Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bw. Philip Parham amesema nchi yake iko tayari kusaidia Tanzania katika harakati za kupambana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.

Amesema miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele ni nyanja ya elimu kwa umma ili wananchi waweze kuelewa maana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

Balozi ameyasema hayo akiongea na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk. Batilda Burian alipomtembelea ofisini kwake jijini leo kwa lengo la kujitambulisha pamoja na kujadiliana naye masuala kadhaa ya mazingira nchini.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dk. Batilda Burian amesema Tanzania kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi hivi sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuzama kwa Visiwa, mfano Kisiwa cha Maziwe huko Tanga, kuyeyuka kwa Barafu katika Mlima Kilimanjaro.

Amebainisha kuwa ili kuhimili mabadiliko hayo ofisi yake imeshaanda Mpango wa Taifa wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi (NAPA) ili kupunguza athari zinazosababishwa na hali hiyo.

Waziri amesema ili kufanikisha programu hiyo ameiomba serikali ya Uingereza kufadhili uchapishaji wa mkakati wa Program ya Taifa ya Kuhimili mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwa ni pamoja na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi kupata fursa ya kuisoma na kuelewa.

Dk. Burian amemwomba Balozi huyo kupitia programu yao ya muda mfupi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi wasaidie katika kujenga uwezo kwa sekta na Wataalamu wanaoshughulika na maafa mfano Mamlaka ya Hali ya Hewa, Idara ya Mazingira, Idara ya Maafa na Vituo vya Tafiti pamoja na kuziwezesha kiteknolojia ili sekta hizo ziweze kukabiliana na matukio mbalimbali yanayotokea.

Aidha, Dk. Burian ameliagiza Baraza la Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wadau wengine kuunda timu haraka kwa ajili ya kufanya Risk Assessiment katika machimbo ya madini wakianza na eneo la machimbo ya vito vya tanzanite huko Mererani kulikotokea maafa ili waweze kuandaa Mkakati wa muda mrefu wa kufanya Environmental Auditing kwa Maeneo yanayozunguka machimbo hayo. Pia NEMC imetakiwa kuja na mapendekezo ya nini kifanyike katika mkakati wa muda mrefu na kuainisha maeneo yaliyoko kwenye hatari zaidi “Risk Areas”

Balozi Parham katika ziara yake ya utambulisho kwa Waziri aliambatana na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza inayopambana na kupiga vita umaskini duniani Bw. Roy Trivedy.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: