*** Aitaka Afrika kuongeza sauti yake kuhusu bei za mafuta na chakula

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) amelionya Bara la Afrika kuamka na kuanza kutafuta njia za kukabiliana na tatizo la bei kubwa za chakula na mafuta duniani.

Akizungumza katika sherehe ya makabidhiano ya uongozi wa Kamisheni ya AU kwenye makao makuu ya AU mjini Addis Ababa , Ethiopia , Rais Kikwete amesema kuwa bei hizo ndiyo changamoto mpya na kubwa zaidi kwa wakati huu ya Afrika na uongozi mpya wa Kamisheni ya AU.

Katika makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Kamisheni iliyomaliza muda wake, Alpha Omar Konare wa Mali amekabidhi madaraka kwa Mwenyekiti mpya, Jean Ping wa Gabon .

Kabla ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamisheni ya AU, Konare alikuwa Rais wa Mali wakati Ping alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Gabon .

Rais Kikwete ambaye alikuwa Mwenyekiti na msimamizi mkuu wa sherehe hiyo, amewaambia mamia ya watu waliohudhuria sherehe hizo:

“Kamisheni mpya inaingia katika madaraka wakati Afrika inakabiliwa na changamoto mbili kubwa sana na mpya. Changamoto hizo ni bei kubwa vya chakula na bei kubwa ya mafuta.”

Ameongeza: “ Kama changamoto hizo hazikukabiliwa haraka na ipasavyo zitamaliza kabisa chumi nyingi za Afrika, ambazo kwa bahati nzuri zimekua zinakua vizuri katika miaka michache iliyopita.”

Rais amesema kuwa iko hatari kubwa kweli kweli kuwa mafanikio yote ya kiuchumi ambayo yamepatikana katika Afrika yatamezwa na bei hizo kubwa za chakula na mafuta.

“Katika hili, sauti ya Afrika inatakiwa kusikika na uongozi katika jambo hili unatakiwa kuonekana dhahiri,” amesema Kikwete.

Mbali na changamoto hiyo ya bei za chakula na mafuta, Rais Kikwete pia aliorodhesha changamoto nyingine zinazolikabili Bara hili kwa kadri uongozi wa Kamisheni unavyotoka mikononi mwa kundi moja kuingia kwa kundi jingine, kwa amani.

Changamoto nyingine ambazo zitaukabili uongozi huo mpya, kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni migogoro katika Darfur , Chad , Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Somalia . “Pia hali za DRC, Burundi na Zimbabwe zinahitaji uangalizi wa karibu wa AU.”

Rais Kikwete pia ameutaka uongozi huyo mpya kuongoza mjadala kuhusu utekelezaji wa Azimio la Accra kuhusu mwelekeo wa baadaye wa AU na mapendekezo ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja ya Afrika na pia kuongoza mjadala kuhusu tathmini ambayo imefanywa kuhusu AU yenyewe.

Hata hivyo, Rais ameongeza: “Pamoja na kwamba changamoto ni kubwa na ni nyingi, lakini sina shaka kwamba taasisi yetu iko katika mikono yenye uwezo na yenye uzoefu ya Jean Ping, Makamu wake Erastus Mweche na makamishna wengine wapya.”

Ameongeza kuwaambia viongozi hao wapya“ Hili linanifanya niwe na imani. Kwa niaba ya Serikali na Watu wa Afrika nawaombeni kusimama kupambana na changamoto hizi. Najua mtaifanya kazi hiyo, kwa ufanisi.”

Rais Kikwete pia ameelezea baadhi ya mafanikio ya AU katika kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwake kutoka taasisi ya zamani ya Organisation of African Unity (OAU).

“AU sasa imejijenga kama taasisi ya kikanda inayoaminika na inayotegemewa kwenye uwanja wa kimataifa. Matokeo yake ni kwamba AU imejenga ushirikiano wa nguvu na Umoja wa Ulaya, Japan, China, Korea Kusini, Nchi za Marekani Kusini na hivi majuzi na India. Tunatarajia kuwa uongozi mpya utaimarisha mahusiano hayo na kujenga mpya.”

Rais Kikwete pia amemwagia sifa kemkem Konare kwa uongozi wake wa AU. “Profesa Alpha Omar Konare ni mtu wa mawazo mengi na makubwa. Visheni ya AU ya mwaka 2015, kimsingi, ni matunda ya ubongo wake; matokeo ya bongo yake inayochemka na visheni. Ndani ya moyo wa Afrika, kuna sehemu maalum ya Afrika, na watu wake. Ni Mwafrika kweli kweli kwenye sifa ambazo ni ngumu kuzielezea kwa ufasaha wa kweli kweli.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Profesa Alpha Konare ni mtoto wa kweli kweli wa udongo wa Afrika ambaye ameitumia taasisi yetu vizuri sana na kwa ari, moyo mkubwa wa kujitolea na imani kubwa. Profesa Konare siku hizo amekuwa chanzo cha ari kwetu sote.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

6 comments:

  1. Wow! Finally I got a web site from where I be able to truly
    get valuable information regarding my study and knowledge.

    ReplyDelete
  2. Keep on writing, great job!

    ReplyDelete
  3. I am always looking online for articles that can aid me.
    Thx!

    ReplyDelete
  4. I always was concerned in this subject and stock still
    am, thankyou foor posting .

    ReplyDelete
  5. I really like your writing style, superb information, thank you for putting up :
    D.

    ReplyDelete
  6. Hi there, I enjoy reading through your article.
    I wanted to write a little comment to support you.

    ReplyDelete