Binti wa Kizungu ambaye ni ‘chachandu’ ya shoo za THT

*Asema muziki wa Tanzania upo juu, ni kipenzi kikubwa cha Hip Hop

Na Michael Maurus

MIONGONI mwa vivutio katika shoo zinazofanywa na kundi la sanaa la Tanzania House of Talent (THT), ni yule mcheza shoo wao wa ‘Kizungu’ ambaye amekuwa akifanya mambo makubwa jukwaani.

Binti huyo ambaye ni raia wa Ujerumani, anafahamika kwa jina la Hanna Elisabeth Waltsgott, au mwenyewe hupenda kujiita ‘Hanuta’, jina alilopewa na babu yake alivyokuwa mtoto.

Kwa jinsi anavyocheza na uwezo wake wa kujinyonganyonga, kulingana na mtindo wao, huwezi kuamini kama binti huyo hana muda mrefu katika kundi hilo lililoanzishwa miaka mitatu iliyopita.

‘Hanuta’, jina alilopewa kutokana na uzito wake katika kuzungumza lugha ya Kijerumani, alijiunga na THT siku nne kabla ya kundi hilo kufanya shoo mkoani Tanga katika Tamasha la Fiesta.

Lakini kutokana na umakini wake pamoja na mapenzi yake katika sanaa, siku hizo chache zilimtosha kabisa kwenda sambamba na wenzake katika kucheza.

Akiongozwa na kinara katika kucheza kwa wasichana, Kay, Hanna, alifanikiwa kuwa mkali mno katika kipindi hicho kifupi kiasi cha kujizolea mashabiki lukuki kila kundi lake lilipofanya mambo.

Na katika matamasha ya Fiesta ambayo binafsi nilipata nafasi ya kuhudhuria, kuanzia mkoani Arusha kwenye viwanja vya klabu ya usiku ya Matongee na hata mkoani Mwanza pale Yatch Club na Uwanja wa CCM Kirumba, binti huyo aliendelea kuwa gumzo.

Nakumbuka pale CCM Kirumba kuna mashabiki wa muziki ambao nilikaa nao karibu ambao walikuwa wakijiuliza kama binti huyo ni ‘Mzungu’ au ‘Mbongo’ kutokana na jinsi alivyokuwa akifanya mambo.

Kutokana na jinsi alivyokuwa kivutio katika matamasha ya Fiesta, likiwamo lile la jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Leaders Club hivi karibuni, gazeti hili liliamua kumtafuta binti huyo ili kufanya naye mahojiano.

Baada ya kuhangaika kwa zaidi ya wiki mbili, hatimaye binti huyo alitinga katika ofisi za gazeti hili zilizopo Sinza Kijiweni, jijini jana ambako alizungumzia jinsi alivyojiunga na THT hadi sasa anapokaribia kurejea kwao Ujerumani.

“Mimi nilikuja hapa Tanzania kwa ajili ya kufanya kazi ya kujitolea katika moja ya vituo vya watu wenye ulemavu vya hapa,” alisema Hanna.

Alisema kuwa alipofika nchini, alijikuta akitua katika kituo cha Mtoni Special School kilichopo Mtoni Mtongani, Dar es Salaam.

Pamoja na kuja kwa lengo hilo, lakini alijikuta akivutika kufanya kitu kingine, ikiwa ni sehemu ya kujifunza mambo mengi zaidi ambayo anaamini kuwa yatamsaidia katika maisha yake ya kila siku.

Hapo ndipo alipotua THT, lakini ilikuwa ni baada ya kuomba ruhusa kwa wenyeji wake ambao pia ni raia wa Ujerumani.

“Nilipofika pale THT niliwaambia kuwa ninataka kujiunga nao katika kucheza, wakataka nifanye majaribio, waliponiona ninaweza, wakanikubalia kuwa nao.

“Nilipoanza mazoezi ilikuwa ni siku nne kabla ya kwenda Tanga kwenye Fiesta, lakini kwa kuwa niliweza mapema, na mimi nilipanda jukwaani kule Tanga na nilicheza vizuri kama wengine.”

Kuanzia hapo, Hanna akawa ni miongoni mwa vipaji vya THT ambaye alikuwa ni miongoni mwa ‘chachandu’ katika shoo zao.

Hata hivyo, nchini kwao binti huyo hakuwa akijihusisha na muziki kama ilivyo hapa nchini, zaidi ya kucheza na kuimba akiwa chumbani kwake kama sehemu ya kujifurahisha.

Binti huyo alisema kuwa alijifahamu kuwa na kipaji cha muziki, lakini kutokana na kukabiliwa na masomo, alijikuta akishindwa kukitumikia kipaji chake hicho.

“Nilipowaambia ndugu zangu kuwa ninacheza muziki huku na moja ya kundi la sanaa, walishangaa sana na pia walifurahi, nimepiga picha nikiwa ninacheza ili niwapelekee waamini niliyokuwa nikiwaeleza,” alisema.

Wakati ikiwa ndio kwanza mashabiki wa burudani wameanza kupandwa na ‘mzuka’ na Hanna, muda si mrefu, binti huyo hataonekana tena katika jukwaa la THT.

Mkataba wake wa kuendelea kuwapo hapa nchini, unamalizika wiki ijayo.

“Nimekuja hapa kufanya kazi kwa miezi mitatu tu, wiki ijayo ninatakiwa kurudi katika nchi yangu, ila nitawakumbuka sana Watanzania.

“Ninaondoka Tanzania nikiwa bado ninawapenda, naona siku zimekwenda haraka sana, siamini kama tayari nina visa mkononi ya kuniwezesha kurudi Ujerumani, siamini hata kidogo,” alisema.

Binti huyo ambaye alisema kuwa anapenda mno kula chapati ambazo hata alipokuwapo ofisi za gazeti hili alitaka kupelekwa sehemu zinapouzwa, alisema kuwa ukaribu na ucheshi wa Watanzania, ni miongoni vya vitu vitakavyoendelea kuwapo katika kumbukumbu zake.

Akizungumza maneno machache ya Kiswahili, ikiwamo lugha ya mitaani kama ‘mzuka’, ‘vihepe’ akiwa na maana chipsi na mengineyo, alisema kuwa iwapo angekaa hapa nchini kwa muda wa mwaka mzima, angekuwa mtaalamu wa lugha hiyo.

“Mungu akipenda nitarudi tena Tanzania, nije kula ugali na chipsi mayai, ninapenda sana ugali.”

Akizungumzia fani ya muziki hapa nchini, Hanna alisema kuwa ipo juu mno japo haijafanikiwa kujitangaza kimataifa.

Hanna anaelezea jinsi alivyoguswa na ujumbe uliomo katika nyimbo za wasanii wa hapa nchini baada ya kutafsiriwa kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza.

Alisema kuwa ili wasanii wa hapa nchini wapate mafanikio ngazi ya kimataifa, ni budi wakatoa kazi zao nje ya mipaka ya nchi.

“Hata lugha nayo ni muhimu, ni vema wakaandaa na kazi zao katika lugha mbalimbali, zaidi ikiwa ni zile zinazotumiwa na nchi mbalimbali,” alisema.

“Nadhani kama wakiimba katika lugha ya Kiingereza, wanaweza kupata mafanikio zaidi kwa kazi zao kujulikana na watu wengi zaidi katika ngazi ya kimataifa.”

Alisema kuwa binafsi anavutiwa mno na muziki wa Hip Hop na kwa hapa nchini, wasanii wanaomvutia ni Joh Makini, Nako 2 Nako, Profesa Jay, Ngwair na Joe Makini.

“Lakini wanaonivutia zaidi ni THT, na ninatamani siku moja niwe nao Ujerumani ili wakaonyeshe vipaji vyao. Nitafanya kila linalowezekana ili niweze kwenda na DVD zao ili nikawatangaze huko,” alisema.

Hanna alizaliwa Julai 14, 1988 katika Jiji la Hamburg, Ujerumani, akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wawili, wakiwa na mwenzake, Linette.

Baba yake anafahamika kwa jina la Uwe Waltsgott, wakati mama yake ni Beatrice Waltsgott.

Alianza elimu ya msingi mwaka 1994 na kumaliza 1998, mwaka uliofuata alijiunga na chuo cha WDG na kuhitimu Juni mwaka huu ambako alitunukiwa shahada ya sanaa.

Baada ya kuhitimu, aliamua kuchagua kufanya shughuli za kijamii na hapo ndipo alipojikuta akitua Tanzania na hatimaye katika jukwaa la THT.

Huyo ndiye Hanna Elisabeth Waltsgott, ambaye ni chachandu ya shoo za THT.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

1 comments:

  1. a very nice artice to read, big up maurus

    ReplyDelete