RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE AMANI ABEID KARUME, AKITUNUKIWA SHAHADA YA UDAKTARI WA SHERIA NA RAIS WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA SOUTH CAROLINA UNIVERSITY, NCHINI MAREKANI DR. LEONARD MC INTYRE, (KUSHOTO) VIWANJA WA CHUO HICHO JUZI.
RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE AMANI ABEID KARUME AKISALIMIANA NA VINGOZI WAKUU WA CHUO CHA SOUTH CAROLINA BAADA YA KUWASILI CHUONI HAPO.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Amani Abeid Karume, ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Sheria, (Honorary Doctorate of Laws) ya Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina, Marekani.
Sherehe hii ilifanywa katika viwanja vya Chuo Kikuu hicho, wakati wa mahafali ya kuwatunuku Digrii wahitimu mbali mbali ambapo maelfu ya wananchi wa mji wa Columbia, Orangeburg na maeneo ya karibu na chuo hicho walihudhuria.

Rais wa Chuo Kikuu cha Taifa South Carolina, Dr. Leonard McIntyre alimkabidhi Rais Karume shahada hiyo ya heshima, alisema, Baraza la Wadhamini la Chuo Kikuu hicho, limeamua kumtunukia Rais Karume heshima hiyo kutokana na kutambua na kuheshimu uongozi wake bora.

Dr. McIntyre amesema kuwa wadhamini wa chuo hicho wamevutika na uongozi wa Rais Karume katika kuleta maendeleo makubwa katika sekta za elimu, afya, ustawi wa jamii, pamoja na kuendeleza uchumi wa Zanzibar na juhudi na mikakati yake katika kuondosha umasikini.

Rais Amani Karume akielezea furaha na kutoa shukurani zake kwa uongozi wa chuo hicho alisema kuwa heshima kubwa aliyopewa, haikuwa ya peke yake bali ni uthibitisho wa heshima inayopata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Akiwa mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu katika mahafali hayo, Rais Karume alitoa furaha na shukurani zake kwa Rais wa Chuo Kikuu cha South Carolina, Bodi ya Wadhamini na Shirika la Maendeleo la Marekani USAID kwa kuanzisha na kuendeleza mradi wa pamoja wa kutunga na kuchapisha vitabu vya Sayansi kwa mfumo wa mashirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina, SUZA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

"Tunatoa shukurani nyingi kwa Chuo Kikuu cha South Carolina na wahusika wote kwa kushiriki kikamilifu katika utungaji wa vitabu vya Sayansi kwa skuli za Zanzibar, alieleza Rais Karume.

"Katika hotuba yake, Rais Karume alieleza juu ya changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini na namna ya kuzitatua. Alihimiza mashirikiano ya kimataifa katika kufikia malengo mbali mbali yanayowekwa; "

Kwa mashirikiano ya pamoja, tunaweza kugeuza Dira kuwa hali halisia" alieleza Rais Karume. Alitilia mkazo uendelezaji wa ushirikiano huo. Aidha, Rais Karume aliwaasa wahitimu wa Chuo

Kikuu cha South Carolina, kukabiliana na changamoto za maisha duniani wakiwa na mtazamo mpya kufuatia taaluma waliyoipata chuoni hapo. Aliwapongeza kwa kuwa na bahati ya kuwa wahitimu wa chuo kikubwa, chenye sifa na kutambulikana kimataifa cha South Carolina.

Aliwataka kuwa mabalozi wazuri wa chuo hicho na kutumia waliyojifunza kuendeleza maadili mema katika jamii. Wahitimu waliohitimu Mahafali hayo walielezea furaha yao kwa mahafali hiyo kupata baraka ya kuwepo kwa mgeni maalum, Rais Amani Abeid Karume wa Zanzibar. Zaidi ya wanachuo 460 walikabidhiwa shahada mbali mbali jioni hiyo kufuatia kufaulu katika masomo yao.

Mnamo Januari mwaka huu, uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina ulitembelea Zanzibar na kukabidhi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar vitabu vya Biolojia kwa ajili ya skuli za Sekondari. Vitabu hivyo vimetungwa kwa mashirikiano na watalaamu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha South Carolina, SUZA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Mahafali hayo pia yalihudhuriwa na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Shadya Karume, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Ombeni Sefue, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani pamoja na maafisa waandamizi waliofuatana na Rais katika ziara yake nchini Marekani.

Rais Karume, mkewe na aliofuatana nao walitembelea mji wa kitalii wa Charlestone ambapo walishiriki katika chakula cha mchana kilichoandaliwa na Meya wa Mji huo, Mhe. Paul Miller.

Rais Karume na aliofuatana nao wataondoka South Carolina jana kuelekea Washington DC ambapo atakutana na viongozi mbali mbali wakiwemo Makamo wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, USAID, kuhutubia katika Chuo Kikuu cha George Washington na kuzungumza na Watanzania wanaoishi Washington Marekani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: