TAASISI ya utafiti wa kudhibiti Malaria (RTI) limepongeza hatua za kupambana na maradhi hayo zilizofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kusaidia sekta ya afya katika kuyatokomeza kabisa Malaria hapa nchini.

Kiongozi wa ngazi za juu wa Taasisi hiyo, Dk. Victoria Haynes aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekaiti wab Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Dk. Haynes alimueleza Rais Karume kuwa Taasisi ya RTI imefarajika kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanya na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya hapa Zanzibar katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dk. Haynes alieleza kuwa mafanikio yalipatika hapa Zanzibar katika kupiga vita Malaria yametokana na kuwepo kwa wataalamu mahiri kutoka Wizara ya Afya ambao wamesaidiana kikamilifu na taasisi hiyo katika kufanikisha mafanikio hayo.

Pia, Dk. Haynes alimueleza Rais Karume kuwa jitihada mbali mbali zimekuwa zikifanyika na taasisi ya RTI katika kupiga vita Malaria, na kusifu juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Karume kwa kuweka mikakati ya kupambana na Malaria.

Dk. Haynes alieleza kuwa programu inaendelea ya kupiga vita Malaria kwa kuanzia katika maeneo ya Muleba na Gagera huko Tanzania Bara chini ya taasisi hiyo utekelezaji ambao unafuata kutokana na mafanikio yaliopatikana Zanzibar ambapo pia aliahidi nafasi za masomo kwa Zanzibar.

Aidha, Dk. Haynes alisifu mipango na taratibu zilizowekwa katika vituo vya afya vya Zanzibar viliopo mjini na vijijini katika kutoa huduma za afya ikiwemo huduma ya uchumguzi wa maradhi ya Malaria kwa wananchi.

Sambamba na hayo, Dk. Haynes alisema kuwa taratibu zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya za kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kupambana na Malaria hali ambayo imeonesha mafanikio makubwa.

Nae Dk. Karume alimpongeza Dk. Haynes kutokana na utendaji mzuri sambamba na mashirikiano ya taasisi anayoisimamia ya RTI katika kusaidia kupiga vita Malaria hapa Zanzibar.

Rais Karume alimueleza Dk. Haynes kuwa Zanzibar inathamini sana misaada pamoja na ushirikiano uliopo kati yake na taasisi hiyo ambayo matunda yake yameweza kuonekana hapa Zanzibar na kutambulika dunia nzima.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alimuhakikishia Dk. Haynes kuwa Zanzibar itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili kupata mafanikio zaidi katika kutokomeza Malaria.

Rais Karume alieleza kuwa kuimarika kwa miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara na mawasiliano pamoja na ukaribu wa huduma za afya na elimu hapa Zanzibar nako kumechangia kufikia mafanikio yaliopatikana.

Pamoja na hayo, Rais Karume aliishukuru taasisi hiyo sanjari na Shirika la USAID kwa kuwa bega kwa bega katika kupambana na Malaria hapa Zanzibar na hivi sasa kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kujijengea mazingira mazuri kwa wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kutoka nje ya nchi wakiwemo watalii.

Miongoni mwa nchi ambazo RTI inafanya kazi zake kwa hapa Afrika ni Angola, Zanzibar, Tanzania Bara, Eritria, Zambia, Uganda, Ethiopia, Madagaska, Malawi, Ghana, Kenya, Mozambique, Rwanda, Senegal, Benia, Liberia na Mali ambapo Dk. Haynes alisifu mafanikio makubwa yaliopatika Zanzibar ikilinganishwa na nchi hizo.

Taasisi ya RTI inamakubaliano ya kufanya kazi zake hapa Zanzibar kwa muda wa miaka mitano kuanzia Desemba 27, 2006 hadi Desemba 26, 2011 kwa kupitia Programu ya (ZMCP) pamoja na programu ya (NMCP) ikiwemo utiaji dawa majumbani na kinga nyengine za maradhi hayo.

Habari kwa hisani ya Rajab Mkasaba wa Ikulu Zanzibar.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: