Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk.Wilbrod Slaa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam jumamosi.Kulia ni Balozi Christopher Ngaiza.-----------
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeunda Kamati Ndogo kwa ajili ya kuchunguza viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kukihujumu, imefahamika. Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbroad Slaa alisema hayo jumamosi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu tamko la Kamati Kuu ya chama hicho baada ya mkutano wake uliofanyika hivi karibuni.Dk. Slaa alisema kwa muda sasa kumekuwa na mikakati inayofanywa na baadhi ya watu ndani na nje ya chama hicho kwa lengo la kuhujumu taswira ya chama hicho na Mwenyekiti wake wa Taifa, Freeman Mbowe. Alisema hujuma hizo ndani ya chama zimekuwa zikihusisha baadhi ya viongozi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa taarifa za upotoshaji kwa umma.
Alidai pia kwamba wahujumu hao wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kutimiza azma yao ingawa hakufafanua. Kwa mujibu wa Dk. Slaa kutokana na mfululizo wa madai hayo ya hujuma Kamati Kuu imeamua kuunda Kamati Ndogo itakayoongozwa na Mwenyekiti mstaafu wa Chama hicho, Bob Makani, itakayofanya uchunguzi dhidi ya viongozi na wanachama ambao wanatuhumiwa kukihujumu katika ngazi mbalimbali.
Dk. Slaa alisema kamati hiyo itawasilisha taarifa yake kwenye kikao kijacho na kwamba hatua zaidi zitachukuliwa kwa wale wote watakaotiwa hatiani kama njia ya kukiwezesha chama hicho kufikia malengo yake. Alisema Chadema pia inalaani kitendo cha baadhi ya wanasiasa kutumia msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Tarime marehemu Chacha Wangwe kuhujumu taswira ya chama hicho na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Dk. Slaa alisema Kamati Kuu imeshapokea taarifa ya awali ya wanasheria wake na kwamba imewaelekeza kufungua mashitaka dhidi ya watu na vyombo vya habari inavyoamini vilihusika kuwachafua viongozi na chama hicho, hasa Mbowe. Katibu Mkuu huyo alisema Kamati Kuu ina imani kubwa na Mbowe na kumpongeza kwa jinsi alivyoweza kutulia na kuonyesha busara wakati chama hicho kikikabiliwa na vitendo vya hujuma.
“Kamati Kuu imesikitishwa zaidi na kitendo cha kumhusisha Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na msiba wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti (Chacha Wangwe). Inalaani kitendo cha baadhi ya wanasiasa wa upinzani na CCM kutaka kutumia msiba wa marehemu Chacha Wangwe kujijenga kwa kuwa si utamaduni wetu Watanzania,” taarifa hiyo ilieleza.


Toa Maoni Yako:
0 comments: