuwa na “ndoto za malengo”.Hatuthubutu hata kujaribu!Tunaingiwa na woga. Tunawaza jinsi tutakavyoshindwa kama tutajaribu. Tunaona jinsi tutakavyochekwa,tutakavyodhihakiwa nk.
Kwa hiyo ni lazima ujenge kwa ndani imani kwamba unaweza,inawezekana na hakuna cha kukuzuia.
Kama alivyowahi kusema bwana mmoja aitwaye David Deida; “Kitu pekee kinachofanya ndoto zisitimie ni uoga wa kushindwa”. Usikubali.
Weka Nukuu za Mafanikio ya Wengine:
Uwezekano ni mkubwa sana kwamba kile unachotaka kufanya au ambacho ndio malengo yako,mafanikio yako, tayari kuna mtu au watu ambao wameshakifanya hapa duniani. Ni kina nani? Wao walifanyaje? Ni kitu gani kiliwasaidia kufanikiwa au kufikia walipofikia?
Hayo ni baadhi tu ya maswali ambayo ni muhimu ukayapatia majibu kwani majibu hayo bila shaka yatakusaidia katika safari yako.Pia kwa kuona na kujifunza kutoka kwa wengine, itakupa ari na moyo zaidi kwamba inawezekana. Kama wao walifanya na wakafanikiwa,kwanini wewe ushindwe?
Tafuta Wenzako Wenye Malengo Sawa na Wewe: Mojawapo ya mambo yanayoleta faraja au ahueni katika maisha yetu ni pale unapokutana na mtu ambaye ana “matatizo” au mtu mwenye “misheni” sawasawa na yale uliyonayo.
Ahueni inakuja pale unapogundua kwamba kumbe haupo peke yako.Kunakuwa na nafasi ya kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wengine.
Hali ni hiyo hiyo kama unatamani mafanikio na hutaki kukatishwa tamaa njiani.
Jaribu kutafuta marafiki au watu ambao mnafanana katika mawazo na malengo.Ukishawapata nenda nao sambamba. Shirikiana na pia saidiana nao.Mara nyingi motisha hutoka kwa watu kama hao.Jipime mwenendo wako kuelekea katika mafanikio kwa kujilinganisha nao.Shindana nao ikibidi.
Kwa ufupi kila mmoja wetu,ukiwemo wewe unayesoma makala hii, ana uwezo wa kujiwekea malengo na kuyatimiza. Amini kwamba unaweza kufanya unachotaka kukifanya.Amini kwamba malengo uliyonayo yanaweza kufikiwa(kumbuka kujiwekea malengo halisia au yanayotimizika).
Tafuta wenzako ambao aidha wameshafanikiwa au walio njiani kufanikiwa.Angalia mienendo yao.Waulize na upate majibu kutoka kwao ikiwezekana.
Soma habari zao iwe ni magazetini au mitandaoni.Kumbuka kama wao wameweza basi hakuna cha kukuzuia.Kuwa jasiri katika malengo yako.Wapo watakaojaribu kukuyumbisha na kukukatisha tamaa. Usiwajali.Mwisho kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza siku zote;Fanya kazi kwa bidii,uadilifu na maarifa.Tuonane wiki ijayo.
Jeff Msangi ni Mhariri wa mtandao wa www.bongocelebrity.com Unaweza kuwasiliana naye kupitia makala@bongocelebrity.com

Toa Maoni Yako:
0 comments: