WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Peter Pinda, anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa albamu ya mwimbaji wa nyimbo za injili hapa nchini Bi. Flora Mbasha, utakaofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Baada ya kukaa kimya tokea ametoa wimbo wa Adui yako uliopo kwenye albamu ya Haleluya Collections Vol.4, Flora anatarajia kuzindua albamu yake ya pili iitwayo Furaha Yako.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili jijini Dar es Salaam hivi karibuni, mwimbaji huyo alisema sasa yuko tayari kuwapa wapenzi wake ladha nyingine tofauti na ile ya mwanzo.

"Namshukuru Mungu kwa kuweza kunifanikishia mpaka nimeandaa albamu yangu ya Furaha Yako ambayo naamini itakuwa ni gumzo," alisema Bi. Mbasha.

Alisema kuwa mpaka sasa amejipanga vema kwa ajili ya uzinduzi huo utaofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda.

Bi. Mbasha aliongeza kuwa, uzinduzi huo utaenda pamoja na uzinduzi wa video ya Unifiche, ambayo ipo kwenye albamu ya pili.

Alizitaja nyimbo hizo 12 zilizopo kwenye albamu hiyo ya Furaha Yako kuwa ni; ‘Rudi nyuma Shetani’, ‘Adui yako ni rafiki yako’, ‘Tufurahie’, ‘Usife Moyo’, ‘Mteule usiogope Yesu anaweza’ na ‘Furaha Yako’ wimbo uliobeba jina la albamu.

Nyingine ni ‘Natembea na Yesu’, ‘Yesu Anaweza’, ‘Tutamwona’, ‘Mwanamke simama imara’ na ‘Yerusalemu’.

Waimbaji watakaomsindikiza siku hiyo ni pamoja na kwaya za mjini Dodoma, pamoja na waimbaji kutoka Dar es Salaam, ambao watajulikana baadaye.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: