Rome, Itali
Juhudi kubwa zinahitajika kufanyika katika nchi za Afrika pamoja na dunia nzima ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuipa kipaumbele mikakati, sera na programu za kuimarisha sekta hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume aliyasema hayo wakati alipokuwa akitoa hutoba yake katika Mkutano wa Wakuu wa nchi na serikali kuhusu usalama wa chakula duniani na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na matumizi ya nishati inayotokana na mazao ya kilimo, unaofanyika mjini Rome nchini Itali kuanzia tarehe 3-5.

Dk. Karume alisema kuwa hatua mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa na Tanzania pamoja na nchi nyengine za Afrika katika kukabiliana na changamoto hiyo kwa hivyo ipo haja ya kuchukuliwa hatua za makusudi kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema kuwa athari kubwa zimekuwa zikijitokeza katika nchi za Afrika pamoja na dunia nzima kwa jumla ikiwa ni pamoja na kushuhudia uhaba wa chakula na kujitokeza kwa ongezeko la bei ya mafuta kutokana na mfomo wa biashara ya chakula.

Akihutubia mkutano huo, Rais Karume alieleza kuwa katika nchi za Afrika zaidi ya watu milioni 100 wanakabiliwa na tatizo la njaa kwa hivyo ipo haja ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kutumia vizuri mazao ya chakula pamoja na kupata misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Alieleza kuwa iwapo hatua za makusudi hazitochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ambalo limewafanya watu masikini kuhangaika kwa ajili ya kujipatia chakula hali ambayo pia inatishia kuwepo kwa amani na utulivu ulimwenguni.

Rais Karume alisema kuwa asilimia 4 hadi 7 ya mazao yanayozalishwa duniani yanatumika kwa ajili ya kutengeneza nishati ambapo hali hii inasababisha kupunguza kiwango cha chakula kusafirishwa kwa nchi husika zinazohitajia chakula hicho.Aidha Rais Karume alizungumzia suala la biashara duniani hasa kuhusu chakula.

Kutokana na hali hiyo Rais Karume alisema kuwa ipo haja ya kutilia mkazo mapendekezo ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na matumizi ya mazao kutengeneza nishati ili yasilete athari kwa kilimo na usalama wa chakula duniani. Alitoa wito kwa nchi zilizoendelea kuzidisha utafiti ili kuanzisha vyanzo vyengine vya nishati.

"Tunatambua kuwa mazao mengi ya chakula yamekuwa yakitengenezwa nishati kwa hivyo tunatilia mkazo kuwa ni lazima kuwepo usawa wa kuhakikisha kuwa chakula cha binaadamu hakitumiki kwa taratibu zinazowaathiri watu", alisema Dk. Karume.

Alisema kuwa nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikiathiriwa na kutolingana kibiashara kunakotokana na makubaliano ya kibiashara ulimwenguni. Pia alisema kuwa sababu ambazo zimekuwa zikisababisha uhaba wa chakula sambamba na ongezeko la bei ya mafuta duniani.

Kutokana na hali hiyo, Rais Karume alisema kuwa kuna haja ya kuwekwa kwa tahadhari za makusudi kwa ajili ya kupambana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuongezwa kwa uzalishaji wa chakula kutokana na uzalishaji wa chakula barani Afrika kuwa mdogo.

Rais Karume ameyataka Mashirika ya Umoja wa Mataifa hasa Shirika la Chakula Duniani FAO, IFAD na WFP kutoa msaada wao kwa kuwasaidia wakulima mbegu za mazao, mbolea sanjari na nyenzo nyenginezo zitakazoongeza uzalishaji wa chakula.

Kwa kutilia mkazo kilimo cha umwagiliaji maji kuna vitu muhimu ambavyo vinaweza kukiimarisha kilimo na kukiweka kuwa kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha, uimarishaji wa miundombinu, soko pamoja na kuwepo kwa mipangilio mizuri ya mavuno.
"Kwa hivyo kuna haja kwa Washirika wa Maendeleo sambamba na Taasisi za Fedha za Kimataifa kuyapa kipaumbele maeneo haya muhimu ili uzalishaji katika Bara la Afrika uzidi kuimarishwa na kushamiri kwa lengo la kupambana na uhaba wa chakula ambao hatimae husababisha njaa", alisema Dk Karume.

Rais Karume alieleza kuwa ufumbuzi na malengo ya muda mrefu wa sekta ya kilimo katika nchi za Afrika ni kuongeza uzalishaji ambapo pia mafanikio na maendeleo ya kilimo barani Afrika yanahitaji msaada wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba yake hiyo Rais Karume alitoa shukurani zake kwa lengo na madhumuni ya mkutano huo na kutoa pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu wa FAO Dk. Jacques Diouf kwa kufanikisha mkutano huo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa nchi mbali mbali duniani wakiwemo Maraisi wa nchi za Afrika ambao walieleza haja ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Chakula Duniani FAO, kuimarisha juhudi zinazochukuliwa duniani za kuendeleza kilimo ikiwa ni pamoja na zinazochukuliwa katika Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa FAO Dk. Jacques Diouf alieleza kuwa Mkutano chimbuko la mkutano huo ni hali ya sasa ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuongezeka kwa bei za mafuta duniani ambapo kumechochea ongezeko la matumizi ya mazao ya kilimo katika uzalishaji wa mafuta.

Alieleza kuwa umuhimu wa mkutano huo unatokana na hali ya sasa ya tatizo kubwa la upungufu wa chakula na kupanda sana kwa bei za vyakula duniani ambako kumechangiwa na sabababu mbali mbali.

Miongoni mwa mapendekezo ya viongozi hao wa nchi waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa chakula ikiwa ni pamoja na nchi kuhakikisha zinakuwa na rasilimali watu, fedha kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vya kukabiliana na njaa na uzalishaji mdogo wa chakula.

Rais Karume pamoja na viongozi wa nchi mbali mbali waliohudhuria mkutano huo walialikwa chakula rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa FAO Dk. Deouf ambapo pia nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Shadya Karume alialikwa chakula rasmi na Mke Mkurugenzi huyo.
Habari kwa hisani Rajab Mkasaba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: